ONGEA NA ANTI BETTIE: Mama anamchukia mume wangu tunayependana

Nimeolewa huu mwaka wa pili, kwa bahati mbaya wakati ninafunga ndoa na mume wangu mama yangu alikuwa masomoni nje ya nchi, alifahamishwa kuhusu ndoa hiyo akashindwa kurudi kwa sababu mbalimbali na nilijitahidi kumuonyesha mume wangu na walikuwa wakizungumza kupitia video call.

Mara kadhaa alikuwa anataka kujua anafanya shughuli gani akawa anamjibu ni mtaalamu wa kompyuta bila kufafanua.

Alipomaliza masomo akarudi nchini na kutukuta mimi na mume wangu tunafanya biashara ingawa bado haijafikia hatua kubwa.

Akaanza malalamiko kuwa sikufanya uchaguzi sahihi, nitapata taabu, mara hamuelewi mume wangu. Kwa kifupi kuanzia hapo ni manyanyaso, dharau na kejeli kwa mume wangu zisizovumilika.

Amefikia mahali tukikutana naye kwenye shughuli za kifamilia anamsema kwa ndugu, jamaa na marafiki kuwa haeleweki na hampendi.

Hii hali inanipunguzia mapenzi kwa mwenza wangu ambaye tulikuwa tunapendana sana na ninamuelewa pengine kuliko mwanaume yeyote.

Pole kwa haya unayopitia, ila nakusihi usije kukwazana na mama yako kwa namna yoyote ile, maana ni mzazi wako.

Kujinasua katika mtanziko huo fanya hivi.

Kwanza kabisa, ni muhimu ujiambie jambo moja la msingi ndoa yako ni yako na ya mume wako, si ya mama yako wala ya mtu mwingine yeyote.

Maoni ya wazazi ni ya kusikilizwa, lakini hayapaswi kuwa hukumu ya mwisho juu ya maisha yako ya ndoa, hasa pale yanapogeuka kuwa manyanyaso, dharau na kuvunja heshima ya mwenza wako.

Ni wazi kabisa kuwa kabla mama yako hajamfahamu mume wako kwa karibu, tayari ameunda taswira hasi akilini mwake labda kwa matarajio yake binafsi, labda kwa hofu, au labda kwa viwango alivyokuwa amejijengea kuhusu mwanaume anayekufaa.

Tatizo kubwa hapa si biashara yenu, wala taaluma ya mume wako, bali ni kukosa kwake kukubali uchaguzi wako.

Unapomruhusu aendelee kumdhalilisha mume wako hadharani, taratibu unaruhusu mizizi ya chuki iingie kwenye ndoa yako na kupunguza mapenzi uliyokuwa nayo, jambo ambalo tayari unaanza kulihisi.

Lazima uchukue msimamo wa ndani kwanza. Jiulize kwa uaminifu je, nampenda mume wangu? Je, nina amani naye? Je, ninaona maisha yangu ya baadaye yako salama na yeye?

Kama majibu ni ndiyo, basi hapo ndipo uamuzi wako unapaswa kusimama.

Usikubali kumpoteza mwanamume unayempenda kwa sababu ya shinikizo la familia, hata kama shinikizo hilo linatoka kwa mama yako mzazi.

Wazazi wanapaswa kulinda ndoa za watoto wao, si kuzivunja.

Muhimu sana uweke mipaka. Heshima haimaanishi kukubali kudhalilishwa. Zungumza na mama yako kwa utulivu lakini kwa msimamo.

Mwambie wazi kwamba unamuheshimu, lakini hukubaliani na kauli zake juu ya mume wako.

Mwambie kwamba maneno yake yanakuumiza wewe kama binti yake na yanaharibu ndoa yako. Usijitetee kupita kiasi weka msimamo, si mjadala.

Kwa hatua ya vitendo, ni busara kupunguza ukaribu wa kihisia na mawasiliano yanayokupa maumivu.

Hii haimaanishi kumkataa mama yako, bali kulinda ndoa yako. Si lazima kila jambo la ndoa yako lijadiliwe na mama yako.

Si lazima kila mkutano wa kifamilia uhudhuriwe kama unajua utageuka kuwa jukwaa la kumdhalilisha mume wako.

Familia ya ndoa mume wako sasa ndiyo kipaumbele chako cha kwanza.

Zaidi ya yote, simama upande wa mume wako. Mwanamume anayedharauliwa na mkwe bila ulinzi wa mke wake huanza kupoteza heshima, motisha na hata mapenzi.

Ukimruhusu mama yako kuendelea, hatimaye utaamka siku moja ukigundua umeharibu ndoa mwenyewe kwa mikono yako, si kwa sababu mume wako alishindwa, bali kwa sababu hukumlinda.

Kumbuka: ndoa ni ahadi ya wawili, si kura ya maoni ya familia. Linda ndoa yako, linda mapenzi yako, na linda uamuzi wako. Mama atabaki kuwa mama yako, lakini mume wako ndiye mwenzi wako wa maisha.