Dar es Salaam. Siku mbili baada ya wabunge wawili kuzungumzia uwepo wa mafisadi nchini, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru) imejitosa katika suala hilo huku ikisubiri maelezo kamili kutoka kwa wabunge hao ili wazifanyie kazi.
Hata hivyo, wachambuzi wa siasa wamemulika kauli za wanasiasa hao wakihimiza haja ya hoja zao kufikishwa kwenye vyombo husika ili zisiishie tu kwenye mjadala wa kibunge, bali zifanyiwe kazi na hatua za kisheria zichukuliwe.
Jana, Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola, alisema ili kumaliza mafisadi na wabadhirifu wote nchini na kuipata ‘Tanzania mpya’, ni lazima vyombo vya dola, kwa maana ya Jeshi la Polisi na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), viwe huru.
Mbali na hayo, alisema watu aliowaita ‘machawa’ ndiyo wameifikisha nchi hapa, akitaka wabunge wawe huru wasibanwe, ikiwemo na vikao vya chama chao cha CCM, ili wawashughulikie kwa lengo la kumsaidia Rais Samia Suluhu Hassan.
Lugola, mbunge wa Mwibara, Mkoa wa Mara, alitoa kauli hiyo siku moja baada ya mbunge mwingine wa chama hicho wa Gairo, Ahmed Shabiby, kueleza kuwa Tanzania bado ina mafisadi wengi na wanakula kuliko inavyodhaniwa.
Shabiby alikwenda mbali zaidi kwa kusema yuko tayari kuwataja kwa majina yao kama itahitajika, huku akiwataka wasaidizi wa Rais Samia kumsaidia ipasavyo na kuachana na mipango ya kujipanga na urais mwaka 2030.
Wabunge hao wameibua hoja za ufisadi huo bungeni wakati wakichangia hotuba ya Rais Samia aliyoitoa alipolizindua Bunge la 13, Novemba 14, 2025. Shabiby alitoa kauli hiyo Januari 28 na jana Januari 29, 2026, Lugola alizungumza tena kwa msisitizo.
Akizungumzia kauli za wanasiasa hao, leo Januari 30, 2026, Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Crispin Chalamila, amesema wameisikia kauli ya Shabiby na kwamba wanasubiri apeleke taarifa rasmi alizonazo.
“Kwa wajibu tu wa kiraia na kizalendo, Shabiby atakuja (Takukuru), ataleta rasmi hizo taarifa pengine kuliko namna alivyofanya. Kwa hiyo tutamtafuta atupe hizo taarifa kama taasisi na kama hatotufuata, sisi tutamtafuta atupe taarifa alizonazo tuzifanyie kazi,” amesema Chalamila.
Profesa wa Uchumi, Samuel Wangwe, amesema kilichozungumzwa na wabunge hao kinafahamika kwa wananchi.
“Waliyoyasema, watu wengi wa kawaida wanafahamu, kwa hiyo hawakupata tu sehemu ya kusemea, hata kwenye ziara ya Waziri wa Vijana, Joel Nanauka, wakati akizunguka kuzungumza na vijana, baadhi ya mambo kama hayo yalijitokeza, hivyo ni kweli,” amesema.
Profesa Wangwe amesema hata sera za CCM zinakataa masuala ya ufisadi na rushwa, hivyo ufisadi unapaswa kupigwa vita.
Mtaalamu huyo wa uchumi amesema pamoja na kwamba wabunge hao walisema anawafahamu mafisadi hao, wananchi nao wanawafahamu lakini sio kazi ya mbunge kuwataja kwani vipo vyombo vya kufanya kazi hiyo.
“Tuna vyombo vya maadili, Takukuru, usalama wa taifa kwenye usalama, usalama wanapaswa kulinda usalama wa uchumi, kwa hiyo hivyo vyombo vilivyoundwa kwa ajili ya kazi hiyo vifanye kazi, kama kuna udhaifu uelezwe lakini vifanye kazi yake,” amesema.
Akichangia hoja hiyo, mchambuzi wa masuala ya siasa, Profesa Ali Makame, amesema tuhuma hizo zipo lakini kuna namna ambayo Serikali inashughulika nayo kupitia vyombo vya uchunguzi baada ya taarifa kuwasilishwa.
