Uume uliokatwa waunganishwa tena Ethiopia

Ethiopia. Timu ya madaktari bingwa kutoka Ethiopia imefanikiwa kuunganisha uume wa kijana aliyejikata mwenyewe usiku wa manane, baada ya kufanyiwa upasuaji maalumu uliodumu kwa saa saba.

Kwa mujibu wa taarifa ya BBC, madaktari hao kutoka Hospitali ya ALERT jijini Addis Ababa, nchini Ethiopia, walifanya upasuaji huo kwa mafanikio licha ya changamoto ya muda uliopita tangu jeraha litokee.

Upasuaji huo ulihusisha kuunganisha upya mishipa ya damu na neva, kurekebisha mfumo wa mkojo pamoja na kurejesha tishu unganishi, hatua iliyowezesha kurejesha uhai wa kiungo hicho.

Akizungumza kuhusu tukio hilo, Dk Abdurrezak Ali amesema uume huo ulikuwa umekatwa kabisa na hivyo kukosa mzunguko wa damu na oksijeni kwa takribani saa tisa kabla ya mgonjwa kufikishwa hospitalini.

“Tulifanya uamuzi wa kufanya upasuaji kwa sababu tuliamini bado kulikuwa na uwezekano wa kuunganisha uume huo, kulingana na muda uliopita tangu jeraha litokee,” amesema Dk Ali.

Ameeleza kuwa utafiti wa kitabibu unaonesha mishipa ya damu na neva kwenye uume inaweza kuendelea kuishi hadi saa 16 baada ya kukatwa, kutokana na ukweli kwamba kiungo hicho hakina misuli.

Madaktari hao wamesema kwa sasa mgonjwa anaendelea vizuri na hali yake inaonesha nafuu.

Wanatarajia aanze kukojoa kwa kawaida ndani ya wiki tatu, huku kurejea katika shughuli za kujamiiana kukitarajiwa kuchukua takribani miezi mitatu.

Tukio hilo limeelezwa kuwa moja ya mafanikio makubwa ya kitabibu, likionesha maendeleo ya upasuaji wa kisasa katika kurejesha viungo vilivyokatwa.