Iringa. Mkoa wa Iringa umeimarisha usimamizi wa kampeni ya upandaji miti kwa kuweka mfumo madhubuti wa ufuatiliaji na uwajibikaji.
Umesema lengo ni kutaka kuhakikisha miti inayopandwa inatunzwa na kukua, badala ya kupandwa kwa lengo la kutimiza takwimu za kampeni pekee.
Hatua hiyo imebainishwa leo Ijumaa Januari 30, 2026 katika Kijiji cha Ihemi, Wilaya ya Iringa, wakati wa kazi ya upandaji miti iliyoongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James kwa kushirikiana na wananchi na viongozi wa Serikali.
Akizungumza katika hafla hiyo, James ametoa agizo la siku 14 kwa taasisi zote za umma na binafsi kuhakikisha zinatekeleza kazi hiyo ya upandaji miti katika maeneo ya ofisi zao bila kisingizio chochote.
Amesisitiza kuwa kila taasisi ina wajibu wa kushiriki kikamilifu katika ulinzi na utunzaji wa mazingira, akieleza kuwa suala la mazingira si la hiyari bali ni wajibu wa kisheria na kimaadili.
Mkuu huyo amesema mkoa hautaridhika na takwimu za miche iliyopandwa pekee, bali utaangalia matokeo halisi ya uhai na ukuaji wa miti hiyo baada ya kupandwa.
Amesema changamoto kubwa iliyojitokeza katika kampeni zilizopita ni kukosekana kwa ufuatiliaji wa kutosha baada ya upandaji kukamilika.
“Mkoa umejipanga kuimarisha usimamizi kwa kushirikisha viongozi wa ngazi zote kuanzia mkoa, wilaya, tarafa, kata hadi vijiji, tunataka kila mti unaopandwa uwe na msimamizi mwenye dhamana,” amesema na kuongeza;
“Kipaumbele chetu siyo idadi ya miche inayopandwa pekee, bali ni kuona miti hiyo inakua, inalindwa na kuleta tija kwa mazingira na jamii.”
Ofisa Mazingira Mkoa wa Iringa, Dk Bahati Golyama amesema mpango huo ni sehemu ya mkakati wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuimarisha mazingira endelevu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Amesema mfumo wa ufuatiliaji utaangalia idadi ya miche iliyozalishwa, iliyogawiwa, iliyopandwa pamoja na kiwango cha miti iliyoota katika kila eneo.
Ameongeza kuwa tathmini za awali zinaonesha kuwa endapo usimamizi utaimarishwa ipasavyo, kiwango cha uotaji wa miti kinaweza kufikia zaidi ya asilimia 80.
Mhifadhi Misitu wa TFS Wilaya ya Iringa, Eutropia Mrema amesema TFS imezalisha miche ya aina mbalimbali ikiwamo ya matunda, vivuli, urembo pamoja na miche ya kibiashara kama mbao na nguzo.
Amesema miche hiyo inagawiwa bure kwa wananchi na taasisi, huku elimu ya utunzaji wa miti ikiendelea kutolewa ili kuongeza uhai wa miti baada ya kupandwa.
Wakizungumza na Mwananchi Digital, baadhi ya wananchi wa Mkoa wa Iringa wamesema wameipokea kampeni hiyo kwa mtazamo chanya, wakieleza kuwa msimamo wa uongozi wa mkoa unaonesha dhamira ya kweli ya kulinda mazingira na kuondoa mazoea ya kupanda miti bila ufuatiliaji.
“Hii ni hatua nzuri sana kwa sababu zamani tulikuwa tunapanda miti lakini hakuna aliyekuwa anauliza imeota mingapi. Ukali huu wa mkuu wa mkoa unatupa matumaini kuwa safari hii miti itatunzwa kweli,” amesema Elibariki Mhando, mkazi wa Ihemi.
Neema Mwakalinga mfanyakazi wa sekta binafsi mkoani Iringa, amesema agizo la siku 14 linaonesha mazingira sasa yamepewa uzito sawa na miradi mingine ya maendeleo.
“Taasisi zikisimamiwa, hata wananchi tutahamasika zaidi kutunza miti,” amesema.
Paulo Mgaya, mkulima wa Wilaya ya Iringa, amesema wanaunga mkono msimamo wa mkoa lakini ameitaka Serikali kuhakikisha ufuatiliaji unafanyika hadi ngazi ya vijiji. “Miti ikitunzwa italinda vyanzo vya maji na hata kuongeza kipato chetu,” amesema.