Utafiti mpya unaonyesha kuwa tatoo zinaweza kuongeza hatari ya mtu kupata saratani ya ngozi aina ya melanoma, ambayo ni miongoni mwa aina hatari zaidi za saratani ya ngozi.
Saratani hii mara nyingi huhusishwa na athari za mionzi ya jua (UV) kwenye ngozi.
Utafiti huo, uliofanywa na watafiti kutoka nchini Uswisi uligundua kuwa watu wenye tattoo, walikuwa na ongezeko la hatari ya asilimia 29 ya kupata melanoma ikilinganishwa na watu wasio na tatoo.
Katika uchambuzi wao, watafiti walizingatia mambo mbalimbali yanayoweza kuathiri matokeo, yakiwemo kiwango cha mtu kukaa juani, aina ya ngozi, pamoja na matumizi ya mafuta ya kujikinga na jua.
Hata hivyo, utafiti huo haukubaini ongezeko la hatari ya aina nyingine ya saratani ya ngozi inayojulikana kama ‘squamous cell carcinoma’, licha ya kwamba nayo pia inaweza kusababishwa na mionzi ya jua.
Vilevile, matokeo hayakuonyesha ushahidi wa moja kwa moja kwamba tatoo kubwa zinaongeza hatari zaidi ya melanoma kuliko tatoo ndogo.
Hili lilionekana kuwa jambo la kushangaza, kwa kuwa tatoo kubwa kwa kawaida hutumia rangi nyingi zaidi ambazo huweza kuwa na kemikali hatarishi.
Watafiti wanaeleza kuwa sababu mojawapo inayoweza kuhusisha tatoo na melanoma ni tabia ya rangi ya tatoo kusafirishwa na mfumo wa kinga ya mwili.
Badala ya kubaki kwenye ngozi pekee, chembechembe za rangi hutambuliwa kama vitu vya kigeni na kusafirishwa hadi kwenye tezi za limfu (lymph nodes).
Chembe hizi zinaweza kukaa mwilini kwa muda mrefu na huenda zikasababisha uvimbe wa muda mrefu, hali ambayo inahusishwa na maendeleo ya saratani.
Pamoja na hayo, watafiti wanasisitiza kuwa matokeo haya hayathibitishi moja kwa moja kuwa tatoo ndizo chanzo cha melanoma.
Utafiti zaidi unahitajika ili kuelewa kwa kina jinsi rangi za tatoo, aina zake tofauti, na mwingiliano wake na mwanga wa jua vinavyoathiri mwili wa binadamu.
Kwa sasa, wataalamu wanashauri kwamba watu wenye tatoo, au wanaopanga kuchora tatoo, wachukue tahadhari za ziada kulinda ngozi yao dhidi ya jua.
Hii ni pamoja na kutumia mafuta ya kujikinga na mionzi ya jua, kuepuka kukaa juani kwa muda mrefu, na kufuatilia mabadiliko yoyote ya ngozi kama vile madoa mapya au mabadiliko ya madoa yaliyopo.
Madhara mengine ya tattoo
Tatoo zinaweza kusababisha madhara ya kiafya, hasa pale zinapofanywa katika mazingira yasiyo salama. Kutumia sindano au vifaa ambavyo havijasafishwa vizuri, kunaweza kusababisha maambukizi ya ngozi, kuvimba na kutokea kwa usaha.
Katika hali mbaya zaidi, mtu anaweza kuambukizwa magonjwa hatarishi kama homa ya ini kupitia damu iliyochafuliwa. Haya ni madhara makubwa ambayo yanaweza kuathiri afya ya mtu kwa muda mrefu au hata maisha yote.
Mbali na maambukizi, baadhi ya watu hupata mzio kutokana na wino unaotumika kuchora tatoo. Mzio huu unaweza kujitokeza mara moja au baada ya muda mrefu, hata miaka kadhaa baadaye.
Dalili zake ni pamoja na kuwashwa, vipele, kuvimba au ngozi kubadilika rangi. Kwa wengine, tatoo zinaweza kuacha makovu mabaya yanayoharibu mwonekano wa ngozi, hasa pale ngozi inaposhindwa kupona vizuri.
Kwa upande wa muda mrefu, tatoo zina changamoto kubwa pale mtu anapobadilisha mawazo.
Kitu kilichoonekana kizuri au cha maana wakati wa ujana kinaweza kisipendeze tena baada ya miaka kadhaa.
Kuondoa tatoo si jambo rahisi; ni ghali, huuma na mara nyingi huacha makovu au alama zisizopendeza.
Hii husababisha majuto kwa watu wengi waliowahi kujichora bila kufikiria kwa kina.
Kijamii na kisaikolojia, tatoo zinaweza kuleta athari hasi.
Katika baadhi ya jamii, familia au sehemu za kazi, tatoo bado hutazamwa kama ishara ya utovu wa nidhamu au kutojali maadili.
Hali hii inaweza kumsababishia mtu ubaguzi, kukosa fursa za ajira au migogoro ya kifamilia.
Kwa vijana, shinikizo la rika linaweza kuwafanya wachore tatoo bila kuelewa madhara yake, jambo linaloweza kuwaathiri baadaye maishani.
Makala hii iliyoboreshwa awali ilichapishwa katika mtandao wa The Conversation