Arusha. Mtoto Lightness Mkindi (11), mkazi wa Mtaa wa Ilboru jijini Arusha amedaiwa kujinyonga ndani ya bafu la nyumba yao kwa kutumia kitenge huku akiacha ujumbe wa maandishi.
Tukio hilo lililotokea jana Ijumaa Januari 30, 2026 jijini Arusha, taarifa za awali zinaeleza kuwa, Mkindi alijinyonga kwa kutumia kitenge chake na kufariki dunia.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo amesema leo Januari 31, 2026 kuwa, mwili wa mtoto huyo umehifadhiwa Hospitali ya Rufaa ya Mount Meru ukisubiri taratibu za maziko.
“Tayari tumefungua jalada la uchunguzi kuhusu tukio hilo na endapo itabainika kuna mtu yeyote aliyehusika, sheria itachukua mkondo wake,” amesema Kamanda Masejo.
Mama mzazi wa mtoto huyo, Lidya Mushi amesema, “ni vigumu kupokea taarifa za kifo cha mwanangu mimi kama mzazi, lakini siwezi kumrudisha duniani. Napaswa kuamini kuwa Mungu alinipa na ameona wakati wa kumchukua, jina lake lihimidiwe, sina linguine.”
Akisimulia, amesema siku hiyo aliondoka nyumbani saa tano asubuhi kwenda msibani kwa jirani yake, aliwaacha watoto wake wawili na mama yao mdogo nyumbani.
Amesema baada ya takribani saa mbili kupita, aliitwa na kijana wa jirani ambaye ni dereva wa teksi, akimwambia anatakiwa arudi nyumbani haraka.
“Nilimshangaa na kumuuliza kuna nini, lakini aliniambia hakuna haja ya kunieleza mpaka tufike nyumbani kwanza,” amesema.
Mama huyo amesema alipofika nyumbani alikuta watu wengi na akaelezwa kilichotokea, pamoja na kuambiwa kuwa mwanaye alikuwa amepelekwa Hospitali ya Mount Meru na amelazwa chumba cha wagonjwa mahututi (ICU).
“Nilipofika mapokezi nikaambiwa mtoto amefikishwa pale akiwa hajitambui, baada ya vipimo tukaambiwa alikuwa amefariki dunia tayari,” amesema.
“Nilikimbilia mwili wa mtoto wangu nikamsalia kama mama. Haikuwa rahisi kuamini, lakini nimemuombea mwanangu, sijui kilichotokea.”
Mama huyo amesema, katika chumba cha mtoto huyo kulikutwa kipande cha karatasi chenye ujumbe uliosomeka: “Ebaba Mungu ninaomba kwa niaba ya familia yangu na jamii nzima kwa pamoja na majirani, Mungu naomba umpe bibi yangu hela pamoja na mama yangu pamoja na baba yangu.
“Bibi yangu apate hela ya marejesho, Baba na mama yangu pia wapate hela ya ada ya shule, Mungu utusaidie milele amina. Amefanya maajabu jina lake lihimidiwe.”
Balozi wa Nyumba Kumi wa Tawi la Namayana, Julius Laizer amesema jana saa saba mchana alisikia kelele kutoka nyumba ya jirani na alipotoka alikuta watu wakivunja mlango wa bafu wakidai kuna mtoto amejinyonga.
Amesema inadaiwa mtoto huyo mara nyingi alikuwa akioga na mdogo wake, lakini siku hiyo alienda kuoga peke yake. “Baada ya muda, mdogo wake alipoenda kugonga mlango ili naye aingie kuoga, hakupata majibu hali iliyomfanya mama yao mdogo kuanza kumuita Lightness bila majibu,” amesema.
Laizer amesema baada ya kushuhudia kimya kisicho cha kawaida, waliamua kuchungulia kupitia katika dirisha la bafu ndipo walipomwona ananing’inia.
Amesema walitoa taarifa kwa majirani waliofika na kuvunja mlango wa bafu.
“Walimkuta bado anaonesha dalili za uhai wakamkimbiza hospitali, lakini alifia eneo la mapokezi,” amedai Laizer.
Akizungumzia kifo hicho, bibi wa marehemu Saria Swai amesema ameishi na mjukuu wake tangu akiwa mdogo na hajawahi kuwa na tabia mbaya.
“Mjukuu wangu alikuwa mcha Mungu, lakini nashangaa nini kimemkuta, tuliwaacha tukaenda msibani kwa jirani na akataka kuoga tukamkataza kuoga kwa maji ya baridi, tulimwambia asubiri apashiwe maji moto lakini baada ya kuondoka ndio akachukua maji na kwenda bafuni,” amesema bibi huyo.
Amesema hawajui hadi sasa kama kuna mkono wa mtu, katika tukio hilo lakini wanamwachia Mungu.