DC Itunda atoa mwelekeo miradi ya maendeleo Halmashauri ya Jiji Mbeya

Mbeya. Madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya wametakiwa kusimamia kwa karibu miradi yote inayotekelezwa na Serikali katika maeneo yao, kuacha migogoro isiyo ya lazima baina yao na watendaji, na kuwa kiungo muhimu cha mahusiano ili kuharakisha maendeleo ya wananchi.

Aidha, wametakiwa kuongeza juhudi katika kusimamia zoezi la uandikishaji wa wanafunzi ambalo kwa sasa limefikia zaidi ya asilimia 70, huku lengo likiwa ni kukamilisha kabla ya Machi mwaka huu.

Akizungumza leo Ijumaa, Januari 30, 2026, katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Solomon Itunda amesema licha ya kazi nzuri inayofanywa na madiwani, bado wanapaswa kuimarisha usimamizi wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwa gharama kubwa katika maeneo yao.

Itunda amesema Jiji la Mbeya limepata mafanikio makubwa katika sekta ya elimu kwa kushika nafasi ya tatu kitaifa katika matokeo ya madarasa ya mitihani, akiwataka madiwani kuongeza nguvu katika kuhakikisha watoto wote wanaandikishwa shuleni mwaka huu.

“Hadi sasa tumefikia asilimia 70 ya uandikishaji wa watoto, tunahitaji kabla ya mwezi Machi tukamilishe zoezi hili. Pia ipo miradi mikubwa ya kimkakati iliyogharimu fedha nyingi, naomba isimamiwe kikamilifu,” amesema Itunda.

Ameongeza kuwa madiwani hawapaswi kukubali migogoro baina yao, watendaji na wananchi, bali wawe sehemu ya kuunganisha pande husika pale panapotokea tofauti, kwa lengo la kuwaletea wananchi maendeleo.

“Pokeeni, sikilizeni na mtatue kero za wananchi badala ya kuruhusu migogoro kuendelea,” amesisitiza.

Itunda amesema katika siku 100 za Rais, Samia Suluhu Hassan, Serikali imeongeza fedha za mradi wa ujenzi wa barabara ya njia nne kutoka Shilingi bilioni 138 hadi Shilingi bilioni 183, huku mradi wa maji wa Mto Kiwira unaogharimu zaidi ya Shilingi bilioni 119 ukiwa umefikia asilimia 50 ya utekelezaji.

Amesema zaidi ya Sh107 bilioni zimetolewa kwa ajili ya utekelezaji wa huduma ya umeme kwa kipindi cha miaka miwili, pamoja na Shilingi milioni 400 kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya Jeshi la Polisi, akibainisha kuwa hatua hizo ni juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita katika kuimarisha huduma za kijamii.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Mwasanga, Brand Nelson amesema madiwani wanatarajia kufanya kampeni ya kuelimisha wananchi kwa kupita nyumba kwa nyumba na mtaa kwa mtaa ili kuwahamasisha kuwaandikisha na kuwapeleka watoto shuleni.

“Asilimia tuliyofikia si ya kuridhisha, hivyo tumepokea maelekezo na tunaelekea kwenye utekelezaji. Binafsi nitapita nyumba kwa nyumba kuwaelimisha wananchi kuwapeleka watoto shule,” amesema Brand.

Naye Diwani wa Kata ya Uyole, Benjamin Mwandete, amesema katika kata yake wamefikia asilimia 83 ya uandikishaji wa watoto, huku akiendelea kuimarisha jitihada za kuhamasisha zoezi hilo.

Kuhusu usimamizi wa miradi, Mwandete amesema ataendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kuhakikisha ukusanyaji na matumizi sahihi ya mapato, pamoja na kudhibiti ufujaji wa fedha za umma.