RAIS SAMIA AMEJIPANGA KUFIKISHA UMEME VITONGOJI VYOTE

:::::::::::

Imeelezwa kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameelekeza Wakala wa Nishati Vijijini (REA), kufikisha umeme kwenye vitongoji vyote vilivyobakia nchini ambavyo bado havina huduma ya umeme ifikapo mwaka 2030.

Hayo yamebainishwa leo Januari 30, 2026 na Bw. Frank Mugogo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mha. Hassan Saidy wakati wa hafla fupi ya kumtambulisha mkandarasi kutoka kampuni ya Central Electricals International Ltd katika Mradi wa HEP 2B ambaye anaenda kutekeleza kwenye vitongoji 218 mkoani Njombe.

“Jumla ya vitongoji vyote mkoa wa Njombe ni 1,833 na vitongoji vyenye umeme ni 1,276. Vilevile vitongoji ambavyo havina umeme ni 557. Hivyo mradi huu unakwenda kupeleka umeme kwenye vitongoji 218 katika mkoa huu na vitabakia vitongoji 339 ambavyo havina umeme navyo vitakamilika, ” Amesema Bw. Mugogo.

Ameongeza kuwa, gharama za kuunganisha umeme huo ni shilingi 27,000 tu na kuwataka wananchi wa mkoa huo kutumia fursa ya kuunganisha umeme kwa gharama nafuu iliyowezeshwa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe.Rais Samia.

Akizungumza mara baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa miradi hiyo mkoani Njombe, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa Bw. Lewisi Mnyambwa amemshukuru Rais Samia kwa kuleta fedha nyingi zaidi ya bilioni 24 ili kupeleka umeme kwenye vitongoji vya mkoa wa Njombe.

“Serikali kupitia REA imefanya kazi kubwa. Tunasisitiza miradi hii ikamilike kwa muda uliopangwa na tutaendelea kuusimamia ipasavyo ili mkandarasi aweze kutekeleza majukumu yake pasipo changamoto yeyote katika kipindi chote cha utekelezaji wa mradi,” Amesema Mnyambwa. 

Aidha, ametoa rai kwa wananchi wanaozunguka eneo la mradi kumpatia ushirikiano mkandarasi huyo na ametakiwa kutoa kipaumbele cha ajira kwa wazawa ili kufanya shughuli mbalimbali katika mradi huo ili uchumi wa wananchi uongezeke na wanufaike na uwepo wa miradi hiyo katika mazingira yao.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Miradi kutoka kampuni ya Central Electricals International Ltd, Bw. Zameer Meghji ameishukuru Serikali kupitia REA kwa kupewa fursa ya kutekeleza mradi huo mkubwa. Amesema watahakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati, watashirikiana na wananchi na kutoa kipaumbele cha ajira kwa wazawa ili miradi hiyo ilete tija kwa wananchi na nchi kwa ujumla.




Mwisho