Mwanza. Vyama vya msingi vya ushirika (Amcos) vitakavyoshindwa kuzalisha angalau kilo 10,000 za pamba kwa mwaka vitafutwa kuanzia msimu ujao, ikiwa ni mkakati wa Serikali kupunguza vyama visivyo na tija na kuimarisha uzalishaji wa zao la pamba mkoani Mwanza.
Kauli hiyo imetolewa leo Ijumaa Januari 30, 2026 na Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Mwanza, Hilda Boniface, wakati wa mkutano mkuu wa 34 wa Chama Kikuu cha Ushirika Nyanza (NCU 1984).
Boniface amesema licha ya Mkoa wa Mwanza kuwa na jumla ya vyama vya ushirika 249, uzalishaji wa pamba bado uko chini kwa kiasi kikubwa, hali inayosababisha vyama vingi kushindwa kujiendesha kiuchumi na kushindwa kuchangia maendeleo yanayotarajiwa.
“Vyama ni vingi, tunavyo 249 mkoani Mwanza, lakini uzalishaji uko chini sana; hii haiendani na fursa tulizonazo. Kizuri zaidi ni kwamba chama chetu cha Nyanza kimeamua kufufua kiwanda cha kuchakata pamba, lakini kiwanda hiki kinahitaji pamba ya kutosha… ni lazima tujiandae kisaikolojia na kimkakati kuhakikisha tunazalisha kwa ajili ya Nyanza,” amesema.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilemela, Mariam Msengi akizungumza kwenye mkutano mkuu wa mwaka wa 34 wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Nyanza (NCU 1984) uliofanyika jijini Mwanza. Picha na Saada Amir
Amesema Amcos yoyote itakayobainika kuendelea kuzalisha chini ya kilo 10,000 za pamba kwa mwaka, itafutwa kuanzia mwaka 2027 kwa kuwa tayari wameanza kufanya tathmini ya uzalishaji shambani, akisisitiza uzalishaji mdogo hauwezi kujenga uchumi imara wala kuleta maendeleo.
“Wewe unazalisha kilo 1,000 au 2,000, kuna uchumi imara hapo? Hakuna. Hatuwezi kuendelea kuwa na vyama vinavyoleta usanii… chama kinapaswa kuweza kulisha kiwanda, kulipa tozo za Serikali, kulipa mishahara ya makatibu na mameneja kwa mujibu wa sheria, na kutoa posho za wajumbe wa bodi,” amesema.
Amesema vyama vitakavyoshindwa kutimiza vigezo hivyo vitafutwa na badala yake vitabaki kama vituo vya kununulia pamba, huku akisisitiza kuwa Serikali iko tayari kubaki na vyama vichache mradi viwe na nguvu kiuchumi.
“Kama mkoa, tupo tayari kubaki na vyama hata 100, lakini viwe vyenye uwezo wa kujiendesha, kuendesha shughuli zake zote, kulipa mishahara na kufanya uwekezaji,” amesema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya NCU 1984, Leonard Jabalima, amesema uzalishaji wa pamba umekuwa ukishuka mwaka hadi mwaka, lakini changamoto hizo zinaweza kudhibitiwa endapo vyama vitaweka mkazo katika kuhakikisha wanachama wao wanalima zao hilo kwa tija.
Amesema chama kitaendelea kutoa elimu ya kilimo bora cha pamba ili kuongeza uzalishaji, akibainisha kuwa katika baadhi ya nchi, mkulima huzalisha kati ya kilo 1,000 hadi 2,000 kwa ekari moja, tofauti na kwa wanachama wao ambao uzalishaji bado uko kati ya kilo 300 hadi 400.
Baadhi ya wanachama wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Nyanza (NCU 1984) wakiwa kwenye mkutano wao mkuu wa mwaka wa 34. Picha na Saada Amir.
“Gap (pengo) ni kubwa sana. Tukiongeza uzalishaji, tutaongeza uwekezaji na kufungua milango ya masoko ya nje yanayonunua pamba kwa bei nzuri,” amesema.
Ameongeza kuwa ujenzi wa kiwanda kipya cha kuchakata pamba wilayani Magu unaendelea, ambapo zaidi ya Sh3 bilioni zinatumika, huku baadhi ya mitambo ikiwa tayari imewasili na usimikaji ukiendelea.
“Msimu wa pamba wa 2025/26, NCU itaingia sokoni kama mshindani wa wanunuzi wengine. Hii italeta faraja kwa wakulima kwa kuwa watapata fursa ya kuuza pamba kwenye kiwanda chao wenyewe,” ameeleza.
Mbali na zao la pamba, Jabalima amesema chama kinaendelea na uwekezaji wa ufugaji wa samaki kwa vizimba, ambapo tayari vizimba vimeongezeka kutoka vinne hadi 12, lengo likiwa ni kuanzisha kisiwa cha vizimba Ziwa Victoria.
Amesema Sh2.5 bilioni zinatarajiwa kutumika kuanzisha vizimba 100 katika Wilaya ya Buchosa, akieleza kuwa ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba bado ni fursa kubwa ambayo haijatumika kikamilifu.
Akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilemela, Mariam Msengi, ameitaka NCU na watendaji wake kuongeza kasi na ufanisi ili kuhakikisha ujenzi wa kiwanda cha kuchakata pamba unakamilika kwa wakati.
“Nawahamasisha wanachama kuongeza uzalishaji wa pamba ili kuhakikisha kiwanda kinapata malighafi ya kutosha na kuleta manufaa yaliyokusudiwa,” amesema.
Amesema Serikali imepokea malalamiko kutoka kwa wakulima kuhusu ucheleweshaji wa pembejeo ikiwemo mbegu na viuatilifu na kuwataka viongozi na watendaji wa Amcos kusimamia upatikanaji wa pembejeo kwa wakati, urahisi na kwa haki.
Kuhusu changamoto ya wakulima kupunjwa wakati wa upimaji wa mazao, Mtanda amesisitiza matumizi ya mifumo ya kidijitali ili kuongeza uwazi na kulinda haki za wakulima.