Usitingishe waya, wikiendi ya wakubwa!

LEO Jumamosi kuna mechi tatu za Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini Watanzania wataitolea zaidi macho ile itakayochezwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex uliopo Unguja.

Mechi hiyo itakayochezwa kuanzia saa 10:00 jioni, Yanga itaikaribisha Al Ahly, timu zilizopo kundi B, huku ikishuhudiwa ile iliyochezwa Misri Ijumaa ya wiki iliyopita wenyeji wakishinda 2-0.

Watu wakiwa wanaangalia hiyo mechi, inabidi utulie, usipitepite mbele ya runinga ukakanyaga waya ukaharibu shughuli. Utapigwa.

Baada ya mechi hiyo, itafuatiwa na ile ya kundi D, Petro Atletico dhidi ya Stade Malien itakayochezwa Angola kuanzia saa 1:00 usiku, kisha saa 4:00 usiku, mechi nyingine ya kundi B, AS FAR Rabat itaikaribisha JS Kabylie ikipigwa Morocco.

Kwa ufupi, wikiendi hii wapenda soka duniani watakuwa bize kufuatilia ligi mbalimbali kuanzia Afrika hadi Ulaya.

Pale England, vijana wa Mikel Arteta, Arsenal baada ya wikiendi iliyopita kupigwa nyumbani 3-2 na Manchester United, leo Jumamosi wataifuata Leeds katika mwendelezo wa Premier League, Brighton itacheza dhidi ya Everton na Wolves ikikipiga dhidi ya Bournemouth, hizi zote zitachezwa saa 12:00 jioni.

CA 01


Kisha saa 2:30 usiku itapigwa London Derby pale Stamford Bridge na Chelsea itaikaribisha West Ham United, kisha saa 5:00 usiku tutafunga pazia kwa kushuhudia Liverpool ikicheza dhidi ya Newcastle United.

La Liga, Serie A, Bundeliga na Ligue 1, huko nako zitapigwa mechi za maana katika muda huu wa duru la pili kuelekea kumalizia msimu wa 2025-2026.

Kipigo cha kwanza ilichopokea Yanga katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ugenini dhidi ya Al Ahly, kimeongeza hasira kwa Wanajangwani hao kuelekea mechi hii ya leo.

Yanga inafahamu, wapinzani wao sio wa kucheza nao kinyonge kwani ni mabingwa wa kihistoria wa Ligi ya Mabingwa Afrika wakichukua taji hilo mara 12, zaidi ya klabu zote.

Pointi saba za Al Ahly katika kundi B ikiongoza, zinawapa jeuri ya kusaka zingine zaidi ili kumaliza kinara na kufuzu robo.

Kwa sasa Al Ahly ikiwa kinara na pointi saba, Yanga inafuatia inazo nne, AS FAR Rabat na JS Kabylie kila moja inazo mbili, zote zikicheza mechi tatu.

Mechi hizi za leo zinaweza kutoa taswira mpya kabisa ya kundi B, kama Yanga itapata ushindi au hata sare, itaiweka sehemu nzuri zaidi kuelekea kufuzu robo fainali.

Mara ya mwisho Yanga kuikaribisha Al Ahly, ilikuwa Desemba 2, 2023 na matokeo yalikuwa sare ya 1-1, huku rekodi za jumla zikionyesha Waarabu hao wamepoteza mbele ya Yanga mara moja walipochapwa 1-0, Machi 1, 2014.

Wakali hao wamekutana katika mechi saba, zote za Ligi ya Mabingwa kwenye hatua mbalimbali. Al Ahly imeshinda nne, sare mbili na Yanga ikishinda moja.

Jambo la kufurahisha ni, licha ya Yanga kupoteza mara nne dhidi ya Al Ahly, lakini haijawahi kufungwa nyumbani, zote ilikuwa ugenini. Nyumbani Yanga ina rekodi ya kushinda mara moja na sare mbili.

Upinzani ilioutoa Yanga ugenini dhidi ya Al Ahly katika mechi iliyopita licha ya kupoteza, unaweza kuibeba leo endapo itarekebisha baadhi ya maeneo ikiwamo kujilinda na kumalizia nafasi.

Al Ahly inapokuwa ugenini hasa mechi kama hizi za makundi, hutumia mbinu za kutoshambulia sana.

Hali hiyo imeifanya mara zote ilipokuja Tanzania imeshinda kupata ushindi mbele ya Yanga.

Kiwango cha Laurindo Depu alichoonyesha katika mechi tatu za mashindano alizocheza tangu atue Yanga zikiwamo mbili za Ligi ya Kuu Bara akifunga mabao matatu na asisti moja, huku nyingine ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Al Ahly, kimeleta matumaini mapya ndani ya kikosi hicho.

CA 02


Kocha wa Yanga, Pedro Goncalves amefichua kwamba, anachokifanya Depu hivi sasa ni kama asilimia 35 ya uwezo wake, endapo akizoeana na wenzake, itakuwa balaa.

Hata hivyo, mechi zote za Yanga dhidi ya Al Ahly, hazijawahi kumalizika bila bao pia hayajawahi kuzidi matatu, hivyo kwa wazee wa kubeti, hapa kuna hela ukiweka lipatikane bao.

Matokeo ya mechi hizo saba kati ya Yanga na Al Ahly yapo hivi; Yanga 1-0 Al Ahly (Machi 3, 2014), Al Ahly 1-0 Yanga (Machi 9, 2013, Al Ahly ikashinda kwa penalti 4-23), Yanga 1-1 Al Ahly (Aprili 9, 216), Al Ahly 2-1 Yanga (Aprili 20, 2016), Yanga 1-1 A Ahly (Desemba 2, 2023), Al Ahly 1-0 Yanga (Machi 1, 2024) na Al Ahly 2-0 Yanga (Januari 23, 2026).

