Refa kutoka Cameroon Antoine Effa Essouma ndiye atachezesha mechi ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu baina ya Yanga na Al Ahly, leo Jumamosi, Januari 31, 2025 katika Uwanja wa New Amaan Complex kuanzia saa 10:00 jioni.
Essouma ana kumbukumbu mbaya nchini kwani alikataa bao la Azam FC katika mchezo wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Novemba 28, 2025 lililofungwa na Japhte Kitambala.
Sababu ya Essouma kulikataa bao hilo ilidaiwa kuwa mchezaji mmoja wa Wydad alifanyiwa faulo wakati wa shambulizi lililozaa bao hilo lakini picha ya marudio ya luninga, zilizonyesha kuwa hakukuwa na faulo iliyofanyika.
Katika mchezo huo, Azam FC ilijikuta ikilala kwa bao 1-0.
Kwa mchezo wa leo, Essouma atasaidiwa na Rodrigue Mpele na Nkemazem Vincent huku mwamuzi wa akiba akipangwa kuwa Fodouop Yanick, wote wakiwa wanatoka Cameroon.
‘Mmakonde’ akabidhiwa lawama ya Simba, Esperance
Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limempanga refa Celso Alvacao kutoka Msumbiji, kuchezesha mechi nyingine ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika baina ya Simba na Esperance ya Tunisia, kesho Jumapili kuanzia saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Marefa wasaidizi ni Zacarias Baloi na Venestancio Cossa huku mwamuzi wa nne akiwa ni Simoes Guambe, wote wakiwa wanatoka Msumbiji.
Refa Azam, Nairobi United huyu hapa
Kwa upande wa mchezo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Afrika baina ya Azam FC na Nairobi United, Jumapili kuanzia saa 1:00 usiku katika Uwanja wa New Amaan Complex, refa atakuwa ni Gerson Angono kutoka Guinea ya Ikweta.
Atezambong Carine kutoka Cameroon atakuwa msaidizi namba moja na Juan Ngua Eleng atakuwa msaidizi namba mbili hukuWilly Ngah kutoka Cameroon akiwa refa wa akiba.