Sh6.9 bilioni zatumiwa kukabiliana na magonjwa yasiyopewa kipaumbele

Dodoma. Ili kukabiliana na magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele, Serikali imetumia kiasi cha fedha Sh6.9 bilioni kwa mwaka wa fedha 2024 hadi 2026 katika Halmashauri 184 na kufanikiwa kutokomeza magonjwa hayo isipokuwa katika Halmashauri saba nchini ambazo bado zina maambukizi ya juu.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), yapo magonjwa 21 yasiyopewa kipaumbele duniani ambayo yanasababishwa na minyoo, bakteria, virusi na fangasi. Kwa upande wa Tanzania, inasumbuliwa zaidi na magonjwa matano ambayo ni ugonjwa wa matende na mabusha, trakoma, usubi, kichocho na minyoo ya tumbo.

Akizungumza na waandishi wa habari Januari 30, 2026 kwenye kilele cha maadhimisho ya magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele duniani jijini Dodoma, Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, amesema jitihada mbalimbali zimefanywa na Serikali pamoja na wadau kukabiliana na magonjwa hayo.

Amesema Serikali, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, wamekuwa wakitoa kingatiba katika maeneo yenye changamoto kubwa ya magonjwa hayo na kwa wengine kufanyiwa upasuaji ili kurejea katika hali ya kawaida.

Amesema Serikali inafahamu ukubwa wa tatizo hili na changamoto wanazopitia wananchi wanapokuwa wamepata magonjwa haya, hivyo imewekeza katika utoaji wa huduma na utekelezaji wa afua zote zinazolenga kuboresha afya ya jamii katika kupambana na magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele.

Ametaja afua hizo kuwa ni pamoja na ugawaji wa kingatiba katika jamii na kwa watoto wenye umri wa kwenda shule kuanzia miaka mitano hadi 14, kutoa huduma za utengamao kwa wagonjwa wenye mabusha, matende na vikope, kufanya tathmini za magonjwa haya ili kuangalia kiwango cha maambukizi, pamoja na ununuzi, ugomboaji, utunzaji na usambazaji wa shehena za dawa, vifaa tiba na vitendanishi nchini.

“Napenda kutoa wito kwa wananchi katika mikoa yote ambayo mazoezi haya ya umezaji dawa (kingatiba) yatafanyika kujitokeza na kushiriki kikamilifu. Mazoezi haya ni muhimu kwani kwa mwananchi kumeza dawa hizi ni kujitibu na kujikinga, pamoja na kupunguza maambukizi kwa wengine,” amesema Mchengerwa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Shirika lisilo la kiserikali la Sightsavers International, Godwin Kabalika, amesema shirika hilo limewekeza kiasi cha Sh1.6 bilioni kwa ajili ya kutokomeza magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele nchini.

Aidha, amesema shirika hilo linafanya kazi kwa karibu na wizara nyingine ili kuhakikisha juhudi za kumaliza magonjwa hayo zinafanikiwa, ikiwemo Wizara ya Maji, Kilimo na Mazingira.

Ofisa Miradi Mwandamizi kutoka shirika lisilo la kiserikali la Evidence Action, Christina Mbise, amesema shirika hilo limejikita katika kutokomeza magonjwa ya kichocho na minyoo ya tumbo kupitia umezeshaji wa dawa nchi nzima.