Lugola ahoji uhuru wa Polisi na DPP, awashukia ‘machawa’

Dodoma. Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola, amesema ili kumaliza mafisadi na wabadhirifu nchini na kuipata ‘Tanzania mpya’, ni lazima vyombo vya dola, kwa maana ya Jeshi la Polisi na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), viwe huru.

Mbali na hayo, amesema watu aliowaita ‘machawa’ ndiyo wameifikisha nchi hapa, akitaka wabunge wawe huru wasibanwe, ikiwemo na vikao vya chama chao cha CCM, ili wawashughulikie kwa lengo la kumsaidia Rais Samia Suluhu Hassan.

Lugola, mbunge wa Mwibara, Mkoa wa Mara, ametoa kauli hiyo siku moja baada ya mbunge wa mwingine wa chama hicho wa Gairo, Ahmed Shabiby, kueleza kuwa Tanzania bado ina mafisadi wengi na wanakula kuliko inavyodhaniwa.

Shabiby alikwenda mbali zaidi kwa kusema yuko tayari kuwataja kwa majina yao kama itahitajika, huku akiwataka wasaidizi wa Rais Samia kumsaidia ipasavyo na kuachana na mipango ya kujipanga na urais mwaka 2030.

Wabunge hao wameibua hoja za ufisadi huo bungeni wakati wakichangia hotuba ya Rais Samia aliyoitoa alipolizindua Bunge la 13, Novemba 14, 2025. Shabiby alitoa kauli hiyo jana na leo Alhamisi, Januari 29, 2026, Lugola ameizungumza tena kwa msisitizo.

Mchango wa Lugola, kwa sehemu kubwa, ulikuwa ukikatishwa na kelele za shangwe na ugongaji wa meza kutoka kwa wabunge wengine, alisifiwa hata alipomaliza.

Mwenyekiti wa Bunge, Najma Giga, aliwaeleza wabunge sababu za kuruhusu makofi, akisema kuwa licha ya kutokuwepo kwa kanuni, aliona kulikuwa na ukweli ndani yake.

Lugola, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani (Julai 1, 2018 hadi Januari 23, 2020) wakati wa utawala wa awamu ya tano wa hayati John Magufuli, alianza kuchangia kwa kuelezea jinsi Rais Samia alivyokuwa akilizindua Bunge na kuonesha kukerwa na ufisadi na ubadhirifu, huku akiomba Bunge limsaidie.

Katika mchango wake, Lugola amesema ili matamanio ya Rais Samia yafikiwe: “Lazima tuboreshe kundi la machawa. Machawa ni kundi hatari, machawa ndimo wanajificha mafisadi, machawa ndimo wanajificha wabadhirifu, na bila kushughulika na machawa, ambamo ndimo kichaka wanamojificha, tukichome moto na kukifyekelewa mbali.”

Ili kuhakikisha hilo linafanikiwa, Lugola amesema Serikali inapaswa kuhakikisha mihimili ya dola, kwa maana ya Bunge, Serikali na Mahakama, inakuwa ni mihimili huru, ikiwemo mijadala ya ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

“Bunge linakuwa huru. Leo, kwa mfano, tukiletewa taarifa ya CAG, lazima tuijadili kwa uhuru na kwa upana ili tushughulikie wabadhirifu. Tutakapoweka maazimio, lazima yaende yakaheshimiwe na Serikali, na Serikali iyatekeleze. Bila hivyo, hatutafanikiwa,” amesema Lugola.

Katika uhuru wa Mahakama, Lugola amesema: “Mahakama iwe huru. Wakipelekewa watu waliofanya uhalifu, watendewe haki ya kuhukumiwa ili waogope fedha za Serikali.”

Lugola, aliyewahi kutamba kama mmoja wa wapambanaji wa ufisadi kwenye Bunge la 11 akiwa na aliyekuwa mbunge wa Ludewa, marehemu Deo Filikunjombe, amesema: “Vyombo vya uchunguzi vya dola navyo viwe huru. Mwendesha mashtaka lazima awe huru, lazima Polisi wawe huru ili wachunguze mafisadi papa wapelekwe mahakamani, kuliko kupelekwa vidagaa. Vimijusi vidogovidogo ndivyo vinavyokwenda mahakamani.”

