Akizungumza katika mkutano na vyombo vya habari katika ofisi za BoT jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Masoko ya Fedha wa BoT, Bw. Emmanuel Akaro, ameeleza kuwa kinachotekelezwa ni mpango wa kuuza dhahabu iliyozidi kiwango kilichoidhinishwa, kwa lengola kusawazisha mizania ya akiba ya fedha za kigeni nchini.
“Sababu ya Benki Kuu kuuza dhahabu ni kujitoa kwenye vihatarishi vya kuwekeza kwenye dhahabu peke yake. Lazima tuhakikishe uwiano wa dhahabu na fedha nyingine za kigeni kwenye mizania ya Benki Kuu zinaendana na matarajio ya Bodi, matarajio ya nchi na matarajio ambayo hayatupelekea sisi kupata hasara”
Mkurugenzi huyo amefafanua kuwa wastani wa kununua dhahabu wa mwezi ni tani moja na kwa kipindi cha mizezi mitano iliyopita BoT imenunua wastani wa tani mbili,hivyo, kulazimika kuwekeza tani moja ya ziada katika fedha za kigeni mbalimbali.
“Kwa kipindi cha miezi mitano iliyopita kila mwezi tunanunua dhahabu wastani wa tani 2 kwa mwezi ambayo ni kwa mujibu wa sheria. Matarajio yetu mwanzoni yalikuwa ni kununua tani moja kila mwezi kwa hiyo tani moja inayozidi tunaitumia kusawazisha mizania ya akiba za fedha za kigeni”
“Kuna utaratibu wa namna ambavyo Benki Kuu inatoa fedha kwenda serikalini,fedha zinapitia Mfuko Mkuu na uidhinishwaji wake unakuwa umefanywa na Bunge na ukiangalia pale hakuna kipengele ambacho kinasema Benki Kuu inaweza kuuza dhahabu ili kuipatia serikali fedha kwaajili ya kufanya miradi yake”, aliongeza Bw. Akaro.
Hadi kufikia jana Januari 29, 2026, BoT ilikuwa na akiba ya fedha za kigeni yenye thamani yadola bilioni 6.52, na kati ya hizo, dhahabu inakadiriwa kuwa dola bilioni 1.2, dola za Marekani bilioni 3.8, na sarafu ya China (yuan) dola milioni 735.



