Mitandao inavyowapa hofu vijana kuoa, kuolewa   

Hadithi na simulizi za kusalitiana, ugomvi, hekaheka, kukosa uhuru na amani zinazotolewa katika mitandao ya kijamii zinaweza kuwa miongoni mwa sababu zinazowafanya baadhi ya vijana kuingia katika taasisi hiyo?

Katika mitandao hiyo ya Instagram, X, Facebook na TikTok zinapokuja mada na simulizi za uhusiano zinazopata uungwaji mkono kwa wingi ni zile zinazohusu changamoto kiasi cha wachangiaji kuandika maoni yenye hofu kwamba ‘Kwa haya wanayozungumza wanandoa na wapenzi nitaoa kweli?’

Zamani, kijana akifikisha umri wa kuanza maisha, swali la kwanza alilokutana nalo kutoka kwa wazee na marafiki lilikuwa: “Lini tunakula ubwabwa?” Lakini leo, hali imebadilika. Ukiuliza swali hilo, unaweza kukutana na majibu yaliyojaa hofu, kejeli, au ukimya mzito.

Katika miaka ya hivi karibuni, taswira ya taasisi ya ndoa imekuwa ikipita katika kipindi cha mpito chenye changamoto nyingi.

Wakati zamani ndoa ilionekana kama kilele cha mafanikio ya kijamii na kiroho, leo hii simulizi zinazotawala vijiwe vya kahawa na kurasa za mitandao ya kijamii zimegeuka kuwa ‘shubiri’ inayowafanya baadhi ya vijana kusita kuvuka mstari huo.

Uwepo wa habari hasi, ushuhuda wa usaliti, na malalamiko ya wapenzi na wanandoa, vimejenga hofu ya pamoja ambayo inatishia mustakabali wa familia mpya.

Leo hii, kijana akiamka asuhubuhi, anakutana na ‘screenshot’ ya mazungumzo ya siri ya mume wa mtu akisaliti, au video ya mwanamke aliyefumaniwa.

Maoni yanayofuata chini ya habari hizo ndiyo sumu halisi.

Ukweli ni kuwa unapokutana na maoni mengi yanayosema ‘Wanaume wote ni mbwa’ au ‘Wanawake mbona hawaridhiki’, akili yako inaanza kuamini kuwa huo ndio ukweli uliopo huku ukianza kujenga hofu akilini bila wewe kujua.

Kwa sababu kijana ambaye hajaingia kwenye ndoa na hajawahi kusaliitiwa anaanza kuhisi maumivu ya hayo anayoyasoma.

Duniani kote, wataalamu wameanza kuona kuwa kuna “janga la hofu” ( linalotokana na jinsi tunavyozungumza kuhusu ndoa

Mmoja wa watu mashuhuri ambaye amechambua jambo hili kwa kina ni Alain de Botton, mwanafalsafa na mwandishi maarufu raia wa Uswisi anayeishi Uingereza.

Alain de Botton anasema kuwa sababu kubwa inayofanya watu walioko kwenye ndoa kutoa maoni hasi na kukatisha tamaa wengine ni kwa sababu walijengewa “picha ya uongo” kuhusu ndoa na vyombo vya habari na filamu.

Kuna kundi la wanandoa ambao wamekuwa ‘mabalozi wa giza’. Hawa ni wale ambao kila wanapokutana na vijana ambao bado hawajaingia kwenye ndoa, badala ya kutoa hamasa, hutoa onyo.

“Usikimbilie huku, baki huko huko nje unakula upepo. Huku ndani ni moto,” ni kauli zinazosikika mara kwa mara kwenye vijiwe vya kahawa na saluni za kike.

Hawa ni watu walioko ndani ya ndoa lakini wanaziponda hadharani. Maneno yao yana uzito mkubwa kwa sababu yanatoka kwa watu waliomo ndani, hivyo yanachukuliwa kama ripoti ya ujasusi kutoka uwanja wa vita.

Mwingine ni mwanasaikolojia mashuhuri wa nchini Marekani mwenye asili ya Ubelgiji, Esther Perel, ambaye ni mtaalamu wa masuala ya usaliti na uhusiano. Katika kitabu chake The State of Affairs, Esther anaeleza jambo linaloitwa ‘The Crisis of Expectation’ (Mgogoro wa matarajio).

Matokeo ya wanandoa walioshindwa wanajikuta wanatoa shuhuda za kukatisha tamaa kwenye mitandao, wakisema ndoa ni mbaya. Esther anasema hizi simulizi hasi zinafanya kizazi cha sasa kione kuwa ndoa ni “mzigo usioweza kubebeka,” hivyo kuamua kubaki wapweke au kuishi bila ndoa rasmi.

Kijana Mathew Sebastian kutoka Dar es Salaam anasema maoni na simulizi hasi za wanandoa mitandaoni, zinaweza kuwafanya watu, hasa vijana, kuogopa kuingia kwenye ndoa kwa sababu huzidisha picha ya matatizo kuliko uhalisia.

“Hata hivyo, simulizi hizo haziwakilishi ndoa zote, nyingi ni za waliokumbwa na changamoto. Badala ya kuua imani, zinapaswa kuchukuliwa kama funzo juu ya umuhimu wa maandalizi, mawasiliano na uchaguzi sahihi wa mwenzio,” anasema.

Zaitun Rashid kutoka Dodoma anasema yeye ni mtumiaji sana wa Instagram na anapenda akaunti zinazoweka shuhuda nyingi kuhusu machungu hasa ya wapenzi, kitu ambacho kimemjengea hofu kuingia katika uchumba.

Lakini Rachel Michael anasema yeye hatilii maanani yale yanayozungumzwa bali ataingia kwenye ndoa, kwani anaamini kila jambo lina changamoto zake hivyo hatoshindwa.

Annastazia Joseph kutoka Dodoma aliyedumu kwenye ndoa miaka 25 kabla ya kufiwa na mumewe, anasema kinachokosewa ni uwazi unaotolewa kwenye mitandao ya kijamii jambo ambalo zamani halikuwepo.

“Tuliweza kuvumilia yaliyomo ndani na hatukuweza kutangazwa popote sio kwamba changamoto hazikuwepo bali tuliamua kuzimezea kitu ambacho ni tofauti na sasa. Nashauri waache kutoa machungu yaliyopo bali wajikite kutoa raha na amani ili kutowavunja moyo wengine,” anasema.

Wanasaikolojia wanashauri haja ya kurudisha simulizi chanya za ndoa. Badala ya kuangazia tu pale ambapo ndoa imevunjika, jamii inapaswa kuangazia pia ndoa zilizofanikiwa na jinsi zilivyoweza kuvuka vikwazo.

Pia, kuna haja ya kupunguza presha ya kijamii kuhusu harusi za kifahari. Ndoa inapaswa kutazamwa kama muunganiko wa watu wawili wenye malengo, na si shindano la nani kafanya sherehe kubwa mjini.

Wataalamu wanashauri ipo haja ya kurudisha heshima ya ndoa kupitia elimu ya kisaikolojia kabla ya ndoa, ambayo haizingatii tu dini, bali uhalisia wa maisha ya sasa.