Mbunge huyo ameendelea kusema Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya nayo inapaswa kuwa huru ili ishughulikie mambo hayo, na bila kufanya hivyo, maono ya Rais Samia hayawezi kufikiwa.

“Rais alisema atatoa ushirikiano kwa Bunge na sisi Bunge tumpe ushirikiano. Haya mambo ya kuleta masuala muhimu ambayo wanajifanya ni machawa kumbe ni mafisadi papa, siyo vidagaa.

“Mama anataka kuinyoosha nchi, lakini uchawa unakuwa mwingi, hao ndiyo madalali wa kuhujumu uchumi, lazima tuponye nchi hii kwa kuelezana ukweli,” amesema Lugola na kuongeza;

“Sisi kule Tarime tunasema, vita ni vita mura. Hii tabia ya kufunika kombe mwanaharamu apite haipo. Tutaelezana ukweli halisi ili tumsaidie mheshimiwa Rais,” amesema.

Akiendelea kuchangia, Lugola amesema: “Na huu mtindo wa kuitana itana kwenye party caucus (kamati za vyama) ndani ya Bunge, halafu mnashindwa kujadili taarifa ya CAG, kumbe kuna ufisadi hii nayo haiwezekani.”

Nje ya Bunge, Mwananchi limemtafuta Lugola kupata ufafanuzi wa kauli zake, ambapo amesema kumekuwepo na utaratibu wa vyama vya siasa kuwaita na kuzungumza na wabunge wao pale inapobidi, hasa kwenye michango inayogusa maslahi ya nchi na wananchi wake.

Amesema siyo utamaduni mbaya, bali usiwe utamaduni wa kuwafunga watu midomo, akisisitiza kuwa lazima chama kiisimamie Serikali maana ndicho chenye uchungu na mahangaiko ya jinsi kilivyosaka dola.

“Kwenye hizo party caucus siyo mbaya, ule ni utamaduni wa kila chama duniani, lakini kuna wakati muwe mnaangalia inawezekanaje taarifa ya CAG ikipelekwa pale, kama nilivyosema, halafu utakuta michango ya wabunge inaanza kuyumbayumba.

“Hapo jiulize kuna nini. Nawasihi wabunge wenzangu hebu tusimame kumsaidia Rais, na hiyo ndiyo maana yangu,” amesema.

Kuhusu uhuru wa vyombo vya kiuchunguzi na Polisi, amesema halina ubishi kwani wachunguzi wamekuwa wakipokea kesi za kila aina na wakati mwingine wanafanya kazi zao kwa weledi, lakini inashangaza kesi kubwa hazikamiliki uchunguzi wake.

“Huko nako kuna shida ya kuingiliwa wakati mwingine. Wanapokea kesi za kuku hadi papa, lakini hawa papa wakati mwingine kesi zao haziendi popote, na zikienda mahakamani zinaahirishwa mara kwa mara,” amesema Lugola.

Amesema vyombo hivyo vikiachwa vifanye kazi yao kwa uhuru, vitamsaidia Rais kwa kiasi kikubwa, na Taifa litasimama katika mstari ambao mkuu wa nchi anataka kupitia hotuba yake.

Amesema Tanzania haitafanikiwa, hata ikitumia mamilioni ya fedha, endapo hakutakuwa na uwajibikaji wa kweli, utawala wa sheria na mapambano ya dhati dhidi ya rushwa, uzembe na ufisadi.

Katika mchango wake bungeni, Lugola amegusia mambo ya jimboni kwake, akitaja uvuvi haramu kuwa umeendelea kuwa kidonda kisichopona katika Ziwa Victoria, ukilikosesha Taifa mabilioni ya mapato kutokana na upotevu wa samaki wanaovunwa kinyume cha sheria.

Amesema wakati Serikali ikiwekeza fedha nyingi katika ulinzi wa rasilimali za maji na kutoa mikakati ya kukuza uvuvi endelevu, vitendo vya wachache wanaolindwa na rushwa vinahujumu juhudi hizo na kuifanya nchi ionekane kama inashindwa kudhibiti rasilimali zake yenyewe.

