Absa Tanzania yazindua ripoti ya viashiria vya masoko ya fedha Afrika

Dar es Salaam. Benki ya Absa Tanzania imezindua rasmi Ripoti ya Viashiria vya Masoko ya Fedha Afrika 2025 kwa Tanzania.

Uzinduzi huo umefanyika leo Alhamisi, Januari 29, 2026 jijini Dar es Salaam, ukiwakutanisha wadau wakuu wa sekta ya fedha. Mbali na uzinduzi, hafla hiyo ilijadili pia mwelekeo wa masoko ya fedha barani Afrika na nafasi ya Tanzania katika taswira hiyo.

Akizungumza katika hafla hiyo kwa niaba ya Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba, Mkurugenzi wa Masoko ya Fedha kutoka BoT, Emmanuel Akaro amesema ripoti hiyo ni chombo muhimu cha kutathmini sera na kupima maendeleo ya masoko ya fedha, huku akirejea nafasi ya Tanzania kama ilivyoainishwa kwenye ripoti hiyo.

“Ripoti ya Absa ya Viashiria vya Masoko ya Fedha Afrika inatoa mwanga muhimu kuhusu hatua ambazo Tanzania imepiga katika kuimarisha masoko yake ya fedha,” amesema Akaro.

Amesema ripoti hiyo inaonesha maeneo ambayo Tanzania imefanya vizuri, hususan katika uthabiti wa uchumi kwa jumla na uwazi wa masoko.

Hata hivyo, Akaro amesema pia imeainisha maeneo yanayohitaji maboresho zaidi, ikiwamo kuongeza ushiriki wa wawekezaji wa ndani, kuendeleza mifuko ya pensheni na kuimarisha mifumo ya kisheria na kitaasisi.

Amesisitiza kuwa dhamira ya Serikali ni kuendelea kutekeleza mageuzi yatakayoongeza ukubwa wa masoko, kupanua wigo wa vyombo vya kifedha na kuifanya mifumo ya fedha ya Tanzania kuendana na viwango vya kimataifa.

Uzinduzi huo pia uliwakutanisha wadau kutoka Benki Kuu ya Tanzania, Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Wizara ya Fedha, Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), viongozi wa sekta ya umma na binafsi, wajumbe wa Bodi, Wakurugenzi na Menejimenti ya Juu ya Benki ya Absa Tanzania.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Absa Tanzania, Obedi Laiser, amesisitiza umuhimu wa kuwa na masoko ya fedha imara na yenye uwazi katika kuchochea ukuaji endelevu wa uchumi.


“Ripoti ya Absa ya Viashiria vya Masoko ya Fedha Afrika ilianzishwa ili kutoa tathmini huru na ya kitaalamu kuhusu mwelekeo wa masoko ya fedha barani Afrika,” amesema Laiser.

Amesema kadri uchumi wa Afrika unavyoendelea kukua na kubadilika, masoko ya fedha yenye kina, uwazi na ufanisi ni nguzo muhimu katika kukusanya mitaji, kusaidia biashara na kuwezesha maendeleo endelevu.

Wakati wa uwasilishaji wa matokeo ya Ripoti ya 2025, wasemaji wakuu kutoka Absa Group wameeleza kuwa licha ya changamoto za uchumi wa dunia, masoko mengi ya fedha barani Afrika yameonesha maendeleo ya kutia moyo. Mageuzi katika uwazi, mifumo ya udhibiti, utofauti wa bidhaa za kifedha na ubunifu wa kidijitali yalitajwa kuwa miongoni mwa nguzo muhimu za kuimarisha ustahimilivu wa masoko hayo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Benki ya Absa Tanzania, Lulu Ngwanakilala, akimwakilisha Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa benki hiyo, Paul Makanza, ameipongeza mijadala iliyofanyika akisema inaonesha kukomaa kwa mazungumzo kuhusu maendeleo ya masoko ya fedha nchini.

“Ingawa Ripoti ya Absa ya Viashiria vya Masoko ya Fedha Afrika 2025 inaonesha kuwa hatua zimepigwa, pia inatukumbusha umuhimu wa ushirikiano endelevu kati ya serikali, wasimamizi, taasisi za kifedha na sekta binafsi ili kuziba pengo lililobaki na kujenga masoko ya fedha jumuishi zaidi,” amesema Ngwanakilala.

Amesema dhamira ya Benki ya Absa Tanzania ni kuendelea kushirikiana kwa karibu na wadau wote katika kusaidia mageuzi yanayokuza uwazi, uimara na uwekezaji wa muda mrefu katika sekta ya fedha.