Pedro afichua jambo la kushtua kuhusu Depu

WAKATI huko Yanga mashabiki wakifurahia moto wa mshambuliaji wao mpya, Laurindo Dilson Maria Aurélio ‘Depu’ lakini kuna kauli imetoka kwa kocha wa kikosi hicho, Pedro Goncalves ikiashiria kuna kitu bado hakijakaa sawa.

Pedro amekutana na pongezi kutoka kwa mabosi wa Yanga juu ya kile anachofanya Depu kutokana na yeye kupendekeza usajili wake, lakini mwenyewe amewashtua vigogo hao akiwaambia kwa namna anavyomjua mshambuliaji huyo, bado hajafikisha hata asilimia 35 za kiwango ambacho anakifahamu.

Bosi mmoja wa juu wa Yanga, ameliambia Mwanaspoti kuwa, Pedro bado anaamini Depu anaweza kufanya vizuri zaidi ya alichoanza kukifanya sasa wakati akiendelea kuelewana zaidi na wenzake.

Ndani ya mechi mbili za Ligi Kuu alizocheza Depu tangu atue Yanga dirisha dogo la usajili msimu huu akitokea Radomiak ya Poland, ameonyesha kiwango kizuri akifunga mabao matatu huku akiwa na asisti moja.

“Ukweli ni kwamba Depu ameanza vizuri sana, kupata mshambuliaji mwenye makali kama haya sio kitu rahisi, tangu kuondoka kwa Fiston Mayele ni sasa angalau unaweza kusema tuna watu sahihi kule mbele, Depu na Dube (Prince),” alisema bosi huyo.


“Wakati juzi tunampongeza kocha kwa ushindi ambao Depu alifunga mabao mawili akatueleza kitu ambacho kilitushtua sana akisema ni kweli ameanza vizuri (Depu) lakini anaona bado hajacheza kwa kiwango kikubwa akisema ni sawa na ametumia asilimia 35 ya uwezo anaoujua.

“Anasema Depu anaweza kucheza kwa kiwango kikubwa sana kuna mambo wanaendelea kuyaimarisha taratibu, kwanza ni kuunganika vizuri na wenzake namna ya kumpa mipira ambayo anaweza kuonyesha ubora zaidi.”

Aidha bosi huyo aliongeza kuwa, Pedro amewaeleza kwamba hatua ya mshambuliaji huyo kutotumika sana akiwa na klabu yake ya Radom Radomiak ilififisha kiwango chake lakini anaamini kwamba akiwa Yanga atarudisha makali yake halisi.

“Tumeambiwa kwamba hatua ya mshanbuliaji huyo kwenda Ulaya na hakuwa anacheza mara kwa mara imepunguza sana makali yake ambapo hapa Yanga sasa atajitafuta upya na kocha anaamini muda si mrefu atakaa sawa.


“Sio Depu tu, wachezaji wetu wengine ambao tumewasajili dirisha hili dogo wako juu sana, kila mmoja ametuonyesha kitu ambacho tunaamini kimeongeza kitu kikubwa kwenye timu, ni wazi tutakuwa na timu imara kipindi hiki cha kumalizia msimu,” alisema.

Mbali na Depu, Yanga katika usajili wa dirisha dogo imewachukua nyota wapya watano ambao ni Mohamed Damaro, Hussein Masalanga, Allan Okello na Emmanuel Mwanengo, huku Kouassi Attohoula Yao akirejeshwa kwenye mfumo baada ya kupona majeraha ya muda mrefu.