Serikali Yalenga Kujitosheleza kwa Mbegu na Mbolea Kupitia Uwekezaji

NAIBU Waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde (Mb) amefanya kikao na wawakilishi kutoka Chama cha Wamiliki wa Viwanda Vidogo na Wazalishaji Wadogo Tanzania (TASSIM)  chenye makao makuu jijini Dar es Salaam, kujadili fursa za uwekezaji na kuboresha ushirikiano katika tasnia ya mbolea, mbegu pamoja na viuatilifu nchini.

Kikao kimefanyika tarehe 29 Januari 2026 katika Ofisi za Wizara ya Kilimo zilizopo Mtumba jijini Dodoma, na kuhudhuriwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa TASSIM, Bw. ELIA Joseph; Mhasibu wa TASSIM, Bw. Twaha Kitongo; Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Mazao wa Wizara ya Kilimo, Bi. Yasinta Nzogela; pamoja na wawakilishi kutoka Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA); na Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC).

Pamoja na mambo mengine, Mhe. Silinde amewaeleza Wadau hao kuwa Wizara ya Kilimo itaendelea kushirikiana na wawekezaji katika masuala ya uzalishaji kwa kuwa mahitaji ya mbegu pamoja na mbolea yanazidi kuongezeka siku hadi siku kutokana na matumizi ya wakulima, hali inayofanya suala la uwekezaji kutokwepeka.  

Fursa mbali zilizopo katika uwekezaji ni pamoja na fursa katika uzalishaji wa ngano na mafuta ya kupikia ambazo zitaiwezesha Sekta ya Kilimo kufikia azma ya Serikali ya kukidhi mahitaji yaliyopo kupitia uzalishaji wa ndani.