KONA YA MSTAAFU: Miradi inayotokana na hela ya mstaafu!

Watu wamekuwa wakisifia sana mitandao ya jamii kuwa inasaidia kuiamsha jamii yetu ijitambue ili kuleta maendeleo ya kweli kwenye nchi. Ni jambo jema. Tusameheane tu kwamba hakuna meza za kupiga makofi ili kushangilia hoja hii njema kama kule “naniliu”!

Wananchi wamekuwa wakitoa mifano hai kulithibitisha hili kuwa tangu nchi yetu ipate uhuru wake miaka 65 iliyopita, vijana wetu wamekuwa wakiaminishwa kuwa wao ni “taifa la kesho”, lakini mitandao imewawezesha kujifahamu sio “taifa la kesho” tu, bali sasa ni “Gen Z”.

Kwamba, sasa wanapaswa kuwa “taifa la leo” kweli na “wakatiwe” haki yao kweli kutoka keki ya Taifa na waitafune wenyewe, na wasiwakilishwe na mtu, kama wanavyofanywa wastaafu wa kima cha chini ambao sio keki ya Taifa tu wanayowakilishwa kuitafuna, bali hata akiba zao wenyewe, pamoja na kwamba wao ndio wameijenga na kuilinda nchi hii!!

Hapa pa mitandao ndipo mstaafu anapoona mitandao ikimsononesha na kumzeesha zaidi anaposoma na kuona habari zinazomharakisha fasta kwenda Kinondoni, badala ya wahusika kuhusika kweli na kuwapunguzia stres zao kwa kuwalipa wastaafu pensheni ya shilingi laki tano kwa mwezi wanazostahili kweli. Si ndio ameijenga na kuilinda nchi?

Amekuwa akisoma mitandaoni kuhusu vikao, warsha, mikutano, makongamano na mabaraza yanayosemekana kuwa ni ya wastaafu, wakati hajabahatika kumuona mstaafu hata mmoja wa kima cha chini, labda wale wanaopokea pensheni ya mamilioni kwa mwezi na wenza wao!

Ndiyo maana husikiagi matamshi ya makelele kutoka kwenye rundo la warsha ama makongamano haya kutaka na kudai nyongeza ya pensheni ya mstaafu wa kima cha chini! Ndiyo maana mstaafu huishia kujiuliza kama kweli hawa ni wastaafu kweli ama ni “mchoro” tu wa kutafuna keki ya Taifa, na kama ni wastaafu kweli, watadai nini zaidi wakati keki ya Taifa wanajikatia tu mapande sio vipande makubwa ya kutosha?

Huko huko kwenye mitandao, mheshimiwa mmoja akaibuka siku chache zilizopita na kutoa rai kwa vibubu vya akiba ya wafanyakazi vijitahidi kuandaa miradi ambayo vijana wetu wanaomaliza vyuoni watapata ajira mara moja! Nikaona “mchoro” mwingine wa kupoteza hela ya wastaafu unataka kuanza..!

Imebidi mstaafu wetu alisome andiko la mheshimiwa mara tatu tatu ili kulielewa, lakini akaishia kutoka kapa, kibuyu wazi wa uzeeni! Vibubu vya akiba ya wafanyakazi vina hela gani ya kuanzisha miradi na kutoa ajira kwa vijana wakati sisi wastaafu wenye hela zetu tulizochanga wenyewe kwa kukatwa mishahara yetu kwa miaka 40?

Sasa tunalipwa pensheni ya shilingi laki moja na elfu hamsini tu kwa mwezi kwa miaka 21 bila nyongeza. Wakianzisha mradi mwingine, si tuishie kulipwa shilingi elfu ishirini?

Tujiulize, ni kibubu gani kinaweza kujitahidi kutengeneza mradi kama ile kibao ya enzi zetu wakati tunalijenga Taifa hili, kama makampuni ya Bora Shoes, Urafiki Textiles, Mwatex, Voil Mwanza, National Matsushita ya redio, betri, tochi na redio kaseti, General Tyres na vinginevyo vilivyotoa ajira kubwa kwa akina sisi!

Hivi nchi yetu sasa ina viwanda vingapi vya kutoa ajira kwa wananchi, au tuna kazi ya kuagiza hata kijiti cha kuchokolea meno China?

Lakini hapo hapo mstaafu wetu akashtuka. Kuna miradi kibao ya “vikwangua anga” ambavyo vimejengwa kwa hela ya akiba ya wafanyakazi waliokatwa kwenye mishahara yao kwa miaka 40 walioijenga na kuilinda nchi.

Hata Siri-kali mwaka juzi tulisikia ikilipa hela iliyotakata iliyokuwa imekikopa kibubu, bila mtu kutufahamisha wastaafu wenyewe, ili kujenga Daraja la Kigamboni!

Hapa mstaafu anaishia tu kujiuliza ni wa nini daraja lijengwe kwa hela yetu halafu wastaafu tuishie kulipa ili kwenda Kigamboni? Kwa wahusika wasiandae utaratibu tu wa kumpa mstaafu kadi ya kumwezesha kupita bure pale, maana akiba yake ilichangia kulijenga?

Lakini swali muhimu zaidi ni lile la kwamba miradi yote ya magorofa yetu nchini, yote yote hutoza kodi ya kueleweka. Hii kodi inayolipwa mbona haitufikii sisi ambao hela yetu ndiyo ilitumika kujenga magorofa hayo?

Kibubu kinatuambia tu tukiisha fariki ndipo watatoa shilingi milioni tano laki tano ili nipelekwe vyema Kinondoni! Yaani kibubu kinipe milioni tano na laki tano nikiwa tayari maiti, sio nikiwa mzee na kunipunguzia stres! Acheni utani mbaya na maisha ya watu!

0754 340606 / 0784 340606