Na Farida Mangube, Morogoro
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Joseph Masunga amewataka wanachama wa chama hicho kuendelea kudumisha amani na upendo wakati wa maadhimisho ya miaka 49 ya kuzaliwa kwa CCM.
Akizungumza katika uzinduzi wa maadhimisho hayo ngazi ya mkoa, Masunga amesema waasisi wa taifa walifanya kazi kubwa ya kujenga na kuilinda amani ya nchi, hivyo ni wajibu wa kizazi cha sasa kuendeleza tunu hiyo muhimu ambayo taifa limeachiwa kama urithi wa kudumu.
Kwa upande wake, Katibu wa CCM Mkoa wa Morogoro Nuru Ngereja amesema katika kipindi cha miaka 49 ya CCM, chama kupitia Serikali yake kimefanikiwa kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ya maji, barabara, elimu, afya pamoja na umeme.
Amesema CCM ni chama kinachoshughulikia matatizo ya wananchi hali iliyowafanya Watanzania kuendelea kukiamini na kukichagua katika Uchaguzi wa Oktoba 29.
“Kwa sasa tumebakiza vijiji vichache tu kuvifikishia umeme. Tuliwaahidi Watanzania maendeleo na tunaendelea kuyatekeleza,” amesema Ngereja.
Ameongeza kuwa maadhimisho hayo ni fursa ya kusherehekea kazi kubwa iliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
“Tunaposherehekea miaka 49 ya CCM, tunasherehekea mafanikio yetu kama Watanzania,” ameongeza.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Maulidi Dotto amesema Serikali itaendelea kutekeleza maelekezo yanayotolewa na Mwenyekiti wa CCM Taifa, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa lengo la kuhakikisha maendeleo yanafika kwa wananchi wote.



