Musoma. “Kanuni hizi ni batili,” ndio kauli iliyotolewa na Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Musoma, wakati ikitoa uamuzi wa maombi ya mapitio ya Mahakama juu ya kanuni za wajibu wa wamiliki wa leseni za madini kwa jamii.
Katika uamuzi wake huo alioutoa Januari 28, 2026 na nakala ya uamuzi huo kuwekwa mtandaoni Januari 29, 2026, Jaji Kamazima Kafanabo alitoa amri tatu muhimu ambazo zimepeleka kicheko kwa wananchi wanaoishi kuzunguka migodi.
Jaji Kafanabo ametoa amri hizo wakati akitoa uamuzi wa maombi ya mapitio ya Mahakama (judicial review) namba 000013576 ya 2025 yaliyofunguliwa na wananchi watano dhidi ya Waziri wa Madini na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Wananchi hao, Godfrey Kegoye, Gotora Chichake, Paul Bageni, Daud Nyamhanga na Bogomba Chichake ni wakazi wa vijiji vya Matongo, Nyangoto, Mjini Kati na Kewanja, Wilaya ya Tarime, vinavyozunguka mgodi wa North Mara Gold Mine.
Walifungua maombi hayo kupinga Kanuni za Wajibu wa Wamiliki wa Leseni za Madini kwa Jamii za Mwaka 2023 na GN namba 409 ya mwaka 2023 iliyotangazwa na Waziri wa Madini na kuchapishwa katika gazeti la Serikali Juni 23, 2023.
Katika uamuzi wake, Jaji Kafanabo ametoa matamko matatu, moja kuwa kanuni zilitungwa nje ya uwezo wa kisheria (ultra vires) na pili, kanuni hizo ni batili na hazina nguvu ya kisheria kwa sababu zinakiuka Sheria ya Madini.
Tatu, Mahakama hii inakataza matumizi na utekelezaji wa kanuni hizo.
Wananchi hao walieleza kupitia kiapo chao kuwa, ile kuishi katika vijiji vinavyozunguka Mgodi wa North Mara Gold Mine, wananufaika moja kwa moja na Wajibu wa Kampuni kwa Jamii (CSR) unaotolewa na kampuni hiyo tangu 2018.
Kupitia kwa mawakili Kassim Gilla na Kevin Mutatina, wananchi walieleza vijiji vyao vilikuwa vimepangiwa kupata mgawo wa asilimia 100 ya CSR inayotolewa na Kampuni ya North Mara Gold Mine kwa vijiji vinavyozunguka mgodi huo.
Hakuna ubishi kuwa, wananchi hao walishiriki kikamilifu katika uandaaji na utekelezaji wa mipango ya CSR katika maeneo ya mazingira, kijamii, uchumi na utamaduni ikiwamo ukarabati wa barabara na ujenzi wa mashule na hospitali.
Hata hivyo, Juni 23, 2023, Waziri wa Madini alitunga kanuni za CSR na kutangaza kuwa sheria, ambazo wananchi hao walidai zinawaathiri wao na wananchi wengine wenyeji wanaoishi katika maeneo mengine kunapochimbwa madini.
Walieleza kuwa, kanuni hizo za CSR ziliwaondoa kabisa katika umiliki wa asilimia 100 wa CSR waliokuwa wanapewa na kampuni na zilifanya zaidi ya asilimia 60 ya CSR zipelekwe kwenye wilaya, miji, manispaa na majiji.
Miji na manispaa hizo wala sio kwa jamii mwenyeji wa eneo lenye madini na asilimia 40 ya CSR inayopelekwa kwenye vijiji vinavyozunguka mgodi huo; ni tofauti na ile ya asilimia 100 waliyokuwa wakipata kabla ya kanuni hiyo.
Hii imewanyima fursa jamii mwenyeji ulipo mgodi pamoja na kuwanyima uwezo wa kupanga na kutekeleza mipango mbalimbali ya maendeleo ya kiuchumi, kijamii na utamaduni.
Hivyo, wananchi hao wakalalamika kuwa kitendo cha mjibu maombi wa kwanza ambaye ni Waziri wa Madini, kutunga kanuni hizo kilikuwa ni nje ya uwezo wake wa kisheria na kwamba, hawakushirikishwa wala kupewa nafasi ya kutoa maoni.
Hata hivyo, wajibu maombi kupitia kwa wakili mwandamizi wa Serikali, Kitia Turoke, hawakupingana na hali (status) ya sasa wa wanavijiji hao kuhusu rasilimali za CSR ambazo vijiji vya North Mara vinanufaika nazo.
Hata hivyo, kupitia kiapo chao kinzani, walieleza kuwa, kanuni za CSR huanzisha utaratibu wa kusambaza hazina na kunufaisha jamii zinazozunguka maeneo ya uchimbaji madini nchini kote wala haziwazuii kupanga mipango ya maendeleo.
Pia, wajibu maombi walieleza hakuna ushahidi kwamba waombaji wameathiriwa na madai ya mgao mdogo wa rasilimali za CSR na kanuni za CSR haziwezi kurekebishwa ili kuzingatia masilahi ya watu wachache, wakati huo huo zinatumika nchi nzima.
