Dar es Salaam. Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, imetangaza kuanza kwa utolewaje wa mikopo ya masharti nafuu kwa wafanyabiashara wadogo nchini.
Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa jana Januari 30, 2026 na Waziri wa wizara hiyo, Doroth Gwajima jijini Dodoma, Serikali inawakaribisha wafanyabiashara wadogo kuchangamkia fursa ya mikopo hiyo inayotolewa kupitia Benki ya Taifa ya Biashara (NMB).
“Ninapenda kutumia fursa hii kuwaalika na kuwahamasisha wafanyabiashara ndogondogo wote kuchangamkia fursa ya mikopo ya Serikali yenye masharti nafuu na riba ya asilimia saba kwa mwaka inayotolewa kupitia NMB ambayo imeingia makubaliano na Serikali kusimamia mikopo hiyo,” amesema Gwajima kwenye taarifa yake.
Mikopo hiyo inalenga kuwawezesha wafanyabiashara ndogondogo wenye mauzo ghafi yasiyozidi Sh4 milioni kwa mwaka, wakiwamo mama na baba lishe, machinga, waendesha bodaboda pamoja na makundi mengine yanayotambuliwa na kusajiliwa na mamlaka husika maeneo mbalimbali nchini.
Kuhusu utaratibu kwa mfanyabiashara ndogondogo ili aweze kunufaika na mikopo hiyo, anatakiwa awe ametambuliwa na kusajiliwa kwenye Mfumo wa Utambuzi na Usajili wa Wafanyabiashara Ndogondogo (WBN-MIS) na Ofisa Maendeleo ya Jamii kutoka katika halmashauri yake.
Pia, awe raia wa Tanzania mwenye umri wa kuanzia miaka 18, mwenye biashara inayotambuliwa katika eneo lake au eneo linalotambuliwa na mamlaka husika; pamoja na kuwa na Kitambulisho cha Taifa( Nida).
Aidha, utaratibu wa kuomba mikopo hiyo unamtaka mwombaji mwenye kitambulisho cha kidijitali au namba ya kitambulisho hicho kufika NMB kwa ajili ya kujaza fomu ya maombi na kuwasilisha nyaraka zinazohitajika.
Kisha, maombi yote yanahakikiwa na kuchambuliwa kwa mujibu wa taratibu za benki hiyo na waombaji wanaokidhi vigezo wanaingiziwa fedha kwenye akaunti zao kulingana na aina ya mkopo waliyoomba.
“Mikopo hii ina masharti nafuu ikilinganishwa na mikopo ya kibiashara, ambapo muda wa mkopo ni kuanzia miezi mitatu hadi miezi 24, kulingana na aina ya biashara, riba ni asilimia 7 tu kwa mwaka na mkopo umewekewa bima dhidi ya kifo na ulemavu wa kudumu kwa mkopaji, kwa lengo la kumlinda mfanyabiashara na familia yake,” amesema Waziri Gwajima.
Aidha, ili wenye uhitaji wa mikopo hii waweze kunufaika nayo, waziri huyo ametoa wito kwa wale ambao bado hawajatambuliwa na kusajiliwa kwenye mfumo wa WBN-MIS wafike katika ofisi za kata au halmashauri za wilaya walipo ili kukamilisha zoezi la utambuzi na usajili.
“Serikali itaendelea kushirikiana Benki ya NMB kuhakikisha mikopo hii inawafikia walengwa kwa uwazi, haki na kwa wakati, huku tukisisitiza nidhamu ya marejesho ya fedha ya mikopo ili fursa hiyo iwanufaishe wananchi wengi zaidi,” amesisitiza.
Akizungumzia mfumo wa utolewaji wa mikopo hiyo na masharti yaliyowekwa, mchambuzi wa masuala ya uchumi na fedha, Dk Tobias Swai amesema mikopo ya namna hiyo ilikuwapo tangu mwanzoni, wafanyabiashara wamekuwa wakipata na bahati mbaya wengi wamekuwa hawarudishi kikamilifu.
“Kikubwa kipya hapo ni mikopo hiyo kupitishwa benki, hasa NMB ambayo ina mtandao mpana nchini. Mategemeo yetu ni kwamba mfumo huu mpya utawawezesha wahitaji kupata mikopo hii na kurejesha kikamilifu, tofauti na awali ambapo wengi walikuwa hawarejeshi,” amesema.
Jesse Kwayu, mchambuzi wa masuala ya siasa na utawala anatahadharisha juu ya usimamizi na uendeshaji wa mikopo hiyo akiibua suala la urasimu na ubadhirifu ambalo limekuwa likipigiwa kelele na walengwa wa mikopo kutonufaika nayo inapotolewa na Serikali.
“Kuna mambo kadhaa ya msingi katika kuwezesha mikopo hii kuwafikia walengwa, mosi, ni kuhusu utambuzi kwa wenye vitambulisho au namba za Nida ukoje na urahisi wa kupata utambuzi huo uko je?,” amehoji akisema tatizo la mikopo huanzia kwenye mifumo yake ya utambuzi wa walengwa.
Pili, amesema mara nyingi benki zimekuwa na masharti mengi akihofia mifumo kuwa kikwazo kwa baadhi ya walengwa ikiwa haitawekewa urahisi kuwezesha waombaji kujaza na kutimiza masharti vyema ili kuepuka kuenguliwa kwenye mfumo kwa makosa madogo ya kimfumo.
“Natamani ningeona fomu ya mkopo huo kwani hapo mara nyingi ndipo huwa na vitu vingi. Kwa kawaida benki haina kupindisha mambo, ni utaratibu na masharti, kwa mfano mhusika kutakiwa awe na akaunti benki inayopitisha fedha za biashara yake huko wengine inaweza kuwa mtihani hapa.”
Pia, amesisitiza kuwa mfumo wa utambuzi wa wafanyabiashara hao kupitia Serikali za kata na halmashauri unapaswa kuwekewa namna rahisi zaidi ili kuepuka mizunguko mirefu inayoweza kuwakwamisha baadhi ya wanaohitaji mikopo hiyo akihoji, “ni rahisi kiasi gani kujisajili kwenye mfumo wa Serikali uliotajwa hapo wa WBN- MIS ili kuepuka usumbufu na kikwazo kwa walengwa?,”
Kwayu amesema malalamiko mengi kuhusu mikopo ya Serikali yamekuwa yakiibuka kwenye usimamizi wa utekelezaji wa mikopo hiyo baada ya Serikali kukamilisha michakato yake akitaka uadilifu katika kuhakikisha inawafikiwa walengwa halali.
“Kumekuwepo mikopo mingi ya aina hii bila mafanikio, mfano ilikuwepo mamilioni ya Kikwete, Zipo asilimia 10 za halmashauri, zote hizi hazikuonesha tija kutokana na changamoto za kiuajibikaji, bila hivyo hata hizi sijui benki, itawezaje kuingiza suala la uwajibikaji katika mikopo hii,” amesema.