Dakika 720 bila ushindi Mbeya City, Maxime, Baraza waenda kujipanga upy

MBEYA City imeendeleza ukame wa ushindi katika Ligi Kuu Bara baada ya kupata sare ya bao 1-1 dhidi ya Pamba Jiji na kuendelea kuwa miongoni mwa timu tatu za mkiani katika msimamo, huku presha ikizidi kupanda kwenye vita ya kukwepa kushuka daraja.

Baada ya mechi hiyo, Mbeya City inafikisha mechi ya nane mfululizo sawa na dakika 720 bila kupata pointi tatu tangu ilipopata ushindi Oktoba 18, 2025 ilipoifumua KMC 3-0 ugenini.

Matokeo hayo yanaifanya City ambayo leo ilipewa sapoti na madiwani wa Halmashauri hiyo katika Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya kubaki nafasi ya 14 kwa pointi tisa baada ya mechi 12 ilizocheza, ikiishusha Tanzania Prisons yenye pointi nane na mechi tisa.

Katika mechi ya leo Januari 30, 2026, Mbeya City ilitangulia kupata bao kupitia kwa Adilly Buha dakika ya 21 kabla ya Kelvin Nashon kusawazisha dakika ya 30.

Mbeya City ikicheza na baadhi ya mastaa wake waliosajiliwa dirisha dogo akiwamo Kelvin Kijiri, Yacouba Sogne na Hassan Dilunga, haikuwa na mabadiliko yoyote ya matokeo zaidi ya sare hiyo.

Kocha Mkuu wa Mbeya City, Mecky Maxime, amesema pamoja na matokeo hayo, lakini watajilaumu kwani wamepata nafasi nyingi lakini umaliziaji ndio ulikuwa butu na kuahidi kufanyia kazi makosa hayo.

“Bado ni mapema lakini mechi ilikuwa rahisi na wazi kwetu kushinda, tumepata nafasi zaidi ya nne lakini tumeshindwa kuzitumia, tunaenda kujipanga na mchezo ujao dhidi ya Dodoma Jiji,” amesema Maxime.

Kocha Mkuu wa Pamba Jiji, Francis Baraza amesema pointi moja dhidi ya wapinzani hao ugenini si mbaya kwao japokuwa mkakati ulikuwa ni kushinda na kwamba anawapongeza nyota wake kwa kazi nzuri.

“Niwapongeze wachezaji kwakuwa wameonesha ushindani, tumeshambulia sana lango la wapinzani na tumeondoka na pointi, tunaenda kujipanga upya na mechi inayofuata,” amesema Baraza.

Pamba Jiji sare hiyo imeipandisha nafasi mbili kutoka ya sita hadi ya nne ikifikisha pointi 17 baada ya mechi 11 ikizishusha Simba na Azam zenye 16.