Uhaba wa mbegu bora unavyokwamisha uzalishaji wa ufuta Tanga

Tanga. Wakulima wa zao la ufuta mkoani Tanga wamelazimika kuendelea kutumia mbegu za asili zenye tija ndogo kutokana na uhaba wa mbegu bora, hali inayosababisha mavuno kuwa madogo licha ya zao hilo kuwa na soko kubwa ndani na nje ya nchi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wakulima kutoka wilaya zinazolima ufuta mweupe mkoani humo wamesema matumizi ya mbegu za asili yamekuwa yakiongeza gharama na nguvu kazi mashambani bila kuendana na kiwango cha mavuno kinachopatikana, hali inayokwamisha juhudi zao za kujiondoa katika umaskini.

Kauli hiyo ilitolewa wakati wa hafla ya makabidhiano ya mbegu bora za ufuta kwa wakulima wa wilaya zinazolima zao hilo mkoani Tanga, mbegu zilizotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA) kwa lengo la kuongeza tija na kuhamasisha matumizi ya teknolojia ya kisasa katika kilimo.

Mkulima wa Kata ya Mkalamo wilayani Pangani, Waziri Mkulima, amesema kwa muda mrefu wakulima wamekuwa wakipanda mbegu za asili ambazo mavuno yake ni madogo ikilinganishwa na nguvu kazi na gharama wanazotumia kuanzia maandalizi ya shamba hadi kuvuna.

“Kwa miaka mingi tumekuwa tukipanda mbegu za zamani na kuvuna gunia moja au mawili kwa ekari. Hii haifanani kabisa na gharama na jitihada tunazoweka. Tumeelezwa kuwa mbegu bora zina uwezo wa kutoa hadi tani moja kwa hekari,” amesema.

Ameongeza kuwa taarifa hiyo imewapa matumaini mapya wakulima wa eneo hilo, wakitarajia kuongeza uzalishaji mara tatu zaidi katika msimu ujao wa kilimo.

“Hali hii imeanza kuwahamasisha wakulima wa kata yetu kutumia mbegu bora za ufuta na hata mazao mengine. Hata hivyo, changamoto kubwa bado ni uhaba wa pembejeo vijijini kutokana na kukosekana kwa maduka ya pembejeo. Tunaomba Serikali na wadau wa kilimo kuboresha upatikanaji wa huduma hizi,” amesema.

Kwa upande wake, Ramadhan Ernest Mlagile, mkazi wa Kijiji cha Boza katika Kata ya Kimang’a, amesema ugawaji wa mbegu bora za kisasa na COPRA utawasaidia wakulima kuondokana na matumizi ya mbegu zisizo na tija na kuwapa fursa ya kufikia malengo ya Serikali ya kuwawezesha kiuchumi.

“Tumekuwa tukijishughulisha na kilimo hiki kwa muda mrefu, lakini kwa kuwa mavuno yalikuwa madogo, hatukuweza kufikia malengo yetu. Sasa kwa kuwa kuna mbegu bora, tunaomba zigawiwe kwa wingi ili kila anayehitaji azipate na ajikwamue kiuchumi kupitia ufuta,” amesema Mlagile.

Naye Adam Hussein, mkulima wa Kijiji cha Stahabu wilayani Pangani, amesema mahitaji ya mbegu hizo ni makubwa kuliko kiasi kilichotolewa.

“Kwa shamba la ekari tano nilihitaji kilo 15 za mbegu, lakini nitapata kilo sita au saba pekee. Hii inaonyesha bado kuna uhaba mkubwa,” amesema.

Akizungumza kuhusu umuhimu wa zao la ufuta, Afisa Kilimo wa Mkoa wa Tanga, George Mbaga, amesema kwa sasa ufuta una soko kubwa ndani na nje ya nchi, huku Wizara ya Kilimo ikiweka mkazo katika matumizi ya mbegu bora kama njia ya kuongeza tija na kipato cha wakulima.

“Mbegu aina ya Lindi 2002 ni ufuta mweupe unaotoa mafuta mengi na una soko zuri. Ni mbegu ya uchavushaji wazi inayomwezesha mkulima kuitumia kwa misimu inayofuata. Kwa awamu hii, wakulima 700 watanufaika, huku zaidi ya wakulima 100,000 wakiendelea kutumia mbegu za asili,” amesema Mbaga.

Kwa upande wa utekelezaji wa mpango huo, Mwakilishi wa COPRA, Paskalia Sitembela, amesema tani 1.35 za mbegu bora za ufuta zimekabidhiwa kwa halmashauri za Pangani, Handeni Mji na Handeni Vijijini kupitia mfumo wa ruzuku wa TFRA kwa wakulima waliouza mazao yao kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani.

“Lengo la COPRA ni kuongeza tija katika kilimo na kutatua changamoto ya matumizi ya mbegu za asili. Tunahamasisha wakulima kutumia mfumo wa stakabadhi ghalani ili wapate faida zaidi kulingana na kiwango cha mazao watakayovuna,” amesema Sitembela.

Akitoa maelekezo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Ayub Sebabili, amesema COPRA inapaswa kuhakikisha mbegu zinazotolewa zinasimamiwa ipasavyo ili kuleta tija inayotarajiwa.

Amesema hatua hiyo ni muhimu katika kuleta mageuzi ya kilimo cha kisasa yanayoendana na dira ya maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025 hadi 2050, huku akiwapongeza wakulima wa mkoa huo kwa kukubali mabadiliko na kuachana na dhana ya kutegemea mbegu za asili pekee.

“Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa kilimo ili kuhakikisha kila mkulima anayehitaji mbegu bora anazipata kwa wakati na kuongeza uzalishaji,” amesema.

Wadau wa kilimo wamesisitiza kuwa ugawaji wa mbegu bora ni hatua muhimu, lakini wamebainisha kuwa mafanikio ya mapinduzi ya kilimo cha ufuta yatategemea upatikanaji wa mbegu kwa wakati, usimamizi thabiti wa matumizi yake na kuimarishwa kwa huduma za pembejeo vijijini, ili wakulima waweze kuzalisha kwa tija na kunufaika kikamilifu na soko lililopo.