:::::::::::
Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini (UNMISS) umeendelea kutambua na kuthamini mchango wa askari kutoka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wanaoshiriki katika operesheni za ulinzi wa amani nchini humo.
Katika hatua hiyo, askari wa Tanzania waliomaliza muda wao wa kuhudumu katika kikosi cha ulinzi wa amani cha UNMISS wamepongezwa kwa kazi nzuri waliyofanya ya kudumisha amani na usalama kwa kipindi chote cha utumishi wao, huku wakikabidhiwa vyeti vya kutambua mchango wao.
Akizungumza kwa niaba ya maafisa, wakaguzi na askari wa vyeo mbalimbali kutoka Tanzania, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Sarah Reuben Bundala amesema kuwa furaha yao kubwa ilikuwa ni kuendeleza juhudi za ulinzi wa amani walipoishia kikosi kilichowatangulia, jambo lililosaidia kudumisha mwendelezo wa amani nchini Sudan Kusini.
SSP Bundala ameongeza kuwa katika kipindi chote cha utumishi wao, askari wa Tanzania wamejivunia kupeperusha vyema bendera ya taifa, huku wakitumia fursa hiyo pia kutoa elimu kuhusu ukatili dhidi ya watoto na wanawake, ambao mara nyingi huwa waathirika wakubwa wa migogoro na vita.
Aidha, ametumia nafasi hiyo kuwashukuru askari kutoka mataifa mbalimbali wanaoshiriki operesheni za UNMISS kwa ushirikiano wao mzuri uliosaidia kuleta matumaini na tabasamu kwa wananchi wa Sudan Kusini.





