POLISI KUTOKA TANZANIA VINARA WA KUTOA ELIMU YA KUPINGA UKATILI SUDAN KUSINI

::::::::::

Askari wa Jeshi la Polisi kutoka Tanzania wanaoshiriki katika operesheni za ulinzi wa amani nchini Sudan Kusini wameendelea kuonyesha umahiri mkubwa katika kupambana na vitendo vya ukatili, hususan kwa kutoa elimu kwa jamii zilizoathirika. Hatua hiyo imechangia kwa kiasi kikubwa kupungua kwa matukio ya ukatili katika maeneo wanayohudumia.

Miongoni mwa askari hao ni Koplo wa Jeshi la Polisi Tanzania, CPL Diana Launoni Laizer, kutoka Ofisi ya GCVPP (Gender, Children and Vulnerable People Protection), ambaye ametambulika kwa kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa katika utoaji wa elimu kuhusu masuala ya ukatili wa kijinsia. Jitihada zake zimepelekea kupungua kwa idadi ya matukio ya ukatili yanayoripotiwa katika eneo la operesheni ya ulinzi wa amani Sudan Kusini.

Akizungumza kuhusu kazi hiyo, CPL Laizer amesema kuwa elimu ya kupinga ukatili imekuwa ikitolewa kwa makundi yote ya jamii, huku msisitizo mkubwa ukiwekwa kwa wanawake na watoto, ambao ndio wahanga wakubwa wa vitendo vya ukatili katika maeneo yenye migogoro na ukosefu wa amani.

Aidha, CPL Laizer ambaye pia ni kiongozi wa masuala ya jinsia, wanawake na watoto katika ofisi hiyo, ndiye askari pekee kutoka Tanzania aliyepata kutambulika na kupongezwa rasmi kwa mchango wake mkubwa katika kutoa elimu ya kupinga ukatili. Kupitia juhudi hizo, jamii nyingi za Sudan Kusini zimeongeza uelewa na kuanza kuacha mara moja vitendo vya ukatili.