Uganda. Seneta wa Marekani Jim Risch, ambaye pia ni mwenyekiti wa Kamati ya Seneti ya Mahusiano ya Kigeni, amekataa msamaha wa umma uliotolewa na Mkuu wa Majeshi wa Uganda, Jenerali Muhoozi Kainerugaba, akiutaja kuwa usio na maana, huku akitoa wito wa kutaka vikwazo vikali zaidi dhidi ya Uganda.
Majibu hayo yametolewa ikiwa ni siku moja baada ya Mohoozi kuomba radhi kupitia mtandao wa X kutokana na matamshi yake kwa Ubalozi wa Marekani nchini Uganda.
Mtandao wa BBC Swahili umeeleza kuwa, katika taarifa iliyotolewa jana Ijumaa, Januari 30, 2026, Risch amesema Muhoozi, ambaye ni mtoto wa Rais Yoweri Museveni, amevuka mipaka yake licha ya kufuta ujumbe kwenye mitandao ya kijamii na kuomba msamaha kwa Marekani.
Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo amesema, Marekani itatathmini upya ushirikiano wake wa kiusalama, unaojumuisha vikwazo na ushirikiano wa kijeshi na Uganda.
Seneta wa Marekani aliongeza kuwa nchi yake “haitavumilia hali ya mashaka kiwango hiki na uzembe”.
Jenerali Muhoozi, ambaye pia ni mshauri mkuu wa Rais Museveni kuhusu oparesheni maalumu za kijeshi, alidai kuwa uongozi wa sasa wa Ubalozi wa Marekani nchini Uganda ulihusika kumsaidia Robert Kyagulanyi maarufu Bobi Wine kuondoka nyumbani kwake Magere,
Awali, katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa X (zamani Twitter), Jenerali Muhoozi alisema:
“Wananchi wenzangu wa Uganda, kutokana na hali ya sasa ambapo kiongozi wa upinzani amejiteka mwenyewe na kutoweka na kwa mujibu wa taarifa zetu za kijasusi, vitendo hivi vilifanyika kwa ushirikiano na uongozi wa sasa wa Ubalozi wa Marekani nchini mwetu.
Kwa sababu hiyo, UPDF imesitisha ushirikiano wote na uongozi wa sasa wa Ubalozi wa Marekani jijini Kampala. Hii inajumuisha pia ushirikiano wetu nchini Somalia.
Ushirikiano wa kiusalama uliokuwa wa thamani kubwa kati ya Uganda na Marekani umeathiriwa vibaya tangu mwaka 2015 na watendaji wa urasimu wasio na ubunifu katika ubalozi huo”.
Baadaye, Jenerali Muhoozi alifuta ujumbe huo na kutoa radhi kwa kauli zake.
Mkuu huyo wa Majeshi ameomba msamaha kwa Marekani kwa matamshi yake ya awali kwenye mitandao ya kijamii ambayo yalikuwa yametilia shaka ushirikiano wa kijeshi unaoendelea kati ya Kampala na Marekani.