Serikali yaagiza tathmini ya nyumba zilizojengwa eneo la mwekezaji

Shinyanga. Serikali imeagiza kufanyika kwa tathmini ya nyumba zilizojengwa katika eneo la mwekezaji lililopo Mtaa wa Butengwa, Manispaa ya Shinyanga.

Imeelezwa kwamba lengo ni kutaka kubaini idadi ya wananchi waliovamia na kujenga bila kibali cha Ofisi ya Ardhi, kufuatia mgogoro wa ardhi uliodumu kwa zaidi ya miaka minane sasa.

Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro, leo Ijumaa Januari 30, 2026, wakati wa ziara yake ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi katika Kata za Ibinzamata na Ndembezi, ili kuchukua hatua na kumaliza mgogoro huo.

Mtatiro amesema migogoro ya ardhi inakwamisha maendeleo ya wananchi kutokana na kushindwa kuyaendeleza maeneo yao, pamoja na kutumia muda na rasilimali nyingi kusaka ufumbuzi wa migogoro hiyo.

Mkuu huyo wa wilaya amesema hali hiyo inasababisha pia kukosekana kwa huduma muhimu za kijamii ikiwamo umeme, maji na miundombinu ya barabara.

“Inasikitisha kuona watu wakijua kabisa eneo lina mgogoro, lakini bado wanaendelea kujenga. Wanajua wazi kuwa Tanesco haiwezi kupeleka umeme, Shuwasa haiwezi kupeleka maji, wala huduma nyingine za kijamii haziwezi kutolewa hadi mgogoro utakapomalizika,” amesema Mtatiro.

Ameongeza kuwa wananchi wanapaswa kufuata taratibu halali za kununua viwanja kupitia Idara ya Ardhi ili kuepuka kudhulumiwa na matapeli wanaotumia mwanya wa migogoro ya ardhi kuuza viwanja kinyemela, jambo linalochochea na kuongeza migogoro.

Akitoa ufafanuzi kuhusu eneo hilo, Ofisa Ardhi wa Manispaa ya Shinyanga, Jacob Mwinuka, amesema ofisi yake haijawahi kutoa kibali chochote cha ujenzi katika eneo la Butengwa, akieleza kuwa eneo hilo linatambuliwa rasmi kuwa ni la mwekezaji Kaseki tangu mwaka 1994.

Baadhi ya wananchi waliovamia na kujenga nyumba za makazi katika eneo hilo lenye nyumba zaidi ya 50, wamesema waliuziwa viwanja na wenyeji wa eneo hilo.

Miongoni mwao ni Saraphina Robart, mkazi wa Ndembezi, aliyedai kuwa alinunua kiwanja kutoka kwa wananchi waliodai kurithi mashamba hayo kutoka kwa babu zao.

Mkazi mwingine wa Butengwa, James Pius, amesema mgogoro huo umedumu kwa muda mrefu tangu mwaka 2017 bila kupatiwa ufumbuzi wa kudumu, hali iliyomsukuma kuiomba serikali ichukue hatua za haraka kumaliza tatizo hilo.

Kwa upande wake, mwakilishi wa mwekezaji Kaseki, Rose Saramba, amesema wananchi walianza kuvamia eneo hilo na kujenga bila kufuata taratibu baada ya kuuziwa viwanja kwa njia za kinyemela, hatua iliyosababisha mwekezaji kutoa taarifa kwa mamlaka ya ardhi na kuanza kufuatilia suala hilo kisheria.