Ni msimamo wa wajibu maombi kwamba utungwaji na uchapishaji wa kanuni hizo za CSR, zilichapishwa na Waziri wa Madini kwa mujibu wa mamlaka aliyonayo chini ya Sheria ya Madini, sura ya 123 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka RE 2019.
Jaji Kafanabo katika uamuzi wake, alirejea kifungu cha 136(1(2) na (5) cha Sheria ya Madini akisema hazitoi ugawaji au usambazaji wowote wa rasilimali za CRS.
Pia, hazielezi utaratibu wa utekelezaji wa mpango wa CRS, isipokuwa kwa mahitaji kwamba, mpango wa CSR utazingatia vipaumbele vya Serikali za mitaa vya jumuiya mwenyeji wa eneo ambako shughuli za uchimbaji madini hufanyika.
Hata hivyo, alisema kanuni za Waziri wa Madini hasa kanuni ya 4 ikisomwa pamoja na kanuni ya 3 na 10, ni wazi Serikali ya mitaa iliyotajwa katika sheria ni au Serikali ya kijiji, mtaa au kitongoji na ndio baadaye mipango inawasilishwa halmashauri.
“Ni kutokana na msimamo huo wa kanuni na sheria, ni wazi kwamba, vipaumbele vilivyoainishwa katika mpango wa CSR vinahusu wenyeji wa kijiji, mtaa na kata inayozunguka eneo la uchimbaji madini,”alisema Jaji Kafanabo.
“Hivi si kipaumbele kwa halmashauri ya mji, halmashauri ya wilaya, manispaa au jiji, mwenye haki ya madini anafanya shughuli zake za uchimbaji madini.”
“Chini ya Kanuni ya 11 ya Kanuni za CSR, mwenye haki ya madini anatakiwa kutenga fedha ili kutekeleza mpango wa CSR kwa wakazi wa eneo ambalo uchimbaji madini hufanyika. Hii ni mipango yote ya CSR iliyoidhinishwa.”
Jaji alisema kwa msingi huo, mmiliki wa mgodi anatakiwa kutoa fedha za ufadhili kufadhili miradi ya CSR ambayo imekubaliwa kwa pamoja kati ya mchimbaji wa madini na wenyeji wa eneo ambalo madini hayo yanachimbwa.
“Kuzingatia hayo hapo juu, swali la msingi ni kama jumuiya mwenyeji zimetengewa fedha kidogo, kinyume na mtazamo wa sheria ya uchimbaji madini?”
“Mahakama hii inaona waombaji wanaathiriwa moja kwa moja na mgao mdogo wa rasilimali za CRS chini ya muundo wa sasa uliotangazwa na kanuni za CSR, ambayo ni kinyume na kanuni ya kifungu cha 136 cha Sheria ya Madini”
“Ni dhahiri kanuni ya 4(4) na (b) ya kanuni za CSR, inayotenga asilimia 60 kwa halmashauri za wilaya, miji, manispaa na majiji na asilimia 40 kwa wananchi wenyeji haiendani na masharti ya kifungu cha 136 cha sheria ya madini.
Jaji Kafanabo alisema kifungu hicho hakikumpa waziri mamlaka ya kutunga sheria kuhusu mgawanyo wa rasilimali za CSR zilizokusudiwa kunufaisha jumuiya mwenyeji na kuzihamishia katika nyadhifa nyingine kwa utashi wa mawaziri.
“Sheria ya madini haikumruhusu waziri kutunga sheria au kanuni kuwapa kipaumbele ambao hawakukusudiwa na Sheria ya Madini na kuharibu madhumuni ya sheria yaani mipango na nyenzo za CSR ili kunufaisha jumuiya mwenyeji,”alisema.
Jaji alisema ni wazi kuwa, uamuzi wa mlalamikiwa wa kwanza kutunga Kanuni ya 4(4)(a) na (b) ya Kanuni za CSR ulikusudiwa kushindwa, kuua au kubatilisha mpango uliokusudiwa kutekelezwa kwa matumizi ya rasilimali za CSR.
Mbali na hilo, kuhusu hoja ya kama wanavijiji walishirikishwa ama la, Jaji alisema baada ya kupitia orodha ya wajibu maombi, amebaini walioshirikishwa ni wale wanafanya shughuli za madini au watendaji wa Serikali za mitaa.
Jaji alisema hakuna uthibitisho wowote kuwa wajibu maombi waliwajulisha jamii zinazozunguka migodi mahali popote nchini kuhudhuria mikutano hiyo.
Jaji alisema hilo linajionesha katika uamuzi uliofikiwa na waziri kwa kutuma kanuni za CSR kugawa fedha zake kwa asilimia 60 kwa halmashauri za miji, wilaya na majiji na asilimia 40 kwa wenyeji kinyume na maoni ya wadau.
Katika uamuzi wake, Jaji Kafanabo alitoa matamko matatu, moja kuwa kanuni zilitungwa nje ya uwezo wa kisheria (ultra vires); pili, kanuni hizo zinatangazwa ni batili na hazina nguvu ya kisheria kwa sababu zinakiuka Sheria ya Madini.
Tatu, Mahakama inakataza matumizi na utekelezaji wa kanuni hizo.