Dakika tisini za uamuzi Simba, Azam, Singida zikijitupa uwanjani

KABLA ya jua kuzama leo Jumapili, Wanasimba watakuwa wamefahamu chama lao litakuwa katika hali gani kunako kundi D la Ligi ya Mabingwa Afrika kwani litakuwa na mechi ya uamuzi dhidi ya Waatabu kutoka Tunisia, Esperance.

Umuhimu wa mechi hiyo umewafanya wachezaji na benchi la ufundi la Simba kutangaza kujitoa kwa kila hali kuhakikisha hakuna matokeo mengine yanayopatikana zaidi ya ushindi.

“Ni mchezo ambao tunahitaji matokeo ya ushindi pekee,” hiyo ni kauli ya msisitizo kutoka kwa kiungo mshambuliaji wa Simba, Morice Abraham akizungumzia mechi dhidi ya Esperance itakayoanza saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Simba ina kibarua cha kusaka ushindi mechi hiyo kwani ikipata matokeo tofauti na hayo kwa maana ya sare au kupoteza, suala la kufuzu robo fainali litakuwa gumu na kutibua rekodi iliyoiweka tangu mwaka 2018.

“Morali ya wachezaji iko juu, kwa sababu kila mtu anajua umuhimu wa mchezo wa kesho (leo). Kila mmoja ana hamu ya kuona tunakwenda kucheza hatua ya robo fainali katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa.

“Ukiangalia haya ni mashindano makubwa na ni nafasi kubwa kwetu wachezaji kwani unapofika mbali ndiyo njia zaidi zinaonekana na tunazidi kuitangaza nembo ya klabu yetu maeneo makubwa duniani. Tumejiandaa kwani tunaamini mchezo wa kesho (leo) utakuwa mgumu.

“Kila mchezaji anatambua hali tuliyonayo kwa sasa, tumeanza vibaya lakini tuna nafasi ya kumaliza vizuri, hilo ndiyo jambo zuri. Ni bora ukaanza vibaya na kumaliza vizuri kuliko kuanza vizuri na kumaliza vibaya,” alisema Abraham.


Saa 10:00 jioni leo Jumapili kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, dakika tisini zitaamua hilo ambalo Abraham amezungumza pale Simba inayoburuza mkia wa kundi D la Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa haina pointi, itakapoikaribisha Esperance yenye pointi tano.

Wakati Simba ikisaka pointi tatu za kwanza, Esperance kwao hata sare ina faida kwani itafikisha pointi sita zinazoiweka timu hiyo kwenye nafasi ya kufuzu robo fainali ikibakiwa na mechi mbili ikiwamo moja ugenini na nyingine nyumbani ile ya kuhitimisha makundi.

Kabla ya wakali hao kuumana leo, jana usiku ilipigwa mechi kati ya vinara wa kundi Stade Malien yenye iliyokuwa na pointi saba iliyoifuata Petro Atletico ambayo ilikuwa na nne.

Simba inayopambana kushinda mechi tatu zilizobaki hatua ya makundi ili kufikisha tisa zinazoweza kuivusha robo fainali, inapambana kulinda rekodi yake ya michuano ya CAF kwani tangu mwaka 2018 ilipofuzu makundi, haijawahi kuishia hapo, lazima ipenye robo fainali huku ikishuhudiwa 2024-2025 ikifika hadi fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Hata hivyo, Simba wakati inapambana kufanya maajabu hayo, rekodi zinaonyesha katika michuano hiyo, hakuna timu iliyowahi kupoteza mechi tatua mfululizo za mwanzoni hatua ya makundi, kisha ikafuzu robo fainali.

Maboresho ya kikosi cha Simba kwa kuingiza wachezaji wapya kipindi cha usajili wa dirisha dogo kimeonekana kufanya mabadiliko makubwa ya kiuchezaji huku mechi iliyopita dhidi ya Mashujaa katika Ligi Kuu Bara ikiibua hisia mpya.

Simba ilipoichapa Mashujaa 2-0 huku usajili mpya Libase Gueye akipachika bao la kwanza na kusababisha penalti ambayo ilikoswa na Kibu Denis, kabla ya Seleman Mwalimu kuongeza bao la pili, kimewafanya Wanasimba kurudisha imani na timu yao.


Pia hata kocha wa Simba, Steve Barker amesema: “Usajili ulioufanyika utairudisha Simba ambayo mashabiki na viongozi wanaitaka, ambapo sasa hatua inayokwenda ni kuendelea kuwaunganisha wachezaji ili kuelewana, hasa wanapokuwa uwanjani kutokana na nafasi zao.”

Ushindi wa nyumbani katika mechi ya wikiendi iliyopita kwenye kundi C la Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya AS Otoho, umeibua matumaini makubwa kwa Singida Black Stars ambayo leo saa 10:00 jioni itakuwa pale Uwanja wa Alphonse Massemba-Débat uliopo Brazzaville nchini Congo kurudiana na wapinzani wao hao.

