KIWANGO cha kipa Aishi Manula ambacho ameendelea kukionyesha Azam FC kimemkosha Kocha Florent Ibenge, ambaye amesema kuwa klabu hiyo ilichanga vyema karata zake kwa kumsajili kipa huyo.
Manula safari yake ya soka ilianzia Azam kabla ya kutimkia Simba, ambako aliichezea kwa miaka saba na kupata mafanikio makubwa pamoja na timu ya Taifa.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ibenge amesemakama kuna hesabu nzuri Azam ilifanya ni kumsajili kipa Manula, kwani wamepata kipa wa daraja la juu.
AmesemaManula ameendelea kuonyesha uwezo mkubwa katika timu hiyo, ila hapo awali alikuwa anakutana naye akiwa mpinzani wake, lakini sasa anafurahia kiwango chake akiwa naye timu moja.
“Manula ni kipa wa daraja kubwa ambaye ataiisaidia sana Azam, siyo kwenye ligi tu bali hata kimataifa, kwani ana ujuzi wa kutosha unaotupa matumaini ya kufika mbali zaidi.
“Kuonyesha uwezo mkubwa alionao kwenye timu hiyo ni jambo linalonipa furaha sana, kwani mafanikio ya timu uwanjani ni yetu sote, hivyo kocha yeyote angetamani kuwa na wachezaji bora kwenye maeneo yote.”
Aliongeza; “Uwepo wa Manula Azam unawaimarisha makipa wengine kama Foba, ambao wanajifunza mengi kutoka kwa mkongwe huyo, hivyo siyo mchezaji tu bali ni mwalimu wa wengine.”
Katika mechi za hatua ya makundi ambazo Azam inaendelea kucheza, Manula amedaka mchezo mmoja dhidi ya Nairobi United huku akiruhusu bao moja, licha ya kwamba Azam ilipata matokeo.
Matajiri hao wa Chamazi wako kundi moja na Wydad ya Morocco, Union Maniema ya Kongo na Nairobi United ya Kenya, huku wakiwa na pointi 03 mpaka sasa, na kundi hilo likiongozwa na Waarabu.
Azam itarejea tena katika uwanja wa nyumbani, Amaan Complex ulioko Zanzibar, Jumapili hii ya Februari Mosi, ambapo itakutana tena na Nairobi United.