BAADA ya kupisha mapumziko ya wiki moja, raundi ya pili ya Ligi ya Championship inaendelea tena leo Jumamosi kwa mechi tatu kupigwa na nyingine kesho Jumapili, huku kila timu ikipambana kwa ajili ya kujitengenezea nafasi nzuri.
Maafande wa Transit Camp iliyoshinda mechi ya mwisho kwa kuichapa KenGold bao 1-0, itakuwa kwenye Kituo cha Ufundi cha TFF, Kigamboni, jijini Dar es Salaam kucheza dhidi ya Kagera Sugar, yenye kumbukumbu ya kuchapwa na Mbeya Kwanza mabao 2-1.
Transit inashika nafasi ya nne na pointi 33 na ikiwa itashinda itafikisha 36, ambazo ni sawa na za Kagera ilizonazo msimu huu, huku mzunguko wa kwanza zilipokutana zilitoka suluhu (0-0), kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba Mkoani Kagera.
Kwa msimu wa 2024-2025, Transit ilimaliza nafasi ya 14 katika Ligi ya Championship na pointi 21, baada ya kushinda mechi tano, sare sita na kupoteza 19 kati ya 30 ilizocheza, ikifunga jumla ya mabao 19 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 50.
Baada ya kumaliza nafasi ya 14, Transit ilicheza mechi mbili za ‘Play-Off’ kusaka tiketi ya kubakia Championship na ilianza kwa kuitoa Kiluvya United kwa jumla ya mabao 3-2, kisha kuiondosha pia Rhino Rangers ya Tabora kwa jumla ya 4-1.
Kagera iliyodumu katika Ligi Kuu Bara kwa miaka 20 tangu ilipoanza kushiriki 2005, ilishuka daraja msimu wa 2024-2025, baada ya kushinda mechi tano tu, sare minane na kupoteza 17, ikishika nafasi ya 15, kufuatia kukusanya pointi zake 23.
Timu hiyo inayonolewa na aliyekuwa nyota wa Simba, Yanga na timu ya Taifa Stars, Juma Kaseja aliyewahi kuitumikia pia Kagera akiwa mchezaji na kocha wa makipa, ana kazi ya kukipambania kikosi hicho ili kirejee tena katika Ligi Kuu Bara.
Pia, ikiwa Kagera itashinda katika mechi hiyo inayosubiriwa kwa hamu kutokana na ubora wa makocha na wachezaji wa timu hizo, itasogea hadi nafasi ya kwanza na kuishusha Geita Gold inayoongoza na pointi 37, itakayocheza kesho na Barberian.
B19 FC iliyochapwa mabao 2-0, dhidi ya Mbuni mechi ya mwisho, itakuwa nyumbani kuikaribisha maafande wa Polisi Tanzania, yenye morali kubwa baada ya kuichapa Gunners FC ya jijini Dodoma mabao 4-0, kwenye uwanja wake wa Ushirika mjini Moshi.
Mechi hii ni ya kisasi kwa B19 iliyo nafasi ya 13 na pointi tisa na ina kumbukumbu ya kuchapwa raundi ya kwanza kwa mabao 4-0, huku kwa upande wa Polisi Tanzania inayopambana kurejea tena Ligi Kuu, ikiwa ya sita na pointi 26.
Polisi msimu uliopita wa 2024-2025, haukuwa mzuri sana baada ya kumaliza nafasi ya 10, katika Ligi ya Championship na pointi 33, ikishinda mechi nane, sare tisa na kupoteza 13, ambapo safu ya ushambuliaji ilifunga mabao 44 na kuruhusu 33.
Kikosi hicho kinapambana ili kurejea tena Ligi Kuu Bara baada ya kushuka daraja msimu wa 2022-2023, kilipomaliza nafasi ya 15 na pointi zake 25, kufuatia kushinda mechi sita tu, sare saba na kupoteza 17, kikifunga mabao 25 na kuruhusu 54.
Mechi ya mwisho kwa leo Jumamosi, itapigwa kwenye Uwanja wa Amani uliopo Mkoa wa Njombe na Hausung iliyotoka suluhu (0-0) dhidi ya TMA ya jijini Arusha, itaikaribisha African Sports ya mjini Tanga iliyochapwa mabao 2-1 na Stand United.
Hausung iliyo nafasi ya 14 na pointi nane ambazo ni sawa na za African Sports inayoshika nafasi ya 15, zinakutana zikiwa hazina mwenendo mzuri msimu huu, huku mechi ya mzunguko wa kwanza zilipokutana Sports ilishinda nyumbani Tanga bao 1-0.
Kesho Jumapili zitapigwa pia mechi tatu na Mbeya Kwanza iliyo nafasi ya tatu na pointi 34, baada ya kuichapa Kagera Sugar mabao 2-1, itakuwa kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi Tabora, kuikaribisha Mbuni FC ya Arusha iliyoichapa B19 2-0.
Mbuni iliyo nafasi ya tano na pointi 28, baada ya kushinda mechi tisa, sare moja na kupoteza mitano kati ya 15, inaingia kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, ikiwa na kumbukumbu nzuri, kufuatia raundi ya kwanza kuichapa Mbeya Kwanza mabao 4-0.
Kwenye Uwanja wa Filbert Bayi, Kibaha Mkoani Pwani, wenyeji, Barberian FC inayoburuza mkiani na pointi nane, itakuwa na kibarua cha kulipiza kisasi dhidi ya vinara Geita Gold, baada ya mechi ya raundi ya kwanza kuchapwa ugenini mabao 3-0.
Stand United iliyoifunga African Sports mabao 2-1, mechi ya mwisho, itakuwa kwenye Uwanja wa CCM Kambarage uliopo mjini Shinyanga kucheza na Songea United, yenye kumbukumbu ya kutoka sare ya kufungana bao 1-1, dhidi ya Barberian FC.
Kocha wa Barberian, Kheri Mohamed alisema baada ya mwenendo usioridhisha katika raundi ya kwanza, kwa sasa wamejipanga kuhakikisha wanarekebisha kasoro mbalimbali zilizokuwepo, hususan kwenye maeneo muhimu ya kujilinda na ya ushambuliaji.
“Mechi 15 zilizobakia kwetu ni zaidi ya fainali kwa sababu hatupo sehemu nzuri na ili kujinasua ni lazima tupate matokeo mazuri kuanzia sasa, haitakuwa rahisi kutokana na ushindani uliopo, ila tutapambana kadri ya uwezo wetu,” alisema Kheri.