Dodoma. Mbunge wa Bukoba Mjini (CCM), Johnston Mutasigwa ameihoji Serikali kwamba, ina mpango gani wa kuwasaidia masoko ya senene na vifaa bora vya kutengeneza bidhaa hiyo kwa wananchi wa Bukoba.
Leo Ijumaa Januari 30, 2026, katika swali la nyongeza, mbunge huyo amesema kwa sasa wafanyabiashara hawana eneo maalumu la kufanyia biashara hiyo na kuomba ikiwezekana watengewe eneo katika soko la mjini Bukoba linalojengwa.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Viwanda Denis Londo amesema Serikali itaendelea kutafuta masoko na kufungua masoko ya uhakika kwa bidhaa za senene.
“Hii inajumuisha kuwaunganisha wafanyabiashara wa senene na masoko ya miji mikubwa nchini, kuwashirikisha katika maonesha ya kibiashara kitaifa na kikanda na kutangaza biashara ya kipekee ya Kanda ya Ziwa,” amesema Londo.
Naibu Waziri amesema Serikali itaendelea kuwaunganisha wafanyabiashara hao kwenye mazoko mapana ya Afrika Mashariki na kwingineko.
Amesema kupitia Shrika la Maendeleo la Viwanda Vidogo (Sido) kwa kushirikiana na Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech) na Veta, Serikali itaendelea kufanya tafiti zinazolenga kuendelea na kuboresha biashara ya senene.
Amesema teknolojia ya rahisi ya mfano itakayosaidia katika uvunaji wa senene imebuniwa na kutengenezwa.
Kuhusu soko la sasa, amesema wako mbioni kutenga eneo na kujenga soko la senene litakalokuwa na uwezo wa kuwaweka pamoja wafanyabiashara hao.