Waarabu wa Simba waifuata Yanga

SIMBA inacheza nyumbani kesho Jumapili dhidi ya Esperance de Tunis, lakini Waarabu wao hao wametua Zanzibar wakifuata mambo mawili wakiwamo Yanga.

Mashabiki wa Esperance wametua Dar es Salaam, kisha wakachukua ndege na kuja Zanzibar kwa lengo la kutalii kidogo, halafu baadaye wakasema wataifuata Yanga.

Mashabiki hao wanajua kwamba mashabiki wa Yanga hawatapenda Simba ishinde na wataishangilia leo dhidi ya Al Ahly, kisha kesho wanajua watawasaidia mbele ya Simba.

Mashabiki hao wa kundi la Utras wamesema kama wakipata nguvu ya mashabiki wa Yanga timu yao itashinda kirahisi.

“Tunataka kuijua Zanzibar kidogo lakini wametuambia Yanga inacheza leo, tutakuja kuwashangilia ili nao watusaidie Jumapili,” amesema shabiki wa Esperance Mohsen Abdelkadir.

“Tuna timu nzuri sana lakini Simba ina mashabiki wengi, Yanga hawaipendi Simba watatusaidia kama wakishinda leo kwa kuwa hawatataka kuona Simba wanafurahi.”

Kesho Jumapili Februari 1, 2026, Simba itakuwa na mchezo wa nne katika Ligi ya Mabingwa Afrika kundi D itakaporudiana na Esperance baada ya kupoteza ugenini kwa bao 1-0.

Simba haijashinda mchezo wowote kwenye makundi ambapo inataka kubadilisha matokeo hayo kuanzia mchezo huo utakaopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.