Ahly yathibitisha kumuacha nyumbani staa wake

Al Ahly imethibitisha kwamba kiungo wake Emam Ashour hayupo kwenye kikosi kitakachoivaa Yanga kesho kutokana na makosa ya kinidhamu.

Timu hiyo ipo Zanzibar ikitarajiwa kupambana na Yanga kwenye mchezo wa nne wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika utakaochezwa katika Uwanja wa New Amaan Complex.

Kocha wa Al Ahly, Jesse Thorup amethibitisha akisema Ashour hakusafiri na timu hiyo kutokana na makosa ya kinidhamu.

Thorup, raia wa Denmark amesema kiungo huyo atapewa adhabu kali kwa makosa ambayo ameyafanya ambapo timu hiyo itaendelea na mechi zake bila uwepo wake.

“Nathibitisha kwamba hatutakuwa na Ashour. Amefanya makosa ya kinidhamu na atapewa adhabu kali. Amebaki nyumbani,” amesema Thorup.

“Nimekuwa nasema tangu nimefika hapa hakuna mchezaji mkubwa kuliko timu. Staa peke tuliye naye hapa ni Al Ahly. Tunahitaji kuwa na nidhamu. Tumeshajiandaa kucheza mechi zinazofuata bila yeye. Tunataka kila mmoja atambue kwamba ukifanya makosa utachukuliwa hatua.”

Kukosekana kwa Ashour ni taarifa njema kwa Yanga, ingawa wapinzani wao wana wachezaji wengine bora akiwemo Hussein El Shahat.