WASANII mbalimbali hapa nchini ambao ni mashabiki wa Yanga SC, wameonyesha imani kubwa kwa timu hiyo ambayo jioni ya leo Januari 31, 2026 itacheza dhidi ya Al Ahly kutoka Misri ikiwa ni mechi ya kundi B katika Ligi ya Mabingwa Afrika.
Mechi hiyo itakayoanza saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa New Amaan Complex uliopo Unguja, Yanga inahitaji kupata matokeo mazuri ili kuongeza nafasi ya kufuzu robo fainali kufuatia kukusanya pointi nne, huku Al Ahly ikiwa nazo saba.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wasanii hao wamesisitiza umuhimu wa nidhamu, mshikamano na kutumia vyema nafasi zitakazopatikana dhidi ya mabingwa hao wa kihistoria Afrika.
Msaga Sumu ambaye ni msanii wa Singeli, amesema: “Mchezo huo ni wa kihistoria kwa Yanga na soka la Tanzania kwa ujumla, kikosi cha Yanga kimekomaa na kina uwezo wa kushindana na timu kubwa kama Al Ahly. Wachezaji wanapaswa kucheza kwa kujiamini na kutokubali kushinikizwa na ukubwa wa mpinzani wao.”
Kwa upande wake, Harmonize amesema: “Mechi hiyo inahitaji maandalizi ya hali ya juu na umakini mkubwa ndani ya uwanja. Yanga ina wachezaji wenye uwezo na benchi la ufundi lenye uzoefu, jambo linaloweza kuisaidia timu kupata matokeo mazuri endapo watacheza kwa nidhamu kwa dakika zote 90.”
Msanii wa muziki wa Dansi, Kalala Junior amesisitiza mchango wa mashabiki katika mchezo huo, akisema: “Uzoefu wa Al Ahly haupaswi kuwatisha wachezaji wa Yanga, bali uwe funzo la kucheza kwa umakini zaidi, kila mchezaji atatimiza majukumu yake ipasavyo, Yanga ina nafasi ya kupata matokeo chanya.”
Chege Chigunda naye amesema: “Hii mechi ni kipimo cha ukubwa wa Yanga kimataifa. Al Ahly wana uzoefu mkubwa, lakini Yanga ina kasi, mbinu na ari ya ushindi. Leo ni siku ya kuandika historia mpya na kuonyesha kwamba soka la Tanzania linaweza kusimama kifua mbele barani Afrika.”
Christian Bella amesema: “Mchezo wa leo unahitaji nidhamu kubwa na kuheshimu mpira. Al Ahly ni timu yenye historia, lakini Yanga ina ubora na uwezo wa kushindana nao. Kila mchezaji akitimiza majukumu yake na kupambana kwa moyo wote, Yanga inaweza kupata matokeo chanya na kuwafurahisha Watanzania.”
Naye Juma Nature amesema: “Leo ni siku ya mashabiki kuamini zaidi kuliko hofu. Yanga imejengwa vizuri, ina mchanganyiko wa vijana na wazoefu, na hilo linaweza kuleta tofauti. Mechi kama hizi zinahitaji uamuzi sahihi ndani ya uwanja na kutumia makosa ya mpinzani.”
Chaz Baba, msanii wa muziki wa dansi, amesema: “Soka ni mchezo wa dakika 90 na lolote linaweza kutokea. Al Ahly wana uzoefu, lakini Yanga ina kiu ya mafanikio na mashabiki wenye hamasa kubwa, leo ni siku ya wachezaji kupambana kuanzia mwanzo hadi mwisho bila kukata tamaa.”
Billnass ni msanii wa Bongofleva, amesema: “Leo tukidhibiti presha ya Al Ahly mapema, mchezo unaweza kwenda upande wetu, na Yanga ikicheza bila presha na kwa kujiamini, inaweza kushangaza wengi, hii ni mechi ya kupima ukubwa wa Yanga kimataifa, naona fahari kubwa kuona timu yetu ikicheza na vigogo wa Afrika.”
Mzee Yusuf ambaye ni msanii wa taarabu, amesema: “Ninaamini sana nguvu ya maandalizi na morali ya kikosi. Yanga imejiandaa vizuri na wachezaji wana kiu ya kuonyesha uwezo wao. Mechi ya leo ni nafasi ya kuandika historia mpya na kuipa Tanzania heshima barani Afrika.”
Msanii wa Bongo Movie, Ray Kigosi amehitimisha kwa kusema: “Kwa upande wangu, mechi hii inahitaji moyo wa ushindi zaidi kuliko majina makubwa. Yanga ikijituma na kuamini mpango wa kocha, inaweza kupata matokeo yatakayowapa furaha mashabiki wote wa kijani na njano.”