Tanzania, 16 Januari 2026.
KAMPUNI ya Airtel Tanzania imezindua minara mitano mipya ya mawasiliano katika maeneo ya Kilindi – Tanga, Mbalamaziwa – Njombe, Ruanda – Songea, Miombo – Sumbawanga, na Buhongwa – Mwanza, hatua inayolenga kuimarisha upatikanaji wa mtandao na kuboresha huduma za simu na intaneti kwa wananchi wanaoishi katika maeneo hayo. Uwekezaji huu ni sehemu ya mkakati endelevu wa Airtel wa kupanua miundombinu ya mawasiliano ili kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora na za uhakika, hususan katika maeneo ambayo awali yalikuwa hayajahudumiwa ipasavyo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi uliofanyika Ruvuma, Diwani wa Kata ya Ruanda, Mheshimiwa Douglas Mwingira, ameishukuru Airtel kwa kuwekeza katika eneo hilo, akibainisha kuwa mnara huo utakuwa kichocheo cha maendeleo ya haraka. Ametumia pia fursa hiyo kuwasihi vijana na wajasiriamali kutoendelea kubaki nyuma. “Mnara mpya wa Ruanda uliyozinduliwa leo utahudumia jamii tatu zinazozunguka eneo hili, hivyo kuongeza wigo wa mtandao na kuboresha ubora wa huduma kwa wananchi wengi zaidi. Huu ni wakati wa wananchi wetu kuchangamkia fursa. Uwepo wa mtandao imara hapa Ruanda unafungua milango ya biashara za kidijitali, huduma za kifedha, na ajira. Tusisubiri tuanze kutumia fursa hizi sasa ili kuharakisha maendeleo ya wananchi na jamii yetu,” amesisitiza.
Kwa upande wa Kilindi, Tanga, Meneja wa Tawi la Airtel Tanga, Bi. Lydia Kalimunda, amesema mnara huo mpya utakuwa na mchango mkubwa katika kuwaunganisha wakazi na fursa zilizo nje ya maeneo yao ya karibu. “Upanuzi huu wa mtandao utawezesha wananchi wa Kilindi na maeneo jirani kuendelea kuwasiliana, kupata huduma za kifedha kupitia simu za mkononi na kushiriki kikamilifu zaidi katika uchumi wa kidijitali,” amesema.
Tukio la uzinduzi likiendelea huko Buhongwa , mwanza Meneja wa Kanda wa Airtel, Bw. Malaki Mchala, alieleza athari chanya za mnara huo katika maisha ya kila siku na maendeleo ya wananchi. “Mnara huu utaboresha kwa kiasi kikubwa mawasiliano katika eneo la Buhongwa. Mwanza inajulikana kwa shughuli zake za uvuvi, kilimo chenye rutuba, na uchimbaji wa madini. Kupitia maboresho haya ya mtandao, wakazi wataweza kupiga simu kwa uhakika, kutumia huduma za simu za mkononi, na kufikia intaneti kwa urahisi, jambo litakalosaidia shughuli za kibiashara na kuboresha upatikanaji wa taarifa na huduma kwa wananchi wa Mwanza,” amesema Bw. Mchala.
Vilevile, mkazi wa Miombo, Sumbawanga, alisema, “Huu ni wakati muhimu kwa jamii yetu. Ujio wa mtandao wa Airtel hapa Miombo unafungua fursa mpya kwa biashara za ndani kukua zaidi ya mauzo ya ana kwa ana. Kwa mtandao wa uhakika, sasa tunaweza kutangaza bidhaa zetu kidijitali, kuuza mtandaoni, na kufikia masoko mapana zaidi ili kuboresha maisha yetu,” amesisitiza.
Airtel Tanzania inaendelea kuipa kipaumbele upanuzi wa mtandao kama sehemu ya dhamira yake ya kukuza ujumuishi wa kidijitali, kuhakikisha wananchi wote nchini wanapata huduma za simu na intaneti zenye uhakika, gharama nafuu, na ubora wa juu. Kupitia uwekezaji endelevu katika miundombinu, Airtel imeendelea kuwaunganisha watu, kuwawezesha wananchi, na kuunga mkono maendeleo ya taifa.
.jpeg)
