Tiseza yatua Shinyanga kuhamasisha uwekezaji

Shinyanga. Katika kuhamasisha uwekezaji wa ndani, Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi Tanzania (Tiseza) imetua mkoani Shinyanga kwa lengo la kuhakikisha uwepo wa miundombinu ambayo itaondoa changamoto kwa mwekezaji.

Hayo yamebainishwa leo Januari 29, 2026 na Meneja Uhamasishaji Uwekezaji wa Ndani kutoka Tiseza, Felix John, baada ya ukaguzi wa uwekezaji katika sekta ya elimu, katika shule ya msingi na sekondari Savanah.

“Serikali inaendelea kuweka mazingira rafiki kwa mwekezaji kwa kuweka miundombinu ambayo itaondoa changamoto ya uwekezaji kama maji, umeme, barabara na mawasiliano katika maeneo yote ya uwekezaji,” amesema John.

Mkuu wa Shule hiyo, Wema Kanika ameeleza kuwa uwekezaji uliofanyika katika shule hiyo unahudumia wanafunzi 936 kuanzia ngazi ya elimu ya awali hadi kidato cha sita.

“Uwekezaji umechukua ukubwa wa eneo la ekari 80 na kuna wanafunzi 512 wa elimu ya awali na msingi, pia, wanafunzi 424 wa kidato cha kwanza hadi cha sita na wafanyakazi 50 ambao wanaishi ndani ya shule huku tukiwa na ng’ombe kwa ajili ya nyama na maziwa kwa wanafunzi, visima vya maji pamoja na miti ya matunda,” amesema Wema.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita ameeleza kuwa katika mkoa huo kuna maeneo mawili makubwa ambayo yametengwa kwa ajili ya uwekezaji wa kiuchumi.

“Kwa mkoa huu kuna maeneo mawili ambayo ni Buzwagi pamoja Nyanshimbi na hakuna eneo la uwekezaji ambalo halina miundombinu ya uwezeshaji, pia, kuna bandari kavu ambayo itachochea maendeleo ya kiuchumi katika wananchi wa Shinyanga,” amesema Mhita.