“Uwajibikaji na utawala wa sheria ndivyo vitakavyotufikisha tunapotaka kwenda. Bila hivyo, hata tukitumia mabilioni ya fedha, hatuwezi kufanikiwa,” amesema Lugola, akisisitiza mapambano ya kweli lazima yaelekezwe katika kupambana na rushwa, uzembe na ufisadi uliokithiri katika baadhi ya sekta.

Kwa upande wake, mbunge wa Kisarawe (CCM), Dk Seleman Jafo, amesema ni wajibu wa kila Mtanzania kulinda amani kwa wivu mkubwa, kwa kuwa nchi ikiharibika hakuna namna ya kuirudisha.

Jafo ametolea mfano baadhi ya mataifa ambayo amani imeharibika, hivyo akasisitiza vijana kusimama imara katika kuilinda Tanzania kwa wivu mkubwa na ajenda ya amani isiwe na mjadala kwao.

‘Bunge linaweza kudhibiti’

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga, amesema Bunge lina mamlaka ya kuisimamia Serikali na kuhakikisha wote wanaobainika kuhusika na vitendo vya ufisadi wa mali za umma wanawajibishwa.

“Bunge lina meno ya kuisimamia Serikali na lina uwezo wa kuhakikisha wale wote wanaohusika na ufisadi wanawajibishwa endapo litaamua kufanya hivyo,” amesema Henga.

Amesema licha ya Bunge kutunga sheria ya kanuni ya maadili ya watumishi wa umma, utekelezaji wake umekuwa dhaifu, huku masuala ya uwajibikaji yakifanyika kwa usiri mkubwa.

“Sheria ya maadili imetungwa, lakini haitekelezeki. Mambo mengi yanafanyika kwa usiri mkubwa, mali zinatangazwa kwa siri na wananchi hawajui,” amesema.

Henga amesema ripoti za CAG zimekuwa zikibaini kasoro na kutoa mapendekezo kila mwaka, lakini changamoto hizo zinaendelea kujirudia kuanzia Serikali Kuu hadi Serikali za mitaa.

“Taarifa za CAG zikienda bungeni hazifanyiwi kazi. Hatujawahi kusikia aliyekamatwa, wanazungumza tu kana kwamba wanajifurahisha, ilhali Bunge lina uwezo wa kusimamia,” amesema.

Amesema Katiba inalipa Bunge mamlaka ya kuisimamia Serikali na kuhakikisha wahusika wanafikishwa mahakamani.

“Mahakama ya mafisadi ipo, swali, tatizo liko wapi kama si kwenye uwajibikaji?” amesema.

Kwa upande wake, mtaalamu wa uchumi, Profesa Anna Sikira, amesema kupuuzwa kwa ripoti na ushauri wa CAG kumechangia ufisadi kuendelea kuota mizizi miongoni mwa watumishi wa umma.

Amesema Serikali na Bunge zinapaswa kuacha kulaumiana na badala yake kuja na suluhu ya kudumu.

“Hatutaki kuona Serikali na Bunge wakilalamika, tunataka waeleze suluhu kwa sababu sheria na vyombo vya uwajibikaji vipo,” amesema.

Profesa Sikira amesema Bunge lina wajibu wa kuisimamia Serikali kwa kuhakikisha idara zote zilizoainishwa katika ripoti za CAG zinachukuliwa hatua.

Naye Profesa wa Uchumi, Samuel Wangwe, amesema kauli za Shabiby kuhusu rushwa ni za msingi na zinapaswa kusemwa hadharani.

“Tatizo la ufisadi halikusikika hata kwenye kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2025, jambo linaloonesha halikutiliwa uzito unaostahili,” amesema.

Amesema vita dhidi ya rushwa lazima itangazwe wazi na kuongozwa na utashi wa kisiasa.

“Vyombo vya kupambana na rushwa vipo, lakini hili ni suala la kisiasa linalohitaji utashi wa kisiasa wa wazi kupinga rushwa,” amesema.

“Wabunge lazima wawe mstari wa mbele kukabiliana na rushwa, waondoe uoga na wasijifiche nyuma kwa sababu wananchi hawataki rushwa,” amesema.