Dar es Salaam. Hakika Uislamu umeipa nafasi kubwa sana elimu ya malezi ya kijamii. Haukuacha jambo dogo wala kubwa isipokuwa umelifafanua.
Umebainisha kwa kina haki za wazazi, haki za wanandoa na watoto, haki za majirani, pamoja na miamala yote na maadili ya Kiislamu. Miongoni mwa maadili hayo ni adabu ya kupiga hodi. Adabu hii ni alama iliyo wazi miongoni mwa misingi ya malezi ya kijamii. Ni adabu nyeti inayokuza hisia za kuwajali na kuheshimu wengine.
Uislamu umeipa adabu hii umuhimu mkubwa sana. Adabu hii Allah Mtukufu Ameieleza kwa kina ndani ya Qur’an: “Enyi mlio amini! Msiingie nyumba zisio nyumba zenu mpaka mwombe ruhusa, na mwatolee salamu wenyewe. Hayo ni bora kwenu mpate kukumbuka” (24:27).
Hakika tofauti nyingi za uhusiano wetu wa kijamii zinarejea kwenye ukweli kwamba wapo watu wasioufahamu mipaka yao wanapoamiliana na wengine.
Hawajui wapi wanapaswa kusimama ili wasivuke mipaka hiyo, wala hawatambui ule “mstari mwekundu” unaopaswa kuheshimiwa, ili wasiwe mzigo mzito kwa wengine na kuwadhuru katika dini yao, heshima na maisha yao ya kila siku.
Wanazuoni wa Sharia ya Kiislamu wamefafanua maana ya kupiga hodi kuwa ni: Kuomba idhini kwa adabu, kwa lengo la kujiepusha na kuangalia uchi au mambo yasiyopasa kuonekana.. Vilevile, wapo waliosema kuwa ni: Kuomba ruhusa ya kuingia katika sehemu ambayo si miliki ya anayeomba ruhusa.
Mtazamo wa kina juu ya siri na hekima za adabu ya kupiga hodi unaonesha uhalisia wake na busara iliyomo ndani yake. Mwanadamu ameumbwa na silika ya matamanio na tamaa; na si kila mtu huweza kuzuia tamaa zake na visababishi vyake kwa msukumo wa dhamira ya kibinadamu au kwa misukumo ya utu na heshima. Badala yake, hujizuia zaidi kwa msukumo wa imani.
Sharia ya Kiislamu ina hukumu nyepesi na mtazamo wa mbali ulio wa kina; kwani inapokataza jambo fulani, hukataza pia kila njia na kichocheo kinachopelekea kwenye jambo hilo. Na hapa ndipo penye tofauti katika ya Sharia za Allah na zile zilizotungwa na wanadamu. Kwa mfano,
Uislamu ulipokataza uzinzi, ulikataza pia visababishi vyake kama kutazama kwa haramu, kukaa faraghani, kuonyesha maungo ya mwili, na kila kinachosababisha uzinzi.
Kubisha hodi ni adabu ya hali ya juu inayolinda heshima na mipaka ya nyumba. Ikiwa hakuna mtu yeyote wa kutoa ruhusa ya kuingia ndani ya nyumba, basi subiri hadi utakaporuhusiwa. Hii ni kwa sababu kuomba ruhusa kunahusiana na heshima ya nyumba na wakaazi wake.
Allah Mtukufu amesema: “Na msipo mkuta mtu humo basi msiingie mpaka mruhusiwe. Na mkiambiwa: Rudini! Basi rudini. Hivi ni usafi zaidi kwenu. Na Mwenyezi Mungu anajua mnayo yatenda. (24:28).
Hii inaonyesha kwamba mgeni anatakiwa kurudi nyuma katika hali mbili: Mosi, anapokosa ruhusa ya wazi ya kuingia, kama vile kuambiwa“rudi” au “usingie.” Pili, anapokosa ruhusa isiyo ya wazi kama hakuna mtu wa kumwitikia hodi yake.
Hakika nyumba za Waislamu zina heshima kubwa mno; Mtume wa Allah (Rehema na amani ziwe juu yake) ameilinda heshima hii kwa kuweka adhabu kali kwa anayekeuka:“Lau mtu angechungulia kwako bila ruhusa, ukamtupia jiwe likampofua jicho, usingekuwa na kosa.” Kubisha hodi huzipa nyumba heshima yake, na huwalinda wakaazi wake na aibu na dhiki inayotokana na kushtukizwa, kuvamiwa ghafla, au kudhurika kwa kufichuka kwa siri. Na siri ni nyingi, si uchi wa mwili pekee kama wengi wanavyodhani. Bali hujumuisha pia siri za chakula, siri za mavazi, na siri za samani na mpangilio wa nyumba, ambavyo navyo vina haki ya kuheshimiwa na kulindwa.
Mtu anayebisha hodi ni sunna kusalimia: “Assalamu ‘alaykum, naweza kuingia?” Kupiga mlango kwa nguvu au kupiga kelele kwa mwenye nyumba ni haramu.
Wanasharia wa Kiislamu wanasema: Kuomba ruhusa kwa maneno yote yaliyojulikana na jamii ni halali, mradi hayako kinyume na sharia ya Kiislamu, lakini kufuata Sunna ni bora zaidi.
Kadhalika; Miongoni mwa adabu muhimu za kubisha ni kuzingatia namna ya kusimama wakati wa kuomba kubisha hodi. Mgeni haipaswi kusimama kueelekea mlango uso wake moja kwa moja, bali asimame upande wa kulia au kushoto wa mlango Adabu ya kubisha hodi inajumuisha pia jinsi ya kujitambulisha pale unapoulizwa: “Wewe ni nani?”
Mgeni anapaswa kutaja jina lake, na si kusema tu: “Mimi” Hii inalingana na mfano wa malaika Jibril alipobisha hodi mlango wa mbingu usiku wa Mi‘raj, alipoulizwa: “Ni nani?” Akajibu: “Jibril.
Watu wa leo, licha ya kuwa ni Waislamu, hisia zao kuhusu adabu hizi nyeti zimepungua. Mtu anaweza kumvamia ndugu yake nyumbani kwake wakati wowote wa usiku au mchana, akagonga mlango mara kwa mara bila kuchoka, na hatimaye hatoki mpaka awakere watu wa nyumba kiasi cha kulazimika kumfungulia. Wakati mwingine, nyumbani kuna simu ambayo ingewezekana kabisa kuomba ruhusa kupitia njia hiyo kabla ya kufika.