“TUNAANZA Ligi na Pamba Jiji.” Ni kauli ya Kipa wa Mbeya City, Beno Kakolanya akiwatuliza mashabiki wa timu hiyo kufuatia mwenendo na matokeo yasiyoridhisha inayopata timu hiyo katika Ligi Kuu Bara.
Mbeya City iliyorejea Ligi Kuu msimu huu, haijawa na matokeo mazuri hadi kufikia uamuzi wa kuachana na aliyekuwa na Kocha wake, Malale Hamsini.
Timu hiyo kabla ya kushuka daraja 2023-2024, ilicheza kwa misimu 10 mfululizo na iliporejea sasa, mwenendo wake hauridhishi ikiwa imekusanya pointi nane ikishika nafasi ya 14 katika msimamo baada ya mechi 11.
Leo Ijumaa saa 10:00 jioni, Mbeya City itakuwa nyumbani Uwanja wa Sokoine kuikaribisha Pamba Jiji, ikiwa na mtihani wa kusaka ushindi ilioukosa kwa muda mrefu.
Mara ya mwisho timu hiyo inayomilikiwa na Halmashauri ya Jiji la Mbeya kupata ushindi katika ligi, ilikuwa Oktoba 18, 2025 ilipoichapa KMC mabao 3-1. Baada ya hapo, imecheza mechi saba bila ushindi ikiambulia sare moja na vipigo sita.
Akizungumzia mechi dhidi ya Pamba Jiji, Kakolanya alisema wanafahamu kipindi kigumu wanachopitia ikiwa ni maumivu kwao binafsi na mashabiki kwa ujumla, akiahidi kuwa leo wanaanza rasmi Ligi Kuu.
Alisema wanaoikatia tamaa timu hiyo, wawe na uvumilivu kwani wachezaji hawajakata tamaa na mechi dhidi ya Pamba Jiji, wanatarajia kushinda ili kurejesha upya nguvu, ari na morali ndani na nje ya uwanja.
“Niwaombe mashabiki wasikate tamaa, tunaenda kuanza na Pamba Jiji kupata ushindi, wote tunaumia kwa matokeo tuliyonayo ila tunaahidi kurejea upya,” alisema Kakolanya.
Kipa huyo aliyewahi kucheza timu kadhaa ikiwamo Yanga, Simba, Singida Black Stars na Namungo, ameongeza kuwa upungufu na makosa yaliyoonekana katika michezo iliyopita kocha ameyaona na kutafanyia kazi ambapo leo wataonesha kwa vitendo.
Kwa upande wake nyota wa Pamba Jiji, Kenneth Kunambi, alisema wataingia uwanjani kwa nidhamu na kuwaheshimu wapinzani kuhakikisha wanaendelea kufanya vizuri.
Alisema baada ya kupoteza mechi iliyopita dhidi ya Mtibwa Sugar, hawatakubali kupoteza tena ili kupambania nafasi nne za juu waliyopo akieleza kuwa wamejipanga kiushindani.
“Tulianza vizuri hadi kuwa kileleni, lakini kutokana na ushindani wa ligi tumekuwa sehemu tulipo, tumetoka kupoteza mchezo ugenini, hivyo hatukubali kuruhusu tena pointi tatu zipotee, tutawahehimu wapinzani ila hatuwaachii kitu,” alisema Kunambi.
Kupitia dirisha dogo la usajili, Mbeya City imefanya maboresho ya kikosi kwa kuingiza nyota wapya akiwamo Yakouba Songne, Hassan Dilunga, Omary Abdallah, Mohamed Ally, Kelvin Kijili, Naushad Said, Hijah Shamte na Abdallah Kulandana.
Kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo jijini Dar es Salaam, itapigwa mechi nyingine ya Ligi Kuu Bara leo kati ya JKT Tanzania dhidi ya Dodoma Jiji kuanzia saa 1:00 usiku.
Ni mechi ambayo JKT Tanzania inaitazamia kwa ukaribu zaidi kusaka ushindi ili kurejea kileleni baada ya kushushwa na Yanga, huku Dodoma Jiji ikitaka kusahihisha makosa yaliyofanya ipoteze mechi iliyopita kwa kufungwa 3-1 na Yanga.
JKT Tanzania yenye pointi 21 ikishika nafasi ya pili kwenye msimamo baada ya mechi 12, inafahamu kwamba baada ya leo itabakiwa na mechi mbili pekee kufunga hesabu za mzunguko wa kwanza, hivyo suala la kukusanya pointi tatu kwao ni muhimu zaidi.
Dodoma Jiji nayo ipo mbali sana na nafasi za juu kwenye msimamo ikikamata ya 12 ikiwa na pointi kumi baada ya mechi 11.
Timu hizi zilizoanza kukutana Septemba 12, 2020 katika Ligi Kuu Bara, hadi sasa zimecheza mechi sita, ambapo JKT Tanzania haijawahi kupata ushindi mbele ya Dodoma Jiji zaidi ya kuambulia sare mbili na vichapo vinne.
Mara ya mwisho timu hizo kukutana Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, nyavu zilikuwa na wakati mgumu kufuatia kufungwa mabao manne katika sare ya 2-2.
Kocha Ahmad Ally wa JKT Tanzania na Aman Josiah wa Dodoma Jiji, leo kila mmoja ana kazi ya kufanya kuhakikisha anayafikia malengo baada ya dakika tisini ingawa zinapokutana timu hizo, mechi haijawahi kuwa rahisi hasa kwa wenyeji.