“Kuwe na madai au shutuma ambazo zimewasilishwa ili vyombo hivi viwe na kazi ya kufanya uchunguzi wa kufuatilia taarifa zinazotiliwa shaka,” amesema.
Profesa Makame amesema taarifa hiyo ya ufisadi inapaswa kufika kwenye vyombo vya sheria na kwamba kuzungumza bungeni pekee ni kuleta taharuki kwa wananchi.
Amesema shutuma zinazotolewa za ufisadi zinapaswa kushughulikiwa kisheria na wahusika wafikishwe mahakamani ili haki itendeke.
Profesa Makame amesema shutuma hizo zisiishie kumzungumzia mtu na suala hilo kuishia njiani kwa kuwa jamii itaachwa katika ombwe la taarifa.
“Ni vema mambo haya yakachukuliwa kwa uzito wake kwa sababu ni ya busara, mali za umma zinapaswa kutumika kwa maslahi ya watu wote, kama ni kweli, wanaofanya ufisadi wanatuhujumu wananchi wote,” amesema.
Mwanazuoni huyo amesisitiza kwamba tuhuma za watu kufanya ufisadi na kujificha kwenye uchawa, mihimili iliyopo kila mmoja ufanye kazi yake na kuwa Bunge si eneo la kuhukumu, bali kuzungumza na kutafuta ukweli wa mambo yaliyopo na kushinikiza Serikali kutimiza wajibu wake.
Kupinga rushwa ni moja ya msimamo wa CCM uliotajwa kwenye katiba yake, hivyo kilichozungumzwa na wabunge hao kinaendana na matakwa ya chama chao kilichoasisiwa mwaka 1977 baada ya kuungana kwa TANU na ASP.
Katika ahadi tisa za wanachama wa CCM, ahadi ya nne inasema “Rushwa ni adui wa haki, sitapokea wala kutoa rushwa”. Ahadi ya tano inasema “Cheo ni dhamana, sitatumia cheo changu wala cha mtu mwingine kwa faida yangu.”
Vilevile, sehemu ya kwanza ya katiba ya CCM inayofafanua Jina, Imani na Madhumuni, inaeleza malengo na madhumuni ya chama hicho.
Kifungu cha 14 kinataja dhumuni la: “Kuona kwamba matumizi ya utajiri wa Taifa yanatilia mkazo maendeleo ya Wananchi na hasa jitihada za kuondosha umasikini, ujinga na maradhi.”
Kifungu cha 15: “Kuona kwamba Serikali na vyombo vyote vya umma vinatoa nafasi zilizo sawa kwa raia wote, wanawake na wanaume bila kujali rangi, kabila, dini, au hali ya mtu.”
Viongozi wa CCM walipotafutwa kuzungumzia kauli za wabunge wao, siyo Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenan Kihongosi, wala Katibu wa Wabunge wa CCM, Agnes Hokololo, aliyepatikana kuzungumzia suala hilo.
Hata hivyo, Katibu wa zamani wa Kamati Maalumu ya Idara ya Itikadi na Uenezi ya CCM Zanzibar, Catherine Nao, amesema kilichosemwa na viongozi hao kipo na hakipaswi kubezwa.
Amesema walichozungumza Shabiby na Lugola ni taarifa ambazo wana uhakika nazo kwa kuwa viongozi hao wana uzoefu bungeni na wanafahamiana kwa tabia.
“Hao viongozi wanafahamiana, kwamba ukipita njia hii unakutana na nani, ninavyoamini kwa akili za binadamu, hadi mtu anakuwa mbunge huwezi kuzungumza jambo bila kuwa na uhakika, lazima kuna chembe ya uhakika, hawa wanafahamu nini kinaendelea,” amesema kada huyo wa CCM.
Catherine amewapongeza wabunge hao kwa kuibua mambo hayo bila hofu akisema hadi mtu anaeleza kuwa anaweza kutaja mafisadi hapaswi kupuuzwa.
Amesema kwa kuwa wabunge wote ni wa chama tawala, mawazo yao yanapaswa kuunganishwa na kufanyiwa kazi.