Rais ateua wanne, yupo Naibu Gavana BoT

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amefanya uteuzi wa viongozi wanne akiwemo Naibu Gavana, Utawala na Udhibiti wa Ndani wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Hiyo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Alhamisi, Januari 29, 2026 na Katibu Mkuu Kiongozi, Dk Moses Kusiluka na kusainiwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Bakari Machumu.

Katika uteuzi huo, Dk Rahma Salim Mahfoudh ameteuliwa kuwa Naibu Gavana, Utawala na Udhibiti wa Ndani wa BoT akihitimisha safari ya Julian Raphael ya siku 3,656 ndani ya benki hiyo.

Dk Rahma Salim Mahfoudh aliyeteuliwa kuwa Naibu Gavana, Utawala na Udhibiti wa Ndani wa BoT.



Raphael anapata mrithi leo Januari 29, 2026 ikiwa ni baada kukalia kiti hicho kwa takribani muongo mmoja tangu alipoteuliwa Januari 26, 2016 na aliyekuwa Rais wa awamu ya tano, John Magufuli.

Kabla ya uteuzi huo, Raphael alikuwa Katibu Mkuu, Wizara ya Biashara na Viwanda, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na alikalia kiti hicho akiziba nafasi iliyoachwa wazi na Juma Reli ambaye alimaliza muda wake Julai 12, 2015.

Katika hatua nyingine, Dk Ladislaus Chan’ga aliyekuwa akihudumu kama Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ameteuliwa rasmi kukalia kiti hicho.

Dk Chang’a alikalia kiti hicho kama Kaimu Mkurugenzi tangu mwishoni mwa mwaka 2022 baada ya aliyekuwa Mkurugenzi wa TMA, Dk Agnes Kijazi kustaafu.

“Pia Rais amemteua Profesa Muhammad Kambi kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Hospitali ya Taifa Muhimbili akichukua nafasi Dk Ellen Mkondya Senkoro ambaye amemaliza muda wake,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Katika hatua nyingine, Rais Samia amemteua Balozi Wilson Masilingi kuwa Mwenyekiti wa Taasisi ya Uhamasishaji Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali za Madini, Mafuta na Gesi Asilia Tanzania (TEITI).

Balozi Masilingi anachukua nafasi ya Ludovick Utouh ambaye amemaliza muda wake.