Mbeya. Serikali imetoa zaidi ya Sh43.7 bilioni kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo hususani ukarabati na ujenzi wa miundombinu mipya ya sekta ya elimu na afya.
Miradi hiyo imeanza kutekelezwa tangu Oktoba 2025 hadi Februari 2026 ikihusisha maboresho elimu bila malipo, vituo vya afya, zahanati, malipo ya watumishi pamoja na utekelezaji miradi ya maendeleo ngazi ya jamii.
Uwekezaji huo umetajwa kuchangia jamii kuwa na mwamko mkubwa wa kuchangamkia fursa za huduma za afya na elimu tofauti na miaka ya nyuma walikuwa wakitembea umbali mrefu.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Mbeya, Erica Yegella leo Ijumaa Januari 30, 2026 wakati akizungumza na Mwananchi kuhusiana na uwekezaji wa sekta ya elimu ulivyochangia ongezeko la wanafunzi shuleni.
Amesema katika jitihada za kupunguza msongamano wa wanafunzi kwa mwaka 2025/2026, halmashauri imejenga madarasa 44, elimu ya msingi na kukarabati mengine tisa ambayo yako katika hatua za ukamilishaji.
“Pia, tumetupia jicho kuboresha miundombinu ya wanafunzi mahitaji maalumu pamoja na vifaa vya kufundishia, lakini kuongeza idadi ya walimu kutoka 1,454 hadi 1,501, madawati kutoka 500 mpaka 1,118 kwa shule 170 za msingi,” amesema.
Amesema katika kuhakikisha elimu bora inatolewa walimu wamejengewa uwezo wa matumizi ya mitaala mipya ya kujifunza na kujifunzia wanafunzi na tayari Serikali imetoa vitabu 170 shuleni.
Idadi ya wanafunzi elimu awali
Yegella amesema kwa mwaka 2026 hadi kufikia Januari 23, 2026 asilimia 67.7, wamejiunga elimu ya awali huku darasa la kwanza ni asilimia 73.6, lakini malengo ifikapo leo Januari 30, 2026 idadi itaongezeka.
Kwa upande wa sekondari, wanafunzi waliojiunga kidato cha kwanza mwaka 2026 ni 6,523, wasichana 3,673 na wavulana 2,850 huku kukiwa na ongezeko la wanafunzi 3,158.
“Lakini tuna mikakati kabambe kuhakikisha watoto wa pembezoni wanapata elimu bora mpaka sasa tumejenga vituo shikizi 41, kati ya hivyo, tisa vimesajiliwa,” amesema.
Yegella amesema Serikali inaendelea kuboresha miundombinu ambapo zaidi ya Sh1.6 bilioni zimetumika ujenzi kituo cha afya cha kimkakati cha Isuto sambamba na kukamilika vingine vya Ulenje, Mbalizi na Swaya.
Kwa upande wake, Ofisa Elimu Divisheni ya Awali na Msingi, Tanu Kameka amesema kimsingi uwekezaji wa Serikali kwenye miundombinu ya sekta ya elimu imeleta hamasa kwa wazazi na wanafunzi kujua umuhimu wa elimu.
“Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imeleta mageuzi makubwa katika sekta ya elimu kwa kutua mzigo kwa wazazi kwenye suala la michango mbalimbali, jambo ambalo limerejesha utulivu,” amesema.
Wakizungumza na Mwananchi, baadhi ya wanafunzi wamesema uwekezaji miundombinu ya kisasa ya vyumba vya madarasa, matundu ya vyoo, maabara za kisasa unawapa morali ya kusoma kwa bidii.
Junior Pondo amesema anaishi na bibi yake, awali, kutokana na kuwepo kwa michango shuleni alikata tamaa kuendelea na masomo, lakini baada ya Serikali kuja na mfumo wa elimu bure, amepata tabasamu na kufanya bidii ya masomo ili atimize ndoto yake.