RC TANGA AIPONGEZA SAADANI, ATANGAZA MKAKATI WA KUITANGAZA KITAIFA

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dkt. Batilda Buriani, amepongeza uongozi wa Hifadhi ya Taifa ya Saadani kwa kuwa na mazao mengi ya utalii, ikiwemo utalii wa mikutano, unaozivutia taasisi, mashirika na Halmashauri kufanya mikutano yao katika ukumbi uliopo pembezoni mwa fukwe za Bahari ya Hindi ndani ya hifadhi hiyo.

Akizungumza katika Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Mkoa wa Tanga uliofanyika Saadani, amesema uwepo wa vivutio vingi vya utalii ikiwemo wanyamapori, fukwe, utalii wa boti na muingiliano wa maji ya Bahari ya Hindi na Mto Wami, umeifanya hifadhi hiyo kuwa ya kipekee kitaifa.

Dkt. Buriani amesema kutokana na utajiri huo wa vivutio, Mkoa wa Tanga umeandaa mikakati madhubuti ya kuanza kuitangaza Hifadhi ya Taifa ya Saadani kitaifa na kimataifa ili kuongeza idadi ya watalii, mapato na kuifanya Tanga kuwa miongoni mwa mikoa inayoongoza kwa utalii wa asili nchini.

Ameeleza kuwa mkakati huo unaunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, za kuitangaza Tanzania kupitia diplomasia ya utalii na kuongeza mchango wa sekta hiyo katika uchumi wa Taifa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Saadani, Gladys Ng’umbi, amesema hifadhi hiyo ina upekee mkubwa wa kiikolojia unaotokana na muunganiko wa bahari, mito na wanyamapori, hali inayochochea ubunifu wa mazao mengi ya kiutalii.

Amesema mafanikio hayo yameifanya Saadani kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 2.5 katika mwaka wa fedha 2024/2025, kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watalii wanaotembelea hifadhi hiyo.

Naye Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi kutoka Ofisi ya Kanda ya Mashariki, Fredrick Malisa, amewahamasisha wananchi, taasisi na mashirika kujitokeza kutumia kumbi za mikutano zilizopo ndani ya hifadhi hiyo kujadili masuala ya kiuchumi na maendeleo.

Amesema baada ya kumaliza mikutano yao, washiriki hupata fursa ya kutembelea vivutio vilivyopo ndani ya hifadhi ikiwemo fukwe, wanyamapori na utalii wa boti, hatua inayochochea utalii wa ndani na kuongeza mapato kwa jamii zinazozunguka hifadhi.

Awali, wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Mkoa wa Tanga walipata fursa ya kutembelea vivutio mbalimbali ndani ya Saadani na kueleza kuvutiwa na mazingira na fursa za kiutalii zilizopo.