Dar es Salaam. Wakati maeneo mbalimbali nchini yakiendelea kushuhudia mvua zinazonyesha chini ya kiwango na mengine kuwa makame, Serikali imesema akiba ya chakula iliyopo inatosha kuhudumia wananchi kwa miezi 18 itakapohitajika.
Akiba ya chakula iliyopo sasa ya tani 550,000 ni zaidi ya kiwango kinachohitajika cha tani 150,000 kwa ajili ya kuhudumia wananchi wake kwa miezi sita.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo alipofanya ziara katika maghala ya Wakala wa Hifadhi ya Chakula ya Taifa (NFRA) yaliyopo katika maeneo ya Kipawa jijini Dar es Salaam leo Jumamosi Januari 31, 2026.
Akizungumza baada ya ziara hiyo, Chongolo amesema baada ya kauli ya Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba kubainisha kuwapo kwa mvua chache kwa mujibu wa utabiri wa hali ya hewa nchini, iliilazimu wizara yake kukaa mguu sawa.
Amesema wamekaa mguu sawa ili chochote kitakachotokea, wanakuwa tayari kuchukua hatua kuhakikisha Watanzania wanakuwa na uhakika wa chakula licha ya hali iliyopo.
Chongolo amesema hilo limemsukuma pia kwenda kufanya ukaguzi wa hifadhi ya chakula katika maghala ya Chang’ombe jijini hapa, lengo likiwa ni kuhakikisha uwepo na usalama wake, ili akiwa anazungumzia hali hiyo, awe anauhakika na kile anachokizungumza kuhusiana na hifadhi ya chakula.
“Najua tuna akiba maeneo mbalimbali ya nchi, ilikuwa ni lazima nipite nijiridhishe uwepo wake, ili niwahakikishie watanzania kuwa serikali inaposema ina akiba ni kweli ipo.”
“Kwa kawaida akiba inayohitajika lazima itosheleze kulisha miezi sita ambayo ni tani 150,000 lakini sisi tuna akiba ya tani 555,000,” amesema Chongolo.
Amesema kwa sababu ya akiba iliyopo ni kubwa, ziada inayobakia inaweza kuuzwa huku NFRA ikisubiri msimu ujao itakapofungua dirisha katika msimu wa mavuno, iongeze.
“Masoko yapo ya kutosha pamoja na hili la ndani ya nchi, watu wananunua mahindi na kwenda kuzalisha unga wanaouza kwenye masoko mbalimbali, nasema masoko yapo kwani kazi kubwa imefanyika ikiwemo kufikia yale ya nchi jirani,” amesema waziri huyo.
Awali akizungumza katika ziara hiyo, Mkurugenzi wa NFRA, Andrew Komba amesema katika maghala ya Chang’ombe wanayo hifadhi ya chakula ya tani 25,000 licha ya kuwa na uwezo wa kuhifadhi tani 32,000.
“Kwa akiba tuliyonayo kama nchi inatosha kulisha miezi 18 itakapotokea uhaba ndani ya nchi, hifadhi hii ina chakula cha kutosha na kiko katika viwango vya ubora vinavyokubalika na kutambulika na taathibati za taasisi zinazofanya uhakiki wa usalama na ubora wa chakula ikiwemo Shirika la Viwango Tanzania,” amesema.
Amesema chakula hicho kikitumika kwa miezi 18 bado nchi itakuwa na ziada. Hivyo amewaalika wadau walio katika mnyororo wa usambazi wa chakula kwenda katika maghala yao, kununua chakula katika kanda zote tisa zilizopo ambazo ni Arusha, Shinyanga, Songwe, Songea, Dar es Salaam, Dodoma, Mpanda na Mpanda.
“Kote huko kuna chakula hivyo kama kuna upungufu katika soko waende katika ofisi zetu zilizopo katika kanda watauziwa chakula katika bei Rafiki na zinazoweza kuwafanya wananchi waondoe hali ya upungufu wa chakula unaoweza kutokea ndani ya nchi,” amesema.
Hata hivyo, hayo yanaelezwa wakati ambao Tanzania na Kenya zimeendelea kuimarisha uhusiano wa kibiashara katika mnyororo wa thamani wa nafaka, hususan mahindi meupe na mpunga kufuatia mazungumzo yaliyofanyika Januari 28, 2026.
Mazungumzo hayo yalifanyika wakati wa ziara rasmi ya ujumbe wa Tanzania ulioongozwa na Katibu mkuu wa Kilimo, Gerald Mweli ambaye alieleza kuwa Tanzania ina uzalishaji wa kutosha wa mahindi na tayari kuendelea kufanya biashara ya mahindi na Kenya kulingana na mahitaji ya soko la nchi hiyo.
Ujumbe wa Tanzania katika ziara hiyo ulifanya vikao na uongozi pamoja na timu za kitaalamu kutoka Wizara ya Kilimo ya Kenya, Agriculture and Food Authority (AFA) na Cereal Growers Association (CGA), ambapo walijadili mikakati ya kuimarisha biashara endelevu ya mazao ya nafaka, kuendeleza na kuimarisha akiba ya chakula ya kimkakati, pamoja na kuhakikisha usalama wa chakula katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Katika ziara hiyo, Mweli aliambatana na Balozi John Ulanga, Mkurugenzi wa Idara ya Diplomasia ya Uchumi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya NFRA.