Othman: Jitihada za kuondoa mkwamo wa kisiasa Zanzibar zipo hatua muhimu

Unguja. Mwenyekiti wa Taifa wa ACT Wazalendo, Othman Masoud amesema jitihada za kupata suluhisho la mkwamo wa kisiasa uliotokana na uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025 visiwani Zanzibar zipo katika hatua muhimu, akisisitiza kuwa mazungumzo yanayoendelea yanalenga kuleta maridhiano ya kweli na amani ya kudumu kwa Wazanzibari.

Othman ametoa kauli hiyo leo Januari 30, 2026, wakati akizungumza na waumini na wananchi baada ya sala ya Ijumaa iliyosaliwa katika Msikiti wa Jasmi, Kijiji cha Kiyongwe, Bumbwini, Wilaya ya Kaskazini B, Unguja.

Kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar, Serikali inaundwa na vyama viwili: chama kinachoshinda katika uchaguzi mkuu na chama kinachopata asilimia 10 ya kura zote zilizopigwa.

Katika matokeo ya uchaguzi, Chama cha Mapinduzi (CCM) kiliibuka na ushindi kwa asilimia 74 huku ACT kikapata asilimia 23.4, ambazo zinakipa fursa ya moja kwa moja kuingia kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).

Hata hivyo, tangu umalizike uchaguzi huo, chama cha ACT bado hakijateua jina la atakayekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais na majina ya watu wanne ambao watathibitishwa na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, kuwa mawaziri.

Sababu kubwa ambayo imekuwa ikitajwa na chama hicho ni kwamba uchaguzi huo haukuwa wa haki, wakidai kuwa kulikuwa na dhuluma, na kufikia hatua ya kufungua kesi mahakamani katika majimbo 33 ya ubunge Unguja na Pemba.

Hata hivyo, tayari mashauri hayo yote yametupiliwa mbali na Mahakama Kuu ya Zanzibar baada ya kukubali pingamizi zilizowekwa na Mwanasheria Mkuu wa Tanzania Bara na Tume Huru ya Uchaguzi, kwamba Mahakama Kuu ya Zanzibar imefungwa kikatiba kusikiliza kesi zinazohusu uchaguzi wa wabunge.

Mwenyekiti wa Taifa wa Chama Cha ACT Wazalendo, Othman Masoud akizungumza na waumini na wananchi baada ya sala ya Ijumaa iliyosaliwa katika Msikiti wa Jasmi, Kijiji cha Kiyongwe, Bumbwini, Wilaya ya Kaskazini B, Unguja.



Akifafanua kuhusu mustakabali wa nchi baada ya uchaguzi wa mwaka jana, Othman, ambaye alikuwa mgombea wa urais wa Zanzibar kupitia chama hicho, amewahakikishia wananchi kuwa viongozi wao wanashughulikia mgogoro huo kwa dhati ili kuepuka suluhu za juu juu.

“Viongozi wenu mmetupa dhamana hii, nasi tunaendelea kwa dhati kupigania utulivu wa kweli, amani ya kweli, maridhiano ya kweli na suluhu ya kudumu, wala si funika kombe,” ameeleza Othman.

Othman, ambaye alikuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar katika kipindi cha kwanza cha utawala wa Serikali ya awamu ya nane, amesema: “Vyeo ni dhamana na si fursa ya kujilimbikizia mali binafsi.”

Kwa mujibu wa Othman, kuna haja ya kurudi katika asili ya Zanzibar inayojulikana kwa ustaarabu, maadili na mshikamano kutokana na misingi yake ambayo hata mataifa makubwa yaliyotawala zamani yaliheshimu sheria zake, ikiwemo Mahakama ya Kadhi na Wakfu.

Hata hivyo, kiongozi huyo ameonyesha kusikitishwa na mmomonyoko wa uadilifu kwa baadhi ya watu wanaoweka maslahi binafsi mbele ya haki za jamii.

“Leo kuna watu wanaona dhuluma ni jambo la kawaida, wanakula haki za watu, na fitna ya kipato imewekwa kubwa kuliko ya nafsi,” amesema.

Kwa upande wake, Khatibu wa sala hiyo, Sheikh Juma Hamad Makame, ametoa onyo kwa viongozi wanaotumia nguvu kupora haki za wananchi, akibainisha kuwa uongozi ni uchungaji na lazima upatikane kwa ridhaa ya watu.

“Kila kiongozi anatakiwa ahakikishe anapata uongozi wake kwa ridhaa ya wananchi wake, pamoja na kuhakikisha wanapata haki zao bila kubughudhiwa,” amesema Sheikh Juma.