Rorya. Benki ya NMB inatarajia kutumia zaidi ya Sh7.4 bilioni kwa ajili ya kusaidia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kijamii nchini, hususan katika sekta za elimu, afya na mazingira, kwa mwaka 2026. Hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa benki hiyo wa kurudisha shukrani kwa jamii inayoiwezesha kufanya shughuli zake.
Kiasi hicho cha fedha kimetengwa kufuatia benki hiyo kupata faida ya zaidi ya Sh746 bilioni kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Taarifa hiyo imetolewa leo Jumamosi, Januari 31, 2026 wilayani Rorya na Mkurugenzi wa Fedha wa Benki ya NMB, Juma Kimori katika hafla ya kukabidhi vifaa vya kuimarisha sekta za afya na elimu katika Mkoa wa Mara, msaada uliogharimu zaidi ya Sh430 milioni.
Kimori amesema benki hiyo inatambua juhudi za Serikali katika kuboresha huduma za jamii, hususan katika sekta za afya, elimu na mazingira, hivyo imeamua kuunga mkono jitihada hizo ili kuhakikisha huduma zinazotolewa kupitia sekta hizo zinakuwa bora zaidi.
“Tuna akaunti zaidi ya milioni tisa zinazomilikiwa na wanajamii hawa hawa, hivyo tumeona ni wajibu wetu kutoa shukrani kwao kwa kutuchagua. Tutaendelea kushirikiana na Serikali katika kuboresha huduma za kijamii ili kujenga jamii bora zaidi,” amesema Kimori.
Ameongeza kuwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, benki hiyo imetumia zaidi ya Sh23 bilioni katika kuboresha huduma za kijamii kwenye sekta hizo.
Aidha, benki hiyo imewezesha upandaji wa miti zaidi ya milioni moja katika mwaka wa fedha 2024/2025, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kulinda mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Akizungumzia vifaa vilivyokabidhiwa, Kimori amesema ni pamoja na mashine nane za kutoa joto kwa watoto wanaozaliwa kabla ya muda, magodoro, vitanda, mashuka, madawati pamoja na vifaa vya kuezekea madarasa. Msaada huo umetolewa kwa wilaya sita za Mkoa wa Mara.
Akizungumza baada ya kupokea msaada huo, Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Dk Halfan Haule mbali ya kuishukuru Benki ya NMB kwa mchango huo, ametoa wito kwa wazazi na walezi wilayani humo kuhakikisha watoto wao wanaripoti shule mapema.
Amesema bado wapo wanafunzi wa awali, darasa la kwanza na kidato cha kwanza ambao hawajaripoti shuleni mpaka sasa.
Dk Haule amesema msako wa kuwatafuta wazazi wa wanafunzi ambao hawajaripoti shuleni utaanza Februari 2, 2026, ingawa hakutaja idadi kamili ya wanafunzi husika.
Amesema Serikali wilayani Bunda tayari imetoa maelekezo kwa walimu kuwapokea wanafunzi wote, hata wale wasiokuwa na mahitaji ya msingi ikiwamo sare za shule, madaftari na kalamu, huku ofisi yake ikiendelea na mchakato wa kuwawezesha wanafunzi wanaotoka katika kaya maskini kuanza masomo bila vikwazo.
“Jukumu la mtoto ni kusoma, wakati jukumu la mzazi ni kuhakikisha mahitaji ya msingi yanapatikana. Hata hivyo, ofisi yangu tayari imepata mabegi na madaftari kwa ajili ya watoto wanaotoka katika kaya maskini ili kuwawezesha kuanza masomo wakati wazazi wakiendelea kutafuta mahitaji mengine,” amesema.
Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali Teule ya Shirati KMT, Dk Bwire Chirangi amesema hospitali hiyo bado inakabiliwa na upungufu wa mashine za kutoa joto kwa watoto njiti.
Amesema hospitali hiyo hupokea wastani wa kinamama 300 wanaojifungua kila mwezi, kati yao, takribani watoto 30 huzaliwa njiti na kuhitaji huduma za ziada, ikiwemo matumizi ya mashine za joto.
Dk Chirangi amesema baada ya kupokea msaada huo, hospitali hiyo itakuwa na jumla ya mashine 10 za kutoa joto, idadi ambayo bado ni ndogo ikilinganishwa na mahitaji halisi.
Amesema upungufu wa vifaa hivyo unaendelea kuwa changamoto kwa watoa huduma za afya katika juhudi zao za kuokoa maisha ya watoto wanaozaliwa kabla ya wakati.