Wazazi wahimizwa kuzungumza na watoto kuhusu afya ya uzazi

Dar es Salaam. Mila potofu, ukosefu wa mawasiliano kati ya wazazi na watoto, pamoja na mitandao ya kijamii imeibua changamoto katika upatikanaji wa elimu sahihi ya afya ya uzazi miongoni mwa vijana, imedaiwa leo na Mwezeshaji wa Kitaifa wa Masuala ya Afya ya Uzazi, Dk Tarama Ndossi.

Dk Ndossi amesema hayo leo Januari 29, 2026 wakati wa mafunzo kwa vijana kutoka vyuo mbalimbali jijini Dar es Salaam, yaliyofanyika kupitia mradi wa AHADI, unaosimamiwa na Shirika la World Vision kwa kushirikiana na Taasisi ya BabaWatoto.

Mafunzo hayo yamelenga kutoa elimu ya afya ya uzazi na kujitambua kwa vijana na tayari yamewafikia zaidi ya vijana 400.

Amesema vijana wanatumia muda mwingi katika mitandao ya kijamii badala ya kuzungumza na wazazi wao, hali inayochangiwa na upweke wa wazazi kutokana na shughuli za kutafuta kipato na hofu ya kuwashirikisha watoto masuala ya kingono mapema.

“Wazazi, umefika wakati wa kuvunja ukimya na kuzungumza na watoto kuhusu afya ya uzazi. Tusisubiri madhara yatokee,” alisisitiza Dk Ndossi.

Ameongeza kuwa taarifa sahihi na elimu ya afya ya uzazi ni muhimu katika makuzi ya watoto na vijana kwani itawawezesha kufanya maamuzi sahihi na kujitambua vyema.

Utafiti wa ‘The importance of parental communication on relationship and sexuality’, uliochapishwa kwenye tovuti ya ‘sexualwellbeing’, unaonyesha kuwa watoto na vijana, hasa wenye umri wa miaka 13, wanapendelea wazazi kuwa chanzo cha kwanza cha taarifa sahihi kuhusu masuala ya jinsia na afya ya uzazi.

Rajabu Makame, mratibu wa mradi wa AHADI, amesema elimu ya afya ya uzazi itasaidia kupunguza mimba za utotoni, kuhamasisha vijana kujitunza, na kuwalinda dhidi ya magonjwa ya zinaa.

Aidha, ameeleza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali, wadau wa afya, wazazi, haki za kiraia na wataalamu wa afya katika kutoa elimu kwa jamii.

Makame pia amesisitiza jukumu la vyombo vya habari: “Ripoti siyo tu matukio, bali tutumie kalamu zetu kutoa elimu kwa jamii na kushawishi watunga sera kuchukua hatua.”

Elimu ya afya ya uzazi pia inachangia maarifa ya kiuchumi na afya ya akili kwa vijana, ikiwasaidia kukabiliana na changamoto mbalimbali za maisha.

Mradi wa AHADI tangu kuanzishwa mwaka 2022, umewafikia vijana zaidi ya 400 katika kata 18 za Dar es Salaam.

Lucia Mbogo, mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, amesema ukuaji wa teknolojia ni ishara kwa wazazi kuvunja ukimya na kuwa wazi katika kuwafundisha watoto kuhusu masuala ya afya ya uzazi ili kupata taarifa sahihi.