Wakulima 90,000 Mbeya wanufaika na mbolea ya ruzuku

Mbeya. Zaidi ya wakulima 91,126 kutoka Wilaya ya Mbeya wamenufaika na mbolea ya ruzuku tani 13,140 baada ya kusajiliwa kwenye mfumo rasmi wa Serikali.

Idadi hiyo imehusisha wanawake 44,117 na wanaume 46,951 ambao walisajiliwa kati ya Oktoba 2025 na Januari 2026.

Hatua hiyo imekwenda sambamba na Serikali kutaka maofisa kilimo kutoa elimu kwa wakulima kuhusiana na matumizi bora ya pembejeo za kilimo, hususani kwa kuzingatia taarifa za Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA).

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Erica Yegella ameeleza hayo leo Alhamisi, Januari 29, 2026, wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kwa waandishi wa habari mkoani hapa.

Yegella amesema licha ya wakulima kusajiliwa kwenye mfumo rasmi wa upatikanaji wa pembejeo za ruzuku, halmashauri imezalisha miche bora ya kahawa 317,000.

“Lengo ni kuwezesha wananchi na wakulima kutotegemea kilimo cha mazoea, lakini tumetoa ruzuku ya mbegu bora za zao la ufuta kilo 500 bure sambamba na kutenga maeneo ya uzalishaji katika Kata ya Mjele,” amesema.

Amesema ili kuhakikisha wakulima wanazalisha kwa tija kubwa, Serikali itaendelea kushirikiana nao, hususani kuhamasisha wataalamu wa kilimo kuwafikia ili kutoa elimu na kufikia malengo.

Katika hatua nyingine, Yegella ameishukuru Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufanya maboresho katika nyanja mbalimbali za kijamii ndani ya siku 100 tangu aingie madarakani.

Mkulima wa Kijiji cha Iwindi, Winfrida John, amesema katika msimu huu wa kilimo, Serikali imefanya jitihada kubwa kuona wakulima wanaondokana na changamoto ya mbolea ya ruzuku kwa wakati.

“Tunaona Serikali ya awamu ya sita bado inaendelea kutushika mkono kuhakikisha pembejeo za kilimo na elimu ya uzalishaji, hususani matumizi ya mbegu bora katika uzalishaji,” amesema.

Kwa upande wake, Ofisa Kilimo wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Cuthbert Mwinuka amesema lengo la kugawa ruzuku ya miche 317,000 ya kahawa ni kuwezesha wakulima kuongeza tija kufuatia bei yake kuwa juu.

“Asilimia 100 ya miche bora ya kahawa tuliyotoa kwa wakulima tumepewa na Serikali; lengo ni kuongeza tija ya uzalishaji kwa kuzingatia kuwa sasa kilo moja inauzwa Sh13,000, jambo ambalo wakulima wamenufaika,” amesema.

Ofisa huyo amesema mkakati ni kuongeza wigo kwenye mazao ya kimkakati ambayo yataongeza kipato kwa mkulima na Serikali, ikiwemo parachichi, ufuta na kahawa kwa Mbeya Vijijini.