Singida inatazamia kusaka pointi nyingine katika mechi hii ili kuzidi kujiimarisha katika msimamo wa kundi C baada ya kuwa nazo nne sawa na Stellenbosch ambayo nayo inacheza dhidi ya vinara CR Belouizdad. Kumbuka AS Otoho inazo tatu, hivyo nayo inazitolea macho pointi za leo.

Uzuri wa kundi hili ni kwamba, kila mmoja anatambia uwanja wake wa nyumbani, hakuna timu iliyokuwa nyumbani ikapoteza, imetokea mara moja tu Singida ikilazimishwa sare na Stellenbosch, lakini zingine zote zilizokuwa nyumbani zimeshinda.


Mara ya mwisho AS Otoho kucheza nyumbani hatua ya makundi iliichapa CR Belouizdad mabao 4-1, hivyo Singida licha ya kushinda mechi iliyopita, ina kibarua kigumu leo cha kuhakikisha haipati matokeo mabaya ili kuzidi kuchonga barabara ya kufuzu robo fainali kwa mara ya kwanza baada ya kufanya hivyo ilipotinga makundi.

Jeshi la Singida linaloongoza na Kocha David Ouma, linaweza kuanza namna hii kutokana na umuhimu wa mechi yenyewe; Amas Obasogie, Abdulmalick Zakaria, Kennedy Juma, Morice Chukwu, Khalid Aucho, Idriss Diomande, Khalid Habib ‘Gego’, Emmanuel Keyekeh, Elvis Rupia, Lamine Jarjué na Joseph Guede.

WAKENYA WALIVYOSHIKA FUNGUO YA AZAM

Baada ya Azam kufuzu makundi kwa mara ya kwanza katika michuano ya CAF tangu ilipoanza kushiriki mwaka 2013, sasa inatazamia kufika mbali zaidi ikiwemo robo fainali, hatua inayofuata baada ya sasa.

Katika kufikia rekodi hiyo, ufunguo wake upo kwa Wakenya, Nairobi United ambayo haina pointi katika kundi B la Kombe la Shirikisho Afrika.


Hata hivyo, Azam inahitaji kufanya kazi ya ziada kuhakikisha haipotezi pointi kirahisi mechi tatu zilizobaki ikianza na leo ya nyumbani dhidi ya Wakenya hao kwenye Uwanja wa New Amaan Complex uliopo Zanzibar kuanzia saa 1:00 usiku.

Wikiendi iliyopita, Azam ikiwa ugenini nchini Kenya iliichapa Nairobi United mabao 2-1 na kuweka rekodi ya kushinda mechi ya kwanza hatua ya makundi kwani kabla ya hapo ilifungwa mbili za awali dhidi ya AS Maniema (2-0 ugenini) na Wydad (1-0 nyumbani).

Pointi tatu za Azam ilizopata ugenini, zimeibua matumaini ya kufuzu robo fainali, lakini ikizipata tatu nyingine za leo zitaiweka pazuri zaidi huku hesabu zikihamia mechi mbili zitakazobaki, nyumbani dhidi ya AS Maniema na ugenini ikienda kuikabili Wydad.

AS Maniema baada ya kuchapwa 1-0 na Wydad mechi iliyopita, leo itakuwa nyumbani kuwakaribisha Waarabu hao wa Morocco wenye pointi tisa, wakiusogelea karibu zaidi mlango wa kutinga robo fainali.

Kwa Maniema iliyoonesha uwezo wa kushinda nyumbani na ugenini ilipoichapa Azam 2-0 na Nairobi United 1-0, si ya kuichukulia poa. Lolote linaweza kutokea dhidi ya Wydad leo pale DR Congo.

Kocha Mkuu wa Azam FC, Florent Ibenge, alisema: “Wakati tunaanza mechi hizi za makundi, tulikuwa na malengo ya kushinda mechi zetu tatu za nyumbani, bahati mbaya tukapoteza ya kwanza dhidi ya Wydad.

“Bahati nzuri kwetu ushindi wetu wa kwanza tumeupata ugenini lakini umetuimarisha, sasa tunataka kushinda hizi mbili za nyumbani tulizobakiza.

“Tunafahamu haitakuwa rahisi tunakutana na timu ambayo inaweza kubadilika,hatutaki kurudi nyuma tena, tumejiandaa kushinda kwenye mchezo huu wa kesho.”

Wakati Ibenge akisema hayo, kocha wa Nairobi United, Salim Ramadhan, alisema kikosi chake licha ya kupoteza mechi tatu za kwanza, bado wataendelea kujipanga kutafuta ushindi wa kwanza.

Ramadhan amesema timu hiyo haiwezi kukata tamaa kwa kuwa bado nafasi wanayo kuweza kutafuta nafasi za juu.

“Tumekuwa na matokeo mabaya lakini kiwango chetu kimekuwa tofauti, naamini tunaweza kubadilika tutaendelea kutafuta ushindi kwenye mechi zilizosalia,” alisema Ramadhan.

“Changamoto yetu kubwa tumekuwa na wachezaji ambao wanapata uzoefu lakini tunajivunia namna wanavyoendelea kuimarika na hatutaki kukata tamaa.”