Uwanja wa Afcon 2027 wafikia asilimia 30 Zanzibar

Wakati maandalizi ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2027 yakiendelea, ujenzi wa uwanja utakaotumika visiwani hapa umefikia asimilia 30.

Uwanja huo unaojengwa Fumba, Mkoa wa Mjini Magharibi na kampuni ya Orkun kutoka Uturuki, ujenzi wake ulianza Mei 2025 na unatarajiwa kukamilika Desemba 2026 kwa awamu ya kwanza ukigharimu Dola za Marekani 150 milioni sawa na Sh389.141 bilioni.

Akizungumza baada ya kufanya ziara maalumu ya kukagua na kutembelea uwanja huo leo Januari 31, 2026, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, amesema serikali inaridhishwa na hatua zilizofikiwa za mradi huo.

“Tumeona hali halisi ya maendeleo ya ujenzi, kazi inaendelea vizuri, na kwa hakika uwanja huu wapo pazuri katika hatua zake za ujenzi na wapo ndani ya muda,” amesema Hemed.

“Nataka niwahakikishie wananchi kwamba kazi hii itaendelea vizuri kwasababu vifaa vyote vinavyohitajika vipo tayari kwenye eneo la ujenzi, kwahiyo hakuna sababu ya kazi hii kuchelewa.”

Amesema azma ya serikali ipo palepale kutumia uwanja huo kwa michezo ya Afcon mwaka 2027.

Amebainisha kwamba viongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) walitembelea uwanja huo jana na wameridhika na kiwango ambacho kimefikiwa cha ujenzi.

Uwanja huo wenye uwezo wa kuchukua watu 36,500, utakuwa na eneo la kuegesha magari zaidi ya 2,000 kwa wakati mmoja.

Awamu ya kwanza ya ujenzi huo, inahusisha uwanja na barabara za ndani na maegesho huku awamu ya pili itahusisha ujenzi wa hoteli ya nyota tano, hospitali ya michezo na viwanja vya michezo mbalimbali.

Amesema baada ya uwanja kukamilika, wataona ni fursa zipi za kibiashara zinazopatikana katika maeneo haya.

“Niwaombe wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla wanaotaka kuja kuwekeza huku, tujiandae basi kutakuwa kuna mji wa biashara kabisa, kwahiyo kutakuwa na soko la vitu vingi, hii ni fursa kwa wawekezaji kuja kuwekeza,” amesema.

Naye Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Riziki Pembe Juma, amesema wizara inaendelea kusimamia hatua hizo ili lengo lililokusudiwa lifikiwe.

“Huu mradi baada ya kukamilika, Zanzibar itakuwa na ugeni mkubwa ambao utatoa fursa kwa watu wengi na kupata neema kubwa,” amesema.

Kwa mujibu wa Dk Riziki, muda utakapofika wataandaa utaratibu mzuri wa wajasiriamali kwenda kuonesha na kuuza bidhaa zao katika eneo hilo ili waweze kunufaika na ujio wa mashindano hayo katika eneo la nyumbani.

“Hii ni fursa ya wote, wakae mkao wa kula, kikubwa tuendelee kuimarisha biashara zetu ili wakati ukifika tupate kunufaika,” amesema.

“Mbali na wajasiriamali wadogo, lakini ujio wa mashindano hayo watafaidika watu wa hoteli, wenye magari ya usafiri, kwahiyo zitakuwa fursa kubwa kwa wananchi wetu.”

Amesema licha ya kuwapo na kamati kuu ya kitaifa, inayoratibu masuala ya Afcon, lakini Zanzibar yenyewe inaendelea kufuatilia kwa ukaribu kazi na mipango yote ya Afcon.

Kwa upande wake Abdulhamid Mhoma, mmiliki wa kampuni ya Al-Hatmy Design and Engineering Consultancy inayosimamia mradi huo, amesema wanaendelea vizuri na wanaamini watamaliza kwa wakati.

“Kwa mujibu wa programu yetu, tumeshafikia asilimia 30 kati ya 100 na hivi mnavyoona tumeshaweka levo ya kwanza ya zege baadaye itakuja ya pili na ya tatu kisha ndio itakuja roof ‘paa’ ambayo kwasasa inatengenezwa Uturuki, italetwa hapa kwa meli,” amesema.

Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, wamekusudia baada ya miezi mitatu wamalize kazi zote za kumwaga zege.

“Kwahiyo Desemba kiwanja kitakuwa kimeshamalizika na itakuwa imebaki kazi kidogo za decoration (mapambo) tu,” amehitimisha.

Afcon ni michuano inayohusisha timu za taifa za soka za nchi wanachama wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF). Michuano hiyo ilianzishwa mwaka 1957 na toleo lijalo la 2027, imepangwa kuchezwa kuchezwa katika mataifa ya Tanzania, Uganda na Kenya.

Kufanyika kwa Afcon ndani ya Afrika Mashariki, kunakuja baada ya kuchezwa CHAN 2024 katika nchi hizo ambapo ufunguzi ulifanyika Tanzania, wakati fainali ikipiga Kenya, huku kusaka nafasi ya tatu mechi ikichezwa Uganda.