Mwigulu ahimiza ushirikiano katika utunzaji na uhifadhi

Arusha. Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, ameagiza wadau wa utalii, uhifadhi na Watanzania kushirikiana na kuendeleza utekelezaji wa mikakati ya uhifadhi kwa maendeleo endelevu na uchumi wa taifa.

Aidha, amewataka Watanzania kuwa na utamaduni wa kuweka akiba ili waweze kufanya utalii wa ndani kwa kutembelea vivutio mbalimbali vilivyopo nchini badala ya kutegemea watalii wa nje pekee.

Dk Mwigulu ameyasema hayo leo, Jumamosi Januari 31, 2026, akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Arusha (TANAPA).

Mwigulu anatarajiwa kumwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika utoaji wa tuzo za utalii maarufu kama The Serengeti Awards usiku wa leo.

Amesema kuwa jukumu la kusimamia uhifadhi siyo la Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) pekee bali ni la wadau wote.

“Nitoe rai kwa wahifadhi na wadau kuhifadhi urithi huu ili na sisi tuwarithishe watoto wetu kama na sisi tulivyorithishwa; kila mmoja tuwajibike kuziendeleza lakini pia tutunze mazingira,” amesema na kuongeza:

“Nimeuliza gharama za Watanzania ni Sh 11,800; naona wanaweza kumudu kama tunavyoona mataifa ya nje wakija kufanya utalii. Haimaanishi ni matajiri, lakini wameweka utaratibu wa kufanya kazi mwaka mzima na wametenga siku za kwenda kwenye maeneo kama haya kuondoa stresi.”

“Utalii isiwe ni jambo la wageni toka nje ya nchi; ukishafanya kazi mwaka mzima, tenga sehemu ya kwenda kuona baraka hizi ambazo Mungu ametupa Watanzania. Wananchi pia mna wajibu wa kutunza rasilimali; si jambo la TANAPA peke yao. Hao tumewapa dhamana, lakini ni mali ya urithi kwa Watanzania—tutunze tuendelee kupata manufaa.”

Mmoja wa wadau wa utalii, Venance Lymo, amesema tuzo hizo zitaongeza thamani katika sekta hiyo na kutangaza Tanzania kimataifa katika utalii.

“Tuzo hizi zinaenda kuongeza thamani katika sekta ya utalii na kutangaza Tanzania kimataifa katika masuala ya utalii; zitahamasisha wawekezaji pia katika sekta hii muhimu inayoingizia Taifa letu mapato,” amesema.