CA 03


Kuelekea mchezo huo kocha wa zamani wa Yanga, Nasreddine Nabi amesemaanaiona timu hiyo ikipata ushindi mbele ya Waarabu hao huku akiwapa mbinu na kutoa tahadhari.

AmesemaYanga inatakiwa kuwa makini kwenye ulinzi na kuwa na kasi ya kutengeneza mashambulizi, kwani mara nyingi Ahly inapofanya vizuri nyumbani haiweki nguvu kubwa ugenini.

“Yanga inatakiwa kujipanga ili kutengeneza ushindi wa haraka, lakini kama itapata sare au ushindi kwenye mchezo huo inaweza kutinga robo fainali,” amesemaNabi.

“Inatakiwa kutambua Ahly haiwezi kufanya makosa mengi, hivyo wachezaji wake wanatakiwa kuwa makini kutumia nafasi, pia watumie wachezaji wenye kasi. Kikosi cha Yanga kina uwezekano mkubwa wa kufanya vyema, kwani kina wachezaji wazuri wenye uwezo mkubwa wa kuwachosha Waarabu.”

CA 04


Kesho Jumapili, ni zamu ya wakali wengine watatu kutoka Tanzania kujitupa uwanjani katika michuano ya CAF, huku Simba ikiwa na mechi ya mtego zaidi iliyobeba uamuzi wa kuendelea kupigania nafasi ya kufuzu robo fainali au kuumaliza mwendo.

Simba inayoburuza mkia wa kundi D la Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa haina pointi, itaikaribisha Esperance kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam kuanzia saa 10:00 jioni.

Esperance yenye pointi tano, inaingia uwanjani ikiwa imetoka kuichapa Simba ilipokuwa nyumbani Tunisia, wikiendi iliyopita. Kundi hilo linaongozwa na Stade Malien yenye pointi saba, huku Petro Atletico ikiwa nazo nne.

Kwa sasa, Simba inapambana kushinda mechi tatu zilizobaki hatua ya makundi ili kufikisha tisa zinazoweza kuwavusha robo fainali.

Si kuwavusha tu, bali kuweka rekodi mpya katika michuano ya CAF kwani haijawahi kutoka timu kupoteza mechi tatua mfululizo za mwanzoni hatua ya makundi, kisha ikafuzu robo fainali. Simba ikiweza itaweka rekodi mpya.

CA 05


Hata hivyo, Simba inataka kuilinda rekodi yake ya kucheza robo fainali ya CAF kila inapokuwa makundi tangu kuanzia 2018. Timu hiyo tayari imecheza robo fainali saba katika kipindi hicho, huku 2024-2025 ikifika hadi fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Kocha wa Simba, Steve Barker, alisema: “Ni kweli tumekutana na changamoto katika mechi zetu tatu za kwanza katika mashindano haya ya Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini huo siyo mwisho wa safari yetu, bado tuna nafasi ya kufanya kitu katika mechi ambazo zimesalia.

“Mechi dhidi ya Esperance ni muhimu sana kwetu, siyo tu kwa sababu ya pointi, bali pia kwa morali ya kikosi chetu.

“Tunahitaji kuonyesha msimamo wetu kama timu. Tukipata matokeo chanya, inaweza kuwa mwanzo wa kurekebisha kilichotokea. Hii ni mechi ambayo tunahitaji sana, sapoti ya mashabiki wetu.”

CA 07


Kesho pia saa 10:00 jioni, Singida Black Stars itakuwa ugenini katika kuzisaka pointi zingine tatu dhidi ya AS Otoho zilipokutana New Amaan Complex, ikiwa ni Kombe la Shirikisho Afrika.

Singida kwa sasa ina pointi nne sawa na Stellenbosch, CR Belouizdad inaongoza kundi C kwa pointi sita, wakati AS Otoho inazo tatu.

CA 08


Ni kundi lililokaa kimtego kwa yeyote anaweza kutoboa, mechi za kesho Jumapili zinaweza kulifumua kundi na kuliweka katika sura tofauti.

Kocha wa Singida Black Stars, David Ouma, amesema: “Tumejiandaa kushindana na kucheza kwa kumuheshimu mpinzani wetu ambaye pia anasaka pointi tatu kama ilivyo upande wetu, mbinu bora na kujitoa kwa wachezaji ndio kutatupa nafasi ya kusonga hatua inayofuata.”

CA 08


Dimba la New Amaan Complex, kesho litachafuka tena kwa mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika, Azam ikiikaribisha Nairobi United, kuanzia saa 1:00 usiku.

Azam iliichapa Nairobi kwao Kenya mabao 2-1, hali iliyoibua matumaini ya kuona inaweza kufuzu robo fainali.

Katika kundi B, Azam ina pointi tatu ikishika nafasi ya tatu wakati Nairobi inaburuza mkia bila pointi. Kinara Wydad yenye tisa, ikifuatiwa na AS Maniena (6).

CA 09


Kocha wa Azam, Florent Ibenge, amesema:

“Ingawa bado kundi letu ni gumu, lakini tutahakikisha tunatengeneza ushindi wa pili ingawa tutakutana na timu ngumu. Mpango wetu wa kwanza ni kuhakikisha tunaten geneza ushindi wa pili kwani ushindi huu wa ugenini umewapa wachezaji imani ya kwamba wanaweza kubadilisha matokeo wakati wowote.”