Waarabu wa Simba waomba sapoti Yanga

SIMBA inacheza nyumbani leo Jumapili dhidi ya Esperance de Tunis, lakini Waarabu wao hao wametua Zanzibar wakifuata mambo mawili ikiwamo Yanga.

Mashabiki wa Esperance wametua Dar, kisha wakachukua ndege na kuja Zanzibar kwa lengo la kutalii kidogo kisha baadaye wakasema wangifuata Yanga uwanjani jana.

Mashabiki hao wanajua kwamba mashabiki wa Yanga hawatapenda Simba ishinde na walipanga jana kuishangilia dhidi ya Al Ahly, kisha leo Jumapili wanajua watawasaidia mbele ya Simba.

Mashabiki hao wa kundi la Utras, wamesema kama wakipata nguvu ya mashabiki wa Yanga, timu yao itashinda kirahisi.

“Tunataka kuijua Zanzibar kidogo lakini wametuambia Yanga inacheza leo (jana), tutakuja kuwashangilia ili nao watusaidie Jumapili,” alisema shabiki wa Esperance, Mohsen Abdelkadir.

“Tuna timu nzuri sana lakini Simba ina mashabiki wengi, Yanga hawaipendi Simba, hivyo watatusaidia kwa kuwa hawatataka kuona Simba wanafurahi.”

Simba itakuwa na mechi ya nne katika Ligi ya Mabingwa itakaporudiana na Esperance baada ya kupoteza ugenini kwa bao 1-0.

Simba haijashinda mechi yoyote kwenye makundi ambapo inataka kubadilisha matokeo hayo kuanzia mechi hii